8/31/2020

MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI CCM RAIS MHE. DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AONGOZA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA MAPINDUZI CCM JIJINI DODOMA


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi pamoja na Wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM wakati wakiimba Wimbo wa Chama kabla ya kuongoza Kikao hicho cha Kamati Kuu jijini Dodoma leo tarehe 31 Agosti 2020



 

    

KATIBU MKUU KILIMO GERALD KUSAYA AJADILI NAMNA YA KUINUA KILIMO CHA MBOGA NA MATUNDA (HORTICULTURE), ARUSHA

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya (pichani kushoto) amefanya kikao na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kuendeleza Mazao ya Bustani (TAHA) Dkt.Jacquline  Mkindi jijini Arusha cha kujadili mikakati na mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo ya tasnia ya mboga mboga na matunda (horticulture) nchini. 

Sambamba na kikao hicho, Katibu Mkuu Kusaya ameikabidhi TAHA zawadi ya Ramani ya Tanzania inayoonesha viwango vya pH na Afya ya Udongo kwa nchi nzima na imepokelewa na Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dr. Jacqueline Mkindi.

Kusaya ameitaka TAHA kuendelea kuelimisha wakulima wengi zaidi kuzingatia kilimo cha kitaalam kwa kutambua aina ya udongo unaofaa kwa zao husika na mbolea gani itumike, ndio maana amekabidhi ramani hiyo kuwezesha utambuzi wa maeneo yanayofaa kwa mazao ya horticulture nchini.

"Tunaendelea kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano mkubwa na wa muda wote inaotupatia wadau wa sekta ya horticulture " Dr Mkindi alisema.

Katibu Mkuu Kusaya alikuwa mkoani Arusha Kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kutembelea taasisi zinazojihusisha na kilimo vikiwemo viwanda vya kuzalisha mbolea kwa matumizi ya kilimo.

    

MSITU WA MINYUGHE ULIOPO IKUNGI MKOANI SINGIDA UPO HATARINI KUTOWEKA

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, viongozi wa Kata ya Mwaru pamoja na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, wakati akikagua Msitu wa Minyughe ambao umevamiwa na kufanyika uharibifu mkubwa wa mazingira.
Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (katikati) na wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Kata ya Mwaru wakiangalia mkaa uliotelekezwa na wavamizi katika msitu huo.Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (katikati) akiwaonesha wajumbe wa kamati hiyo mkaa uliotaifishwa na Serikali baada ya kutelekezwa na wavamizi katika Msitu wa Minyughe wilayani humo mwishoni mwa wiki wakati akikagua msitu huo. Kulia ni Mshauri wa Jeshi la Akiba wa wilaya hiyo, Capteni Gabriel Chabimia na Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP)  Stephano Chaula.


Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Mjummbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Mwaru, Mohamed Mrisho (katikati) akielezea uharibu wa msitu huo.
Ulinzi ukiimarishwa wakati wa ukaguzi wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na mtoto Soud Seme anayeishi na wazazi wake ndani ya msitu huo.
Wajummbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Mwaru,wakimwaga mkaa uliohifadhiwa kwenye viroba na wavamizi wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) na wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Kata ya Mwaru wakiangalia mkaa uliotelekezwa na wavamizi katika msitu huo.
Mhifadhi Misitu Wilaya ya  Ikungi (DFC), Wilson Pikoloti akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwaru, Mwinyimvua Midelo , akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha wa Kijiji cha Mwaru, Shabani Nyombe akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mjummbe wa Kamati ya Huduma za Jamii wa Kijiji cha Mwaru, Johari Haji, akielezea uharibifu wa msitu huo.
Safari ya ukaguzi wa msitu huo ikiendelea.

Na Dotto Mwaibale, Singida
HALI ya Msitu wa Minyughe uliopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imeendelea kuwa mbaya kutokana na wakazi wanaouzunguka kuuvamia kwa kukata miti hovyo na kuingiza mifugo bila ya kufuata taratibu.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo mwishoni mwa wiki ilitembelea na kujionea hali halisi na namna uvunaji wa mazao ya msitu huo ikiwemo ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa ukifanyika bila ya kufuata utaratibu wimbi kubwa la wahamiaji kutoka mikoa ya jirani wakihusishwa na uharibifu huo.
Msitu huo wenye ukubwa wa takribani hekta 230,000 upo katika Tarafa za Sepuka, Ihanja na Ikungi na kuundwa na vijiji 26 wilayani Ikungi.
Msitu huo ulianzishwa chini ya mradi wa LAMP (Land Management Programme) ukifadhiliwa na Shirika la Sida la Uswisi mwaka 2002.
Msitu huo una uoto wa asili wa miti jamii ya miombo na maeneo kidogo ya mbuga na uoto adimu wa vichaka vya Itigi (Itigi Thickets) huku ukiwa na wanyamapori na viumbe wengine wa aina mbalimbali ambao walifanya makazi ndani ya msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, viongozi wa Kata ya Mwaru pamoja na waandishi wa habari wakati akikagua msitu huo alisema lengo la kuuanzisha ilikuwa ni kutunza uoto wa asili na bioanuwai zilizokuwa hatarini kutoweka ikiwemo wanyamapori
Alitaja lengo lingine kuwa ni kutunza mazingira kwa ujumla na kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa, kutunza rasilimali asili kwa kizazi kilichopo na kijacho pamoja na jamii kunufaika moja kwa moja na rasilimali misitu zilizopo.
Mpogolo alisema msitu huo ni nguzo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ukiungana na msitu wa mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi katika kuimarisha mvua zitokazo misitu ya Kongo.
"Msitu huu ni chanzo cha maji ya Ruaha Mkuu ( Internal Drainage) ukiunga pori la akiba la Rungwa, Muhesi na Kizigo lililopo Manyoni" alisema Mpogolo.
Alisema msitu huo ni kidaka maji ( Catchment Forest) kwa bonde la Wembere linaloweka uhai wa Ziwa Kitangiri na Eyasi.
Mpogolo alikamilisha kuzungumza na wajumbe hao na waandishi wa habari kwa kutoa maagizo ya kuwachukulia hatua watu wote waliovamia msitu huo kwa kujenga na kuingiza mifugo yao ambapo alitaka orodha yao ikiwa na kuondoka mara moja ndani ya msitu ndipo wafanye utaratibu wa kuomba upya kwa serikali ya kijiji.
"Haiwezekani kuingia kwenye hifadhi bila ya kufuata taratibu na kufanya uharibifu huu mkubwa, Serikali ya kijiji na kamati yangu ya ulinzi na usalama ni lazima tuhakikishe uhalibifu huu wa msitu haujirudii tena" alisema Mpogolo.
Alisema hali hiyo ikiachwa eneo hilo litakuwa jangwa na jamii inayoishi humo itapata matatizo ya maisha kwani hata madawa yatokanayo na miti ya asili hayata patikana.
Mpogolo alitumia nafasi hiyo kuwaagiza viongozi wa halmashauri ya kijiji katika eneo hilo kuitisha mkutano utakaowakutanisha wavamizi hao na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ili kujua walipateje kibali cha kuingia kwenye hifadhi hiyo kwani yamekuwepo madai ya watu kuwa kuna baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vijiji vinavyozunguka msitu huo kuchukua fedha au ng'ombe kutoka kwa wafugaji hao na kuwagawia ardhi katika hifadhi.
Alisema kupitia mkutano huo watawabaini viongozi waliojihusisha kwa namna moja au nyingine kutoa maeneo kwenye hifadhi hiyo nao watachukuliwa hatua za kisheria huku wavamizi hao wakifanyiwa utaratibu na halmashauri wa kutafutiwa maeneo mengine ya kuishi na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji nje ya hifadhi. 
Aidha Mpogolo alisema mvamizi  atakaye kahidi hatua hizo za awali za mazungumzo na kuwasikiliza atachukuliwa hatua kali ikiwemo kuondolewa kwa nguvu ndani ya hifadhi hiyo.
    

WAZIRI UMMY ASHIRIKI HARAMBEE KANISA LA ANGLIKANA CHUMBAGENI TANGA,ATOA NENO KWA VIONGOZI WA DINI

 

WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza wakati alipoongoza  harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga Mtaa wa Mtakatifu Augustino wa Hippo Chumbageni Tanga kulia ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa kushoto ni Canon  Rev Chistopher Kiango ambaye ni Kasisi kiongozi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga 
Canon  Rev Chistopher Kiango ambaye ni Kasisi kiongozi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga  akizungumza wakati wa harambee hiyo

MKUU wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa akizungumza wakati wa halfa hiyo
WAZIRI  wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kushoto akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa Katibu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tanga Mtaa wa Mt.Augustino wa Hippo Chumbageni Tanga. 

WAZIRI  wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kushoto akipokea mchango wa mtoto Nicolaus Galula wakati wa harambee hiyo
MENEJA wa Hotel ya Tanga Beach ya Jijini Tanga Joseph Ngoyo akizungumza jambo wakati wa harambee mara baada ya kukabidhi mchango wake kwa niaba ya familia yake
WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kushoto akipokea mchango kutoka kwa Catherine Kitandula wakati wa harambee hiyo
Kwaya ikitumbuiza wakati wa harambee hiyo


WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewataka viongozi wa dini kote nchini kuendelea kuliombea Taifa amani, umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu.

Ummy aliyasema hayo leo wakati alipoongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga Mtaa wa Mtakatifu Augustino wa Hippo Chumbageni Tanga.

 

Katika harambee hiyo walifanikiwa kukusanya fedha taslimu milioni 13.7 papo hapo na ahadi ikiwa ni milioni 47.2.huku mwisho wa kukusanya michango hiyo ikiwa ni Septemba 20 mwaka huu. 

Katika harambee hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa na viongozi wa dini wakiwemo waumini huku kwaya mbalimbali zikitumbuikza

“Lakini pia tunawashukuru viongozi wa dini kwa jinsi walivyotuunga mkono kwa sala za kila siku katika mapambano dhidi ya Corona na mungu akatuepusha na janga hili hivyo niwaombe hata wakati huu nchi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu tuendelee kuiombea nchi”Alisema Waziri Ummy

“Nimekuwa nikipata ujumbe kutoka kwa mawaziri wa nchi nyengine Afrika tumefanya kitu gani mpaka hakuna Corona nisema kwamba ugonjwa huo umetoweka kutokana na Mungu ameipenda Tanzania”.

 Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi Katibu wa Kanisa hilo Cyprian Mtweve alisema lengo la harambee ya leo katika kuadhimisha sikukuu ya Mt.Agustino wa Hippo ni kupata kiasi cha sh.milioni 125 kwa ajili ya kuezeka kanisa.

 Alisema wanaamini kiasi hicho sio kikubwa kwa Mungu cha kushindwa kupatikana huku wakimshukuru mgeni rasmi kuwaongozea zoezi la harambee hiyo na kushiriki kwa moyo na kwa ukamilifu.

 Aidha alisema upanuzi wa jengo la kanisa hilo umekuwa ukifanywa kwa kulirefusha kwa kiwango ambacho mawasiliano baina ya kasisi anayeongoza ibada madhabahuni na waumini wanaokaa viti vya mwishoni nyuma ya kanisa yanakuwa hafifu sababu ya umbali.

“Jengo hili limejengwa kwa kutumia teknologia ya zamani isiyohimili uwekwaji wa mifumo mbalimbali ya kisasa ikiwemo ile itakayoboresha ibada”Alisema

Miongoni mwa viongozi ambao wamechangia kwenye harambee hiyo ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Profesa Palamagamba Kabudi wakiwemo wakuu wa wilaya .

    

8/30/2020

WALIMU WA HEDHI RUKWA WAJA NA MUAROBAINI WA TAULO ZA KIKE

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi akitoa nasaha wakati wa kufungua mafunzo ya Hedhi Salama kwa baadhi ya waalimu wa Shule za Msingi Mkoani Rukwa.

 

Baadhi ya Waalimu kutoka halmashauri ya wilaya ya Kalambo wakionesha vyeti vyao baada ya kupatiwa mafunzo ya Hedhi Salama wakiwa katika picha ya pamoja na Mratibu wa Mradi wa SWASH Mkoa Matinda Mwinuka (aliyechuchumaa kushoto) na Mwezeshaji Jesca Lwiza (aliyechuchumaa kulia)

 NA MWANDISHI WETU, RUKWA

UMOJA wa Walimu wa Hedhi Salama kwa shule za msingi mkoani Rukwa wamepania kuhakikisha wanapunguza fikra potofu kuhusu suala la hedhi kwa wasichana wanaovunja ungo pamoja na kukomesha utoro kwa wananfunzi wa kike wanaoona aibu kuhudhuria shule pindi wanapopata hedhi kwa kutoa elimu sahihi ya suala la hedhi mashuleni.

Azma hiyo imekuja baada ya waalimu hao kupewa mafunzo yanayohusu namna ya kutengeneza taulo za kike (pedi) kwa kutumia aina mbalimbali za vitambaa pamoja na kukabiliana na wanafunzi wanaoona aibu ama fedheha pindi wanapopata hedhi wakiwa shuleni na hivyo kuwarahisishia Maisha yao wanapokuwa shuleni huku wakiwahamasisha kuendelea kuhudhuria shuleni ili wasiachwe nyuma kimasomo.

Aida Mwanauta ni mwalimu wa Hedhi Salama kutoka Shule ya Msingi Ilambila, Wilayani Kalambo, aliishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo muhimu kwani changamoto wanazokumbana nazo ni nyingi na mafunzo hayo yamamsaidia kujua namna ya kuwasaidia wasichana hao pindi wanapokuwa katika hedhi kutokana na wanafunzi wengi kutokuwa na ufahamu wa kutosha juu ya namna ya kukabilina na hali hiyo.

“Kuna mwanafunzi anakuja shuleni hajui ni namna gani anaweza akajistiri, mwingine anatoka nje anakimbia, huko nje anachukua hata makaratasi, majani kwaajili ya kujistiri ambayo inaweza ikamletea matatizo baadaye, kwahiyo katika semina hii tumejifunza mambo mbalimbali, tumejua ni mambo gani ambayo unaweza ukamfundisha mtoto, akajua jinsi ya kujihifadhi akiwa shuleni na hatimae akawa anasoma na asiwe mtoro shuleni, na kujiona ni sawa na wengine,” Alisema.

Nae, Mwalimu Victoria Tanganyika alisema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kujua vifaa vinavyotumika kutengeneza pedi za kike na namna ya kuvitekeza pamoja na kujua mazungumzo anayotakiwa kufanya na matoto ili kumshawishi aweze kujiamini  na kushiriki katika michezo na masomo katika mazingira ya shule.

Kwa upande wake Mwalimu Clifonsia Remidio ameiomba serikali kuendelea kutumia njia mbalimbali za vipeperushi na kutoa semina kwa waalimu wengi zaidi wanaotoa huduma ya hedhi salama mashuleni ili kuweza kuwasaidia wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakipata tabu kusoma wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.

“kuna vitu vingi tulikuwa hatuvifahamu, kuna wakati mwingine hata kama mimi mwalimu nimeshasoma lakini bado nitaona aibu kuenenda kumuelekeza yule mwanafunzi, lakini ameshatuelekeza mwezeshaji tumepata mwanga mzuri pia nimefurahi kwasababu hili suala linashirikisha pande zote mbili, upande wa waalimu wa kiume na upande wa waalimu wa kike pia kwamba tuwasaidie Watoto wanaposikia ile hali ya mabadiliko ya mwili,”Alisema.

Aidha, Mwezeshaji wa mafunzo hayo ya Hedhi Salama, Mwalimu Jesca Lwiza alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi ili kupunguza utoro mashuleni na kuongeza kuwa wanategemea kuona mabadiliko makubwa ya mahudhurio shule kwa shule ambazo waalimu wake wamehudhuria mafunzo hayo.

“Kuna ukimya ambao upo katika masuala ya hedhi salama, wanafunzi wanakosa elimu sahihi, lakini pia wanakosa namna ya kujiamini wanapokuwa katika masomo na wakati mwingine shuleni hakuna vyumba maalum vya kujihifadhi wanapokuwa katika hedhi, kwa kulitambua hilo tumeona serikali namna ilivyoweza kuwezesha kwa kuwapa mafunzo waalimu lakini imeweza kuboresha miundombinu iliyopo mashuleni kwa kuweka vyumba hivyo,” Alisema.

Wakati akifungua mafunzo hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi alisisitiza kuwa tafiti zilizofanyika zimeonesha kuwa wasichana wengi hawana taarifa za awali kuhusu hedhi za pia walipata hedhi ya kwanza pasipo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mabadiliko ya miili yao hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waalimu kufikisha elimu katika shule.

“Tafiti zinaonesha kuwa bado kuna fikra zisizo sahihi kuhusu masuala ya hedhi hususani miiko na unyanyapaa inayosababisha wasichana na wanawake kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kijamii na wanafunzi wa kike kukosa baadhi ya siku za masomo na wengine kuacha shule wanapokuwa kwenye hedhi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulitambua hilo imeweka jitihada kuhakikisha kuwa fursa za elimu zinapatikana kwa makundi yote,” Alieleza.

Halikadhalika mratibu wa mradi wa School Water Sanitation and Hygiene (SWASH) Mwalimu Matinda Mwinuka aliwaasa waalimu kuhakikisha shule zinakuwa na vyombo maalum kwaajili ya walemavu pamoja na vyumba kwaajili ya wasichana kubadili pedi za hedhi pindi wanapokuwa katika hali hiyo nasio kutumia vyoo vya kawaida ambavyo havina mazingira mazuri ya kubadilishia vifaa vyao.

“Kuna shule moja fundi kaweka shule maalum, anasema kuwa kile ndio chumba maalum, walemavu wataingia humo humo, hedhi salama wataingia humo humo, ametoboa tundu na kuweka ‘pipe’ anasema Watoto wa kike wakishaingia humu ndimo watatumbukiza vile vitu vyao yaani ni vitu vya ajabu kwakweli.”

Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri tatu za Mkoa wa Rukwa kwa muda wa miaka minne huku kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Mkoa ulipewa kiasi cha Shilingi 578,486,955.63/= kwaajili ya utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa katika mikoa 17 na Halmashauri 86 za Tanzania Bara ukiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia, kujenga vyoo bora shuleni na kuweka miundombinu ya maji safi na salama.

 


    

KATIBU MKUU KILIMO AKABIDHI GARI BODI YA PARETO

Mkulima wa mbegu bora za mahindi Bw.Aron Nguma (kulia) wa Arusha akikabidhi mahindi yaliyokauka ya mbegu kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya leo alipotembelea shamba hilo Ngaramtoni kukagua hali ya uzalishaji mbegu za mahindi,maharage na ngano .Shamba hilo linamilikiwa na Wakala wa mbegu Nchini (ASA)

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kushoto) akikabidhi funguo za gari Toyota H/Top kwa Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Pareto Lucas Ayo  jijini Arusha. Gari hiyo imekabidhiwa ili kusaidia bodi kuhamasisha wakulima wengi kulima zao la pareto nchini.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pareto Lucas Ayo akionyesha funguo za gari mara baada ya kukabidhiwa  toka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kushoto). Hafla hiyo ilifanyika jijini Arusha.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (katikati) akitoa maelekezo  kwa dereva wa Bodi ya Pareto  Venance Haule (kushoto) leo alipokabidhi gari kwa bodi hiyo jijini Arusha .


 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (wa saba toka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa wizara na taasisi zake zilizopo Arusha  alipokabidhi gari kwa Bodi ya Pareto nchini.