8/31/2021

WAZIRI MKUU AZINDUA TAWI LA BENKI YA MWANGA NA KUTOA MAAGIZO SABA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Tawi la Benki ya Mwanga Hakika jijini Dodoma, Agosti 31, 2021. Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo, Ridhiwani Mringo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Benard Kibessa na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Jagjit Singh. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Tawi la Benki ya Mwanga Hakiki jijini Dodoma, Agosti 31, 2021.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt Benard Kibessa (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Benki ya Mwanga Hakika, Ridhiwani Mringo tawi la Dodoma, baada ya kuzindua tawi hilo Agosti 31, 2021.Kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi pamoja na watumishi wa Benki ya Mwanga Hakika baada ya kuzindua tawi la Benki hiyo jijini Dodoma, Agosti 31, 2021. Waliokaa kutoka kushoto ni Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo, Ridhiwani Mringo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Benard Kibessa na kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo.. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

************************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua tawi la benki ya Mwanga Hakika jijini Dodoma na kuitaka benki hiyo iwe kimbilio la wajasiriamali na wakulima wadogo.
“Kuweni kimbilio la wajasiriamali na wakulima wadogo. Njooni na bidhaa na vivutio muhimu kwa makundi hayo ya wajasiriamali na wakulima wadogo. Hilo ni kundi ambalo linahitaji zaidi huduma zenu katika kuliwezesha kujikwamua kiuchumi,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Agosti 31, 2021) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali, wanahisa na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa tawi la benki ya Mwanga Hakika (Mwanga Hakika Bank) jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ameitaka benki hiyo ipunguze riba ili kuendana na dhamira ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akilisemea suala hilo mara kwa mara. “Nanyi pia lizingatieni hili katika kukua kwenu kwani kupungua kwa kiwango cha riba kutasaidia kusisimua biashara na shughuli nyingine za kiuchumi,” amesisitiza.
Ameitaka benki hiyo iongeze ubunifu. “Kuweni wabunifu. Sambamba na kutengeza faida, kuongeza amana za benki na kutoa gawio kwa wanahisa, njooni na ubunifu utakaoboresha huduma zenu na kuzifanya kuwa ubora zaidi, zenye tija na gharama nafuu kwa walaji.”
Ameitaka benki hiyo ipunguze gharama za tozo kwani tozo za mabenki kwa wateja bado ni kubwa na wakati mwingine haziendani hata na mfumuko wa bei. “Hakikisheni huduma za kibenki zisiwe kikwazo kwa wananchi wa kawaida.”
“Sogezeni huduma kwa wananchi hususan maeneo ya pembezoni ili kuwahakikishia usalama wao pamoja na fedha zao. Angalieni uwezekano wa kufungua matawi huko Mpwapwa, Kongwa, Kondoa, Bahi na maeneo mengine ya jirani ikiwa ni njia ya kupanua wigo kwa kuwafuata wateja.”
Amesema MHB hawana budi kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na akaunti sambamba na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja. “Waelimisheni wananchi ili waache kutunza fedha majumbani, wekeni matawi madogo madogo ili wafungue akaunti kwa urahisi,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ameitaka benki hiyo iunge mkono juhudi za Serikali ili kuwezesha kufikiwa kwa azma ya Serikali kujenga uchumi wa viwanda. “Iungeni mkono Serikali hii kwa kukuza kilimo, viwanda na biashara. Tuwaondoe wananchi woga wa kukopa katika benki. Mheshimiwa Rais amekuwa akihamasisha watu wafanye biashara na lengo la Serikali hii likiwa ni kutoka katika uchumi wa kati ulio chini na kwenda katika uchumi wa kati ulio juu,” amesema.
Amesema benki ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha kwa wananchi. Hivyo, katika kuwahudumia wananchi wazingatie mahitaji yao, wawahamasishe na kuwaelimisha umuhimu wa kutumia benki.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara iliyokuwepo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa aliwapongeza wanahisa wa MHB kwa uamuzi wao wa kuunganisha taasisi tatu za kifedha na kufikia kuwa benki inayotoa huduma tofauti na hapo awali.
Waziri Bashungwa ambaye alizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, alisema benki hiyo imeweza kuwafikia wateja zaidi ya 100,000 na kutoa mikopo ya sh. bilioni 38.9 baada ya kuunganisha taasisi za kibenki za EFC Tanzania Microfinance Bank (EFC), Hakika Microfinance Bank (Hakika) na Mwanga Community Bank (MCB).
“Tunataraji kuwa mikopo hii itakuwa na manufaa kwa sekta mbalimbali za kiuchumi na nipende kuwahakikishia uongozi wa Mwanga Hakika Bank kuwa itapata ushirikiano kutoka Serikalini,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda aliiomba benki hiyo iwasaidie wakulima hasa kwenye mazao ya alizeti na zabibu ambayo ni maarufu mkoani Dodoma na Serikali imeamua kuyatilia mkazo ili kuongeza uzalishaji wake.
“Tunahitaji wafanyabishara kwenye sekta ya kilimo kama vile wanunuzi wa mbolea na viuatilifu. Tunahitaji watu wa kusindika mazao ya wakulima (agro-processing) na wasambazaji wa viuatilifu (agro-chemicals). Ninaahidi kufanya kazi kwa ukaribu na Mwanga Hakika Bank ili kuinua kilimo,” alisema.
Naye, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Bernard Kibesse alisema uzinduzi wa tawi hilo jijini Dodoma, utahakikisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi (financial inclusion) na kwamba uamuzi wa kuunganisha taasisi tatu umewawezesha kuwa na mtaji mkubwa zaidi.
“Miaka michache iliyopita taasisi hizo zilikuwa zinatishiwa kufungwa na Benki Kuu kwa kukosa mtaji wa shilingi bilioni mbili. Leo hii wamevuka lengo la sh. bilioni 15 zinazotakiwa ili waweze kuwa benki ya kibiashara. Kwa hiyo, waje wakati wowote ili wakamilishe taratibu na tuwape kibali hicho,” alisema.
    

