Monday, May 31, 2021

KAMATI YA BUNGE YATOA WITO WAKANDARASI WABOVU MIRADI YA REA WASIPEWE TENA KAZI

 Veronica Simba na Zuena Msuya.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetoa wito kwa Serikali kuwa wakandarasi ambao hawakutekeleza miradi ya umeme vijijini kwa kiwango kinachoridhisha katika awamu zilizopita, wasipewe tena kazi hiyo.

Wito huo ulitolewa jana, Mei 31, 2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula alipokuwa akitoa majumuisho ya hoja mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya Wajumbe, katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati, ikilenga kuijengea Kamati hiyo uelewa wa kazi zinazoendelea kutekelezwa na sekta husika.

Alisema, baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakikwamisha jitihada na dhamira njema ya serikali inayolenga kuwafikishia umeme wananchi wote walioko vijijini, kutokana na kuchelewesha kukamilisha miradi hiyo na wengine kutekeleza chini ya kiwango kinyume na mikataba yao.

Aliutaka Uongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake, hususan Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutoa kipaumbele kwa wakandarasi waliotekeleza kazi zao kwa umahiri katika awamu zilizopita.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi mzima wa Wizara na Taasisi zake, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aliwahakikishia Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa, Serikali itazingatia maelekezo yote yaliyotolewa.

Akifafanua, Waziri Kalemani alieleza kuwa tayari Serikali ilikwishachukua hatua za kuachana na wakandarasi wabovu ambapo alibainisha kuwa katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa pili ambao unaendelea hivi sasa, wakandarasi wote wazembe hawakupewa kazi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani aliieleza Kamati hiyo kuwa, Wizara yake imeamua kutumia nguzo za zege katika maeneo korofi hususan yenye ardhi inayohifadhi maji ili kutatua changamoto ya kuharibika kwa nguzo za miti ndani ya kipindi kifupi.

Pia, aliahidi kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kusimamia kikamilifu suala la uzalishaji nguzo za miti zenye ubora, unaofanyika ndani ya nchi ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kimataifa. 

Aliongeza kuwa, lengo ni kuepusha hasara katika miradi ya usambazaji umeme inayotekelezwa kote nchini, ambapo Serikali inatumia nguzo hizo baada ya kuacha kuagiza kutoka nje ya nchi.

Awali, akiwasilisha mada kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA, Mkurugenzi wake Mkuu, Mhandisi Amos Maganga alibainisha kuwa Wakala umejiwekea malengo ya kufikisha miundombinu ya umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara, ifikapo Desemba, 2022.

Aidha, alieleza kuwa REA imejipanga kuhakikisha hali ya upatikanaji wa huduma za umeme inafikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wa mafanikio, Mhandisi Maganga alibainisha kuwa ni pamoja na kufikisha na kusambaza umeme katika Makao Makuu ya Wilaya zote za Tanzania Bara. Vilevile alisema, kupitia REA, Serikali imewezesha hali ya upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini kuongezeka kutoka asilimia mbili mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69.6 mwaka 2020.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuwezesha taasisi za afya, elimu na maji kufikiwa na huduma za umeme hivyo kuboresha na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma. Pia, kuwezesha uboreshwaji wa kilimo cha umwagiliaji katika mashamba.

Semina hiyo ilifanyika katika Ofisi ndogo za Wizara zilizopo Kikuyu Dodoma.

 Viongozi wengine wa Serikali walioshiriki ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato, Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu Kheri Mahimbali na Wataalamu mbalimbali wa Wizara, REA na TANESCO.

Taasisi nyingine zilizowasilisha mada katika semina hiyo ni kutoka TANESCO iliyowasilishwa na Mkurugenzi wake Mtendaji, Dkt. Tito Mwinuka pamoja na kampuni yake tanzu ya uendelezaji jotoardhi (Tanzania Geothermal Development Company - TGDC), iliyowasilishwa na Meneja Mkuu, Mhandisi Kato Kabaka. 

KAMISHENI MNAZOZISIMAMIA NI NYETI KATIKA JESHI LA POLISI: IGP SIRRO

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, akiwavalisha cheo cha Ukamishna wa Jeshi la Polisi (CP) Camilius Wambura (pichani juu) na Hamad Khamis Hamad(Picha ya chini)kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam Mei 31, 2021. Rais Samia aliwateua Kamishna Wambura kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) huku Kamisha Hamad yeye akiteuluwa KUWA MKUU wa Logistic na Fedha. KATIKA ujumbe wake mara baada ya kuwapandisha vyeo, IGP Sirro aliwakumbusha matamanio ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Samia ya kwamba ni kuona Utendaji kazi uliotukuka.

"Katika Jeshi la Polisi Kamisheni hizi ni nueti sana, nakufahamu Kamishna Wambura wewe ni mzoefu katika Upelelezi sasa nenda kafanyie kazi mlundikano wa kesi uliopo, Hali kadhalika kwa Kamishna Hamad ninauhakika nafasi uliyopewa utaitekeleza kwa weledi wa Hali ya juu." Alisema IGP Sirro.(Picha na Jeshi la Polisi).
 

Sunday, May 30, 2021

TANESCO YASIFIWA KWA UTEKELEZAJI BORA WA MIRADI.*

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepongezwa na kusifiwa kwa utekelezaji thabiti wa Miradi mbalimbali ya Umeme ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati na miradi midogo midogo ya usambazaji Umeme Nchini kote. 
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka Tarehe 30 Mei 2021 alipotembelea banda la TANESCO katika maonyesho ya Teknolojia yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. 
Sambamba na pongezi hizo, Mhe Mtaka ameshauri wataalamu wa Tehama wa Shirika kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu ili kuboresha mifumo ya utoaji huduma ikiwemo  huduma za ununuzi wa umeme wa LUKU  na kuwezesha wateja kununua umeme kisha umeme huo kuingie  katika mita  bila kumlazimu mteja kwenda kuweka umeme katika mita.
Mhe. Mtaka amesema pamoja na mambo mengi mazuri ambayo TANESCO imekuwa ikiyafanya, ni vvyema Shirika likafanya  ushirika na taasisi za elimu ya juu ili kukuza ubunifu na kuwezesha wataalamu wa ndani kutumika katika kutekeleza miradi mbali mbali bila kuhitaji wataalamu kutoka nje ya nchi na ikiwezekana wataalamu wa Shirika waweze kufanya na kusimamia hata miradi mingine mikubwa inayotekelezwa katika nchi jirani.
 “Hii nikutokana na uzowefu ambao wataalam wa TANESCO watakuwa wameupata baada ya kukamilisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati” Alisema Mhe. Mtaka

Mhe. Mtaka aliongeza kuwa, Miradi  ya umeme vijijini inatekelezwa  kwa weledi wa hali ya juu, ni vyema sasa TANESCO ikawezesha wataalam wake kwa kushirikiana na Taasisi zingine za serikali kuanza kupeleka wataamamu katika kandarasi za usimamizi wa miradi nje ya Nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony  Mtaka akipokea maelezo  kutoka kwa Meneja wa TANESCO  Mkoa wa Dodoma   Mhandisi Kenneth Boimanda  wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipotembelea Banda la TANESCO katika maonyesho ya teknolojia yanayo endelea katika Uwanja wa jamuhuri jijini Dodoma Leo  30 Mei 2021

Mhandisi Erasto Chiswanu akielekeza wanafunzi wa Shule Sekondari ya  Wasichana ya  Msalato jinsi Mradi wa Julius Nyerere unavyo tekelezwa  wakati wanafunzi hao walipo tembelea banda la TANESCO  katika maonyesho ya Teknolojia  yanayo endelea katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Leo 30 Mei 2021
 

Saturday, May 29, 2021