MIFUKO HIFADHI YA JAMII ISIGEUZWE UPATU – WATAALAMU
*Wasema “itakuwa kama DECI – wastaafu wa sasa kutakata, wa kesho chali”
Na
Mwandishi Wetu, Arusha.
UNAWEZA
kushangaa pale ambapo Shirika la Kazi Duniani, ILO, linawalalamikia viongozi wa
Chama cha Wafanyakazi Tanzania, TUCTA, kwamba wanaua mifuko ya hifadhi ya jamii
nchini, baada ya kupandisha kikokotoo.
Kwa
nini ILO wawalalamikie TUCTA wakatii kikokotoo kimepanda juu sana kuliko taifa
lolote duniani, hata kuyazidi mataifa yote yenye uchumi mkubwa zaidi duniani
kama Marekani, China, Ujerumani, Uingereza, Japan, Ufaransa na hata Afrika ya
Kusini?
Shirika
la kazi Duniani liliona Kikokotoo cha asilimia 50 kilikuwa kinakwenda kuifilisi
mifuko ya hifadhi ya jamii. ILO wenyewe wakalalamika. Hata Kikokotoo chetu cha
sasa cha asilimia 33, ILO wametuweka kwenye uangalizi (red flag).
Hata
hivyo, kwa huruma tu, tunaweza kupanda kidogo, iwapo Serikali itaamua kuingiza fedha
zake, jambo ambalo linahitaji uangalifu mkubwa. Labda elimu ya kina itolewe kwa
watanzania na wapotoshaji wadhibitiwe.
Ongezeko
dogo linaweza kuwa himilivu kwa ufadhili wa Serikali, kiubishi, kwa ubinadamu
tu, lakini pia kwa uangalifu mkubwa sana.
“Wakati
mifuko inaunganishwa, uhai wa mfuko wa PSPF uliokuwa unalipa kikokotoo cha
asilimia 50, ulikuwa umebakia miaka 11 tu ufe. Hii ina maana kuwa, baada ya
miaka 11, kusingekuwa na mfuko wa pensheni wa watumishi wa umma. Ukwasi wake
ulikuwa taabani,” alisema mbobezi wa hifadhi ya jamii nchini, Dkt. Aggrey
Mlimuka.
Wakati
PPF na NSSF zilizokuwa zinalipa kwa kutumia Kikokotoo cha asilimia 25, zilikuwa
na uhai wa maelfu ya miaka. Hivyo, kuijumuisha mifuko na kurekebisha kikokotoo,
kumeuongezea mfuko huu uhai wa miaka mingi zaidi.
Wabobezi
hao walikuwa wakiongea katika mjadala wa Kikokotoo uliofanyika kwa kutumia
mtandao wa kijamii.
Wakumbushia
Majuto ya Malipo Makubwa ya Mkupuo
“Sisi
wengine tulionja chungu ya “provident fund,” mifuko ya akiba (ni tofauti na
mifuko ya pensheni, kwenye akiba unatunza na kupewa ulichoweka na kifaida kidogo)
na mkupuo wa mara moja. Ni wale tuliorithi mfuko wa University of East Africa
ulioitwa Senior Staff suprennuation Scheme (SSSS),” alionya Mwanazuoni mmoja
mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aliendelea,
“usiombe! Afadhali sisi waajiriwa wa 1976 na 1977, tuliokolewa kwa kuongezewa
ruzuku ndogo na Serikali kupitia PPF. Waliotutangulia walilia sana. Mkupuo
mmoja ni mbaya sana,” aliongeza.
Mhadhili
huyo mstaafu aliyeandika vitabu vingi vya kitaaluma na mshauri wa kimataifa,
alisema kujadili ongezeko la mkupuo si vibaya, lakini mantiki inaelekeza ongezeko
hilo lisiwe kubwa ili malipo ya kila mwezi baadaye yawe na maana,” aliongeza.
Wahenga
walisema uzee dawa. Dkt. Mlimuka, sasa mstaafu, lakini anayetumika kushauri
mifuko ya hifadhi ya jamii, mwenye miaka
mingi ya uzoefu katika sekta ya hifadhi ya jamii, nchini na nje ya nchi,
alikumbushia yaliyotokea miaka ya nyuma.
“Baadhi
ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), waliokataa kujiunga na
PPF ili wapate pensheni ya kila mwezi, mpaka leo walikuwa wanajutia maamuzi yao,”
alisema.
Aliongeza
kwamba, wafanyakazi hao, wengi wakiwa wahadhiri, walichagua kuendelea na mfuko
wa akiba wa SSSS, ambapo walipata mkupuo mmoja mkubwa na hawana pensheni hadi
leo.
“Kwa
mfanyakazi aliyezoea kupata mshahara wa kila mwezi, pensheni nzuri ya kila
mwezi ni bora kuliko malipo ya mkupuo, ambayo mara nyingi huisha mapema,”
aliongea kutokana na uzoefu wa tasnia hiyo.
Naye
mtaalamu wa sayansi ya mahesabu (Actuarial Scientist), Phostine Oyuke, alitoa
ushauri kwa waastaafu watarajiwa.
“Wenzangu
ambao tuna miaka 10-20 kustaafu, tukijaaliwa, tunadhani mkupuo ni suluhu.
Provident funds hazijawahi kusaidia kwenye stability ya social security popote.
Haya mambo yamefanyiwa tafiti duniani kote,” alisema.
Bw
Oyuke ambaye ni Actuarial na amebobea katika fani ya bima, aliongeza, “Niseme
tu, iwapo mtu anataka kikokotoo kipande zaidi ya hapo, maana yake, anataka
kuigeuza mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa upatu, “ponzi schemes”, yaani
wachangiaji wa mwanzo wapate wa mwisho wakose,” aliongeza.
Bw
Oyuke alisema wastaafu wataathirika sana iwapo, baada ya kutafuna mkupuo wote,
wakiwa hawana kipato cha kukidhi walau mahitaji yao ya kila siku.
Hifadhi
ya Jamii sio UPATU
Mtaalamu
huyo alisema kuwa hifadhi ya jamii haipaswi kuwa UPATU (pyramid Scheme) kama
ilivyokuwa DECI. “Watu wazima tunakumbuka wazazi wetu walilipwa mkupuo mmoja,
lakini walilalamika ili walipwe kidogo kidogo,” alikumbusha.
Mwanasayansi
huyo alitabiri kuwa, iwapo kikokotoo kitapanda na kulipa kiinua mgongo cha asilimia
50, upo uwezekano kuwa ndani ya miaka 7 hadi 10 hakutakuwa na mifuko ya hifadhi
ya jamii.
“Mimi
sina tatizo na kikokotoo cha asilimia 33, ni kizuri na wapo wafanyakazi wengi
wake comfortable [wanaridhika] nacho, ikifika tarehe 25 ya kila mwezi, muamala
unasoma,” alisema Bw Junus Ndaro, Katibu Mtendaji wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta
ya Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (TEWUTA).
Wastaafu
walikuwa wanasubiri hadi miaka mitatu bila kulipwa
Mwanasayansi
mmoja mwenye uzoefu wa hifadhi ya jamii nchini alibainisha kuwa, kabla ya
kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2018, mfuko wa PSSSF ulikuta
wanachama elfu kumi (10,000) waliokuwa wanalipwa kwa kikokotoo cha mkupuo cha asilimia
50, wanasubiri kulipwa kwa zaidi ya miaka miwili hadi mitatu baada ya kustaafu.
Mtaalamu
huyo ambaye pia ni actuarial, anasema kuwa baada ya kushusha kikokotoo hadi
asilimia 33, sasa wastaafu wanasubiri mafao yao kwa siku 60 tu na juhudi
zinaendelea kufanywa ili walipwe mkupuo wao ndani ya siku 30 tu baada ya
kustaafu.
Hii
ni kwa sababu kikokotoo cha 33 ni himilivu. Kikokotoo kikiwa kikubwa sana
kuliko uwezo, wastaafu wanaweza kurejea kwenye hali ya zamani ya kusubiria kwa
miaka, wakisugua lami, kama ilivyokuwa akina mama wakisubiria maji ya chemchem
kisimani yajae ili wachote.
“Watanzania
wanapotoshwa na baadhi ya wanasiasa wasio wataalamu wa mahesabu,” alisema mmoja
wa walimu walioshiriki semina ya kikokotoo, Mwalimu Joseph Laurenti wa Arusha.
Mikupuo
Ilivyowatesa Wastaafu wa Kiltex
Miaka
kadhaa iliyopita, walikuwepo wastaafu wa kiwanda cha nguo cha Kilimanjaro (Kiltex)
ambao kwa wakati huo, waliruhusiwa kuchukua fedha zao zote.
“Bila
hiana, nao walichukua, wakaondoka kwa furaha tele na bashasha za kutosha. Baada
ya mwaka mmoja, wote wakarudi kwa umoja wao, wakiomba warudishwe kwenye
pensheni ya kila mwezi, wakaambiwa kuwa hilo lisingewezekana kwa kuwa
walishachukua fedha zao zote, wakalalamika sana maisha magumu. Hadi leo bado
wanalilia jambo hilo,” alisema Dkt. Mlimuka ambaye kwa miaka mingi alikuwa
Mtendaji Mkuu wa chama cha waajiri Tanzania (ATE).
“Mimi ninayepokea pensheni ya kila mwezi, hata ukiniambia leo nipewe fedha zilizobaki, siwezi kukubali, kwa kuwa ninajua adha ya mkupuo na raha ya kupokea pensheni kila mwezi,” aliongeza mbobezi huyo.
Mwandishi
wa Makala haya ni mchangiaji wetu na mtafiti katika eneo la hifadhi ya jamii.
Anapatikana jijini Arusha, Tanzania.
Comments
Post a Comment