MAJALIWA: SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA.

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro (katikati) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Stella Mutabihirwa  (kulia) wakati wa ufunguzi wa majengo ya Makao Makuu ya Polisi Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Singida,

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 30, 2021 amefungua majengo ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida na Ofisi za Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Singida, miradi ambayo imegharimu shilingi bilion 1.314

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Waziri Mkuu amesema kuwa amefurahishwa na mradi huo ambao ujenzi wake umetumia muda mfupi na umeokoa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali. Ameahidi kuwa serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya vyombo vya ulinzi na usalama.

“Nawapongeza sana wasimamizi wa mradi huu kwa kuhakikisha unatekelezwa vema na kuakisi thamani ya fedha za mradi yaani value for money sanjari na kukamilika kwa wakati. Tumeelezwa hapa kuwa mradi huu uliotekelezwa kwa mfumo wa nguvu kazi yaani force account, ulianza tarehe 20 Februari, 2021 na kumalizika tarehe 15 Julai 2021 na kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3 badala ya ile ya mkandarasi ya 1.9.” 

Aidha, Waziri Mkuu amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kufuata miongozo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa weledi na kuboresha mifumo ya kiutendaji wa jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na vyombo vingine ili kuepuka ucheleweshwaji wa upelelezi wa kesi kwa lengo la kuondoa mlundikano wa mahabusu magerezani.

“Naliagiza Jeshi la polisi liendelee kuimarisha mfumo wa ulinzi na usalama kwenye ngazi ya jamii ili kujenga mfumo wa kutambua, kutoa taarifa na kuchukua hatua za awali dhidi ya vihatarishi vya ulinzi na usalama vinavyojitokeza katika maeneo yao.

 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Taasisi nyingine za Serikali zinazotekeleza miradi ya ujenzi ziige mfano huo. “Ujenzi wa miradi kupitia mfumo wa nguvu kazi ukisimamiwa vema tena kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo hutoa matokeo chanya.” amesema

“Nawaomba Jeshi la Polisi liendeleze ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama vya nje ya nchi pamoja na taasisi mbalimbali za kimataifa (Interpol) katika kukabiliana na kupambana na matishio ya kiusalama na makosa yanayovuka mipaka hususan ugaidi, makosa ya kimtandao (cyber-crime), uharamia, utakatishaji fedha haramu, biashara haramu ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu, ujangili na bidhaa bandia,”

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chilo, amesema Wizara yake iko thabiti katika kusimamia Sheria na wako tayari kuhakikisha raia wote na mali zao wanaishi kwa usalama na utulivu na kutoa wito kwa watu wote wanaopanga kufanya matendo ya kiuhalifu kuacha mara moja.

 

Naye, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro  amesema ujenzi huo umekamilika kwa kipindi cha miezi mitano kwa kutumia mfumo wa nguvu kazi, (Force Account) ambapo jengo hilo lina ghorofa mbili, vyumba vya ofisi 30 na kumbi mbili za mikutano.

    

8/30/2021

RC KUNENGE AHUZUNISHWA NA AJALI YA MOTO ILIYOTEKETEZA NYUMBA 19 HUKO RUFIJI

NA MWANDISHI WETU PWANI.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amehuzunishwa na tukio la ajali ya moto uliopelekea nyumba zaidi ya 19 kuteketea kabisa kwa moto kwenye Kitongoji cha Shaurimoyo, Kijiji cha Nyamwage Wilayani Rufiji.

Ajali hiyo imetokea baada ya mwananchi mmoja aliyekuwa  akisafisha shamba lake kwa kuchoma moto na moto huo kuwa mkubwa hali iliyopelekea kushindwa kuudhibiti na hivyo kuunguza nyumba.

Akizungumza kwenye eneo hilo la tukio usiku wa kuamkia leo Agosti 30, 2021 akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ameagiza serikali ya wilaya kufanya tathmini kwa haraka ili kujua ukubwa wa athari iliyosababishwa na ajali hiyo na hivyo msaada unaohitajika utolewe haraka. 

"Nimehuzunishwa sana na ajali hii na niwape pole wote mlioathirika na moto huu, na pia nawapongeza sana wananchi waliochukua hatua za haraka kwa kuwahifadhi na kuwasaidia wanakijiji wenzenu," alisema RC Kunenge na kuongeza.....naagiza tathmini ifanyike kwa haraka ili tujue namna ya kuwasaidia wenzetu hawa." Alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele ameeleza kuwa hakuna vifo wala majeruhi kutokana na ajali hiyo, licha ya kwamba moto umetekeleza kila kitu.

Wilaya ilichukua hatua mara moja baada ya kutokea tukio hilo na kutoa rai kwa wakazi wa wilaya hiyo kuwa makini wakati wanachoma moto kwani kwa sasa ni kipindi cha upepo mkali, alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Wananchi wa eneo hilo nao wameeleza tukio jinsi lilivyowaathiri hivyo kuomba serikali kuweza kuwasaidia kwa haraka maana hawana mahala pa kuishi.









    

8/29/2021

SERIKALI YAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU MATUMIZI YA TIBA ASILI NCHINI.


Na WAMJW- DOM 

Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  imeendelea na zoezi la kutoa Elimu kwa wananchi katika maeneo ya kutolea huduma za Afya juu ya umuhimu wa matumizi ya tiba asili/mbadala katika mapambano dhidi ya magonjwa mbali mbali, ikiwemo UVIKO-19. 

Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya tiba asili ya mwafrika Wadau wa tiba asili wakiongozwa na kitengo cha Tiba asili na Baraza la tiba asili kutoka wizara ya afya wameweza kutembelea na kutoa elimu katika  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma, kituo cha Afya cha Makole na Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

Akiongea wakati wa utoaji elimu hiyo Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Tiba Asili/Mbadala  Dkt. Vumilia Liggie alisema kuwa, Wataalamu wa Tiba asili na tiba mbadala kutoka Wizarani wameongozana na Waganga wa tiba hizo kutembelea vituo vya Afya katika sehemu ya wagonjwa wa nje wa Hospitali (OPD) ambapo wameweza kuzungumza na wagonjwa na kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa tiba asili katika mapambano dhidi ya magonjwa mbali mbali nchini. 

"Kwa siku ya leo tumetembelea vituo vya Afya vitatu, tumetembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma General kama kituo cha kwanza, ambapo tumeenda sehemu ya wagonjwa wa nje wa Hospitali ambapo tumeweza kuzungumza na wagonjwa na kuwapa elimu kuhusu tiba asili." Alisema.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali tuna Baraza la tiba asili na tiba mbadala ambalo linatekeleza Sheria namba 23 ya mwaka 2002 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza hili ndio linasajili dawa, Waganga wa tiba asili, na kuwajua wako wapi na wanafanya nini, na kuhakikisha dawa hizo ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Baraza la tiba asili na tiba mbadala linafanya kazi kwa kushirikiana na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Maabara ya TMDA, maabara ya taasisi ya dawa asili pamoja na Maabara ya Shirika la viwango Tanzania, Alisisitiza Dkt. Liggie. 

Naye, Katibu Mkuu wa Shirika la dawa asilia na ulinzi wa mazingira Bw. Boniventura Mwalongo ameeleza zaidi ya asilimia 93 ya dawa zinaagizwa kutoka nje ya nchi, hivyo Serikali imelenga kuboresha tafiti za ndani, kuongeza uzalishaji wa ndani ili kutoa fursa za ajira, hususan kwa vijana, hivyo kupitia kuikuza tiba asili nchini yote yanawezekana.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Waganga wa tiba asili katika zoezi hilo Dkt. Elizabeth Lema alisema kuwa, wiki hii ya maadhimisho inatoa fursa kwa Waganga wa tiba asili na tiba mbadala kuonesha bidhaa zao mbali mbali ambazo tayari zimesajiliwa kupitia Baraza la tiba asili na tiba mbadala na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu. 

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuhudhuria maonesho hayo yatayofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ili kujifunza, kuelimishwa na kupata fursa ya kuuliza maswali mbali mbali kuhusu tiba asili na tiba mbadala kisha kufahamu namna ya kuzipata na kuzitumia. 

Wiki ya tiba asili na tiba mbadala ya Mwafrika inaongozwa na Kauli mbiu ya "Mchango wa tiba asili katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 " ambapo mwisho wa kilele ni Agasti 31, huku Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kufunga maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka.