CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"

 NA MWANDISHI WETU NA MASHIRIKA YA HABARI

KOCHA mpya wa Simba, Pablo Franco Martin, mzaliwa wa Madrid, nchini Hispania, ndiye kocha mwenye CV iliyosheheni kuwahi kutokea katika historia ya soka hapa nchini.

Pablo Franco, alizaliwa Juni 11, 1980 katika jiji la Madrid, na hadi “Anatangazwa kuja” kwa Wekundu wa Msimbazi Simba, kocha huyo ana leseni ya UEFA Pro Licence ambayo inaelezwa kuwa ndiyo leseni inayotolewa kwa muhitimu wa mafunzo ya juu kabisa ya Ufundishaji (Coaching) na Usimamizi (Managerial) wa wa soka barani Ulaya.

Kocha huyo kijana ni miaka minne tu iliyopita alikuwa akifanya kazi na Kocha mwenye mafanikio makubwa Duniani kwenye mpira wa miguu akiwa kama mchezaji na kocha, Maestro  Zinedine Zidane “Zizou” kwenye Klabu ya Real Madrid ya Uhispania  kama kocha msaidizi.

Kocha Pablo mbali na kuiongoza Real Madrid kam Kocha Msaidizi, aliwahi pia kufundisha timu za Getafe CF na Getafe B zote za Hispania, pia timu za Club Deportivo Santa Eugenia, Club Deportivo Illescas, Club Deportivo Puertollano zote za huko huko Hispania na FC Saburtalo ya Georgia.

Kocha huyo ana shahada ya juu ya kufundisha mbinu za mpira wa miguu, utimamu wa mwili wa mwanasoka na jinsi ya kuusoma na kuuchambua mpira wa soka timu zinapokuwa uwanjani.

Kocha Pablo anakuja Simba SC ikiwa nafasi ya pili na alama 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC Premier League) msimu huu wa 2021-2022,ikiwa ndiyo timu pekee kwenye ligi ambayo haijafungwa bao hata moja.

Hata hivyo kumekuwepo na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya washabiki wa timu hiyo kuwa kutokana na ukubwa wake na wachezaji ilio nao haistahili kuwa hapo ilipo na hasa ukizingatia haikuwa na wakati mzuri kwenye Pre-Seson, na michuano ya Ligi ya Mabingwa ambapo licha ya kupata ushindi wa ugenini w amabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ilikuja kuchapwa mabao 3-1 kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa na kutolewa kwenye michuano hiyo ya mwaka huu ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Kazi kubwa ambayo kocha huyo Mhispania anatarajiwa kuifanya ni kuhakikisha Simba ambayo ni mabingwa mara nne wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara na kwa sasa anatete taji hilo inarejea kwenye hadhi yake ya kutandaza mpira kwa pasi za uhakika na kupata matokeo yatakayoiwezesha kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.




Comments