Saturday, July 24, 2021

VIFAA TIBA NA WATAALAMU ZAIDI WA AFYA YA KINYWA NA MENO WAHITAJIKA PWANI

 Hayo yamebainishwa leo Julai 24,2021 na Mhe Abubakar Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Pwani wakati akitoa salaam kwenye Shughuli ya Utoaji Elimu, Uchunguzi wa Matibabi ya Afya ya Kinywa na Meno kwa Wananchi wa  Kijiji cha Msoga Halmashauri ya Chalinze, shughuli iliyofanyika katika Viwanja vya Hospital ya Msoga.

"Huduma za Afya ya kinywa na Meno zinatolewa katika Halmashauri zote 9 za Mkoa, Mkoa una vituo 39 unazotoa huduma hizo, Kama Mkoa unaendelea na juhudi kuhakisha Hospital zote za Halmshauri zinakuwa na Vifaa tiba za  kutosha ikiwemo Wataalamu na  Upatikanaji wa Huduma ya Dental Exray kwenye Hospital zetu.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno Dk. Deogratus Kilasara Ameeleza kuwa Mkoa huo umefanya Vizuri katika utoaji wa huduma ya Afya ya Kinywa na Meno kwa kuwa huduma hii inapatikana katika Vituo 39 Kati ya vituo 298 vya Serikali. "Huduma hii inapatika kwa asilimia 13 kulinganisha na huduma zingine za afya na ipo juu kulinganisha na hali ya kitaifa ambayo hadi sasa ni asilimia 7. Ameeleza Mkoa pia unakabiliwa na uhaba wa Wataalam na Vifaa tiba


Naye Mgeni Maalumu kwenye Hafla hiyo Rais Mstaafu awamu ya nne Dkt. Jakaya  Mrisho Kikwete amesema " bado kuna mahitaji makubwa ya kuimarisha huduma ya Afya ya kinywa na Meno katika Halmashauri ya Chalinze na Mkoa wa Pwani, ameongeza kuwa bado ipo kazi ya kuendelea kutafuta Vifaa tiba ikiwemo Dental Exray kwa Hospital nane za Halmshauri za Mkoa huo, ambayo  kwa Sasa ipo moja tu kwa Mkoa mzima katika Hospital ya Wilaya ya Mafia" Ameeleza kuwa kupatikana kwa vifaa tiba na wataalam ni jambo linalowezekana amewataka kuendelea kujipanga kutatua Changamoto hiyo.

SHEHENA YA CHANJO DHIDI YA CORONA YAWASILI NCHINI

CHANJO dozi Milioni Moja ya Covid-19, imewasili nchini leo Jumamosi Julai 24, 2021.

Shehena ya Chanjo hiyo aina ya Johnson & Johnson imetolewa na serikali ya Marekani kama msaada chini ya Mpango wa COVAX, ubalozi wa Marekani nchini umesema.

Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, shehena hiyo imekabidhiwa kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Waziri wa Afya, Dkt  Dorothy Gwajima na Balozi wa Marekani nchini, Dkt.Donald Wright.


Friday, July 23, 2021

MAJALIWA: TUTAMALIZA TATIZO LA UPATIKANAJI WA MAJI NCHINI

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vya wilaya ya Ruangwa, Lindi.

Amesema suala la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika awamu hii, hivyo suala la upatikanaji wa huduma ya maji ni endelevu. “Tutaendelea kuboresha miradi ya maji ili maeneo yote nchini yapate maji ya uhakika.”

Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Julai 23, 2021) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji vya Mpara, Mtimbo, Mmawa, Chikoko, Chinokole na Kilimahewa wilayani Ruangwa.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi. Amewataka waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imedhamiria kuwatumikia.

Akizungumzia kuhusu tatizo la maji wilayani Ruangwa amesema Serikali inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ambao unatoa maji Ndanda hadi Ruangwa. “Mradi huu mkubwa unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la upatikanaji wa maji wilayani Ruangwa.”

Waziri Mkuu amesema mbali na huduma ya maji safi na salama, pia Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini, hivyo amewataka wananchi wafanye maandalizi ya kufikisha nishati hiyo katika makazi yao.

Amesema Mheshimiwa Rais Samia anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme nchi nzima vikiwemo na vijiji vya wilaya ya Ruangwa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.


NAIBU WAZIRI CHILO AKERWA NA MLUNDIKANO WA BODABODA VITUO VYA POLISi

 Na Abubakari Akida,MOHA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo amesikitishwa na uwepo wa idadi kubwa ya bodaboda katika Vituo mbalimbali vya Polisi nchini huku akiwaasa wananchi ambao mashauri yao yanasikilizika wafike katika vituo hivyo ili kuondoa msongamano wa vyombo hivyo.

Ameyasema hayo leo Visiwani Zanzibar baada ya kupata maelezo na kutembelea karakana ya kuhifadhia vidhibiti hivyo katika Kituo cha Polisi Madema ambapo amesikitishwa na wingi wa bodaboda kituoni hapo.

“Nchi yetu inataka kupiga hatua za kmaendeleo na uchumi, kwa namna hii ya mrundikano wa bodaboda katika vituo vya polisi maana yake shughuli nyingi huko za vijana zimesimama, naelewa kuna vidhibiti kwa ajili ya kesi maalumu ambazo nyingine ziko mahakamani hivyo haviwezi kuachiwa lakini kwa vile ambavyo kanuni na sheria inaweza kuviruhusu basi viondoke, natoa wito kwa wananchi kufika vituo vyote vya polisi nchi nzima na kufanya mazungumzo na wakuu wa vituo ili tuondoe mrundikano huu,kila mkoa ninaotembelea nakuta vituoni kuna mrundikano wa bodaboda,wananchi njooni muonane na wakuu wa vituo mchukue vyombo vyenu”alisemam Naibu Waziri Chilo

Akizunguma katika ziara hiyo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Unguja, Awadh Juma Haji amesema vyombo vingi vilivyopo kituoni ni kutokana na waliovitendea makosa kutofika vituoni kwa wahusika wakuu hali inayopelekea uwepo wake hapo ambapo alikiri imekua ni kero kwa jeshi la polisi.

“Mheshimiwa Naibu Waziri hapa vyombo vilivyopo ambavyo tunavishikilia hatuwezi kuvitoa ni vile ambavyo mashauri yake bado yapo mahakamani lakini kuna vingine watuhumiwa wake wamekimbia tangu vikamatwe bado awajajitokeza tunachofanya tunasubiri ule muda wa kisheria wa miezi sita ili taratibu za utaifishaji zifanyike hapa tuna magari ya wizi,bodaboda nyingine zimeshiriki katika makosa ya usalama barabarani nyingine zimehusika kwenye uporaji na tatizo linguine wahusika hawaji vituoni kuonana na wakuu wa vituo kuchukua vyombo vyao hali hiyo upelekea mrundikano huu.”alisema RPC Awadh

Akitoa hali ya ulinzi na usalama katika Kipindi hiki cha Sikukuu Kamanda Awadh amesema Sikukuu ya Eid imesheherekewa vizuri pasipo kuwepo matukio makubwa ya uhalifu huku Jeshi la Polisi likiendelea na doria zake za kawaida katika kuhakikisha amani na usalama vinakuwepo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.


Thursday, July 22, 2021

WAZIRI MKUU AITAKA BODI YA KOROSHO KUTAFUTA MASOKO YA UHAKIKA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Korosho Tanzania ihakikishe inatafuta masoko ya uhakika ya zao hilo na yatakayotoa bei nzuri na kuwanufaisha wakulima.

Pia, Waziri Mkuu ameitaka bodi hiyo isimamie mwenendo wa ujenzi wa viwanda vidogo na vikubwa vya kubangulia korosho katika maeneo yote yanayolima zao hilo ili kuondokana na uuzwaji wa korosho ghafi.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Julai 22, 2021) wakati akizungumza na Wakuu wa mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Ruvuma, Mrajisi wa Ushirika, Viongozi wa vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho katika kikao kilichohusu upatikanaji wa pembejeo za korosho kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa mkoani wa Lindi.

Amesema lazima bodi hiyo ambayo ameizindua lazima iwajibike ipasavyo katika kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa zao hilo na iwapo itashindwa Serikali haitosita kuivunja. 

"Lazima mfuatilie na kuufahamu mwenendo wa zao mnalolisimamia na mjue mfumo unaotumika katika mauzo yake. Pia muwe na takwimu za wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili kuweza kuwahudumia kwa urahisi."

Waziri Mkuu amesema bodi hiyo inatakiwa iandae kalenda maalumu inayoonesha hatua zote zinazopaswa kufuatwa katika kilimo cha zao hilo kuanzia hatua za uandaaji wa shamba hadi mavuno kwa kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika na ipelekwe kwa wakulima.

Amesisiza kwamba utaalamu lazima ufuatwe na uzingatiwe katika kilimo hilo kwa lengo la kuongeza tija kwa wakulima. Pia, Waziri Mkuu ameitaka bodi hiyo ihakikishe pembejeo ikiwemo miche bora na viuatilifu vinapatikana kwa urahisi.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameigiza bodi ya korosho iweke mkakati wa utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na faida ya kulima zao la korosho. "Tumieni magari maalumu kwa ajili ya kwenda kuwafuata wakulima katika maeneo yao na kuwapa elimu."


RAIS SAMIA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA TONY BLAIR WAZIRI MKUU MSTAAFU WA UINGEREZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 22 Julai, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe. Tony Blair, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Mhe.Tony Blair ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change) amemhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa taasisi yake inaunga mkono jitahada mbalimbali anazochukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania. Amesema taasisi yake inafanya kazi katika nchi 16 Afrika ikijikita kutekeleza vipaumbele vya Serikali zao ambapo amsema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu taasisi yake imejikita zaidi katika masuala ya kukabiliana na janga la UVIKO 19.Mhe. Tony Blair amesema katika kukabiliana na janga la UVIKO 19, taasisi yake inashughulika zaidi na masuala ya upimaji na usambazaji wa chanjo ambapo amesema taasisi yake inaweza kusaidia Tanzania kuwafikia wazalishaji wa chanjo hizo.Aidha, amesema mbali na masuala ya UVIKO 19, pia wanajengea uwezo nchi washirika kufuatilia miradi ya kilimo, nishati na matumizi ya teknolojia.Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Tony Blair kwa kumjulisha masuala yanayofanywa na taasisi yake katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nchi washirika. Mhe. Rais Samia amesema kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Kuhusu UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amemueleza Mhe. Tony Blair kuwa tayari Serikali ina mpango wake wa Kitaifa kuhusu namna ya kushughulikia masuala yote ya UVIKO 19 ikiwemo uratibu wa chanjo.Mhe. Rais Samia amesema katika kujijengea uwezo kwa sasa Serikali ina mpango wa kujenga viwanda vya kuzalisha chanjo za aina mbalimbali na hivyo kuomba taasisi ya Tony Blair kuunga mkono jitihada hizo.Aidha, Mhe. Rais Samia ameikaribisha taasisi ya Tony Blair kuja nchini kufanya kazi na taasisi za Tanzania kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali.


 Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe. Tony Blair wakati Mhe. Blair , akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipofika  Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 22,2021. (Picha na Ikulu)