‘TUKIIMARISHA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA YA MAMA NA MTOTO TUTAPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI’-UMMY MWALIMU
Serikali
kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha ubora wa huduma za Afya ya mama na
mtoto katika vituo 25 vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto
tumboni (CEmONC) katika Mkoa wa Dar Es Salaam ili kupunguza vifo vitokanavyo na
Uzazi.
Waziri
wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Machi 28, 2024 wakati akifungua
mafunzo elekezi kazini juu ya huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika
Mkoa wa Dar Es Salaam ambapo mafunzo hayo ni endelevu yanayotolewa nchini nzima
ili kupunguza vifo vya mama mjamzito na mtoto.
“kuimarisha
ubora wa huduma za Afya ya mama na mtoto katika vituo 25 vya Afya vinavyotoa
huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni yaani (CEmONC) tutakua
tumetatua asialimia 84 ya changamoto za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kwa Mkoa
wa Dar Es Salaam.” Amesema Waziri Ummy
Amesema,
mafunzo haya ni muhimu sana ambayo yamesaidia kupunguza vifo katika katika Mkoa
wa Tabora ambapo kwa mwaka 2023 vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo
50 hadi vifo Vinne kwa miezi Mitatu, lakini pia mafunzo hayo yanasaidia kupeana
mbinu mbalimbali za kuwahudumia vizuri wagonjwa ili kuendelea kupunguza vifo
vitokanavyo na Uzazi.
“Mkoa
wa Dar Es Salaam kwa Mwaka 2023 kulikua na vifo vya wajawazito 219, vifo vya
watoto wachanga 1,701 hivyo tunaamini kupitia mafunzo haya tutapunguza takwimu
hizi za vifo kwa zaidi ya asilimia 50, inawezekana.” Amesema Waziri Ummy
Aidha,
Waziri Ummy amezitaka Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha watoa
huduma waliopatiwa mafunzo hayo ili waweze kwenda kutoa mafunzo hayo kwenye
vituo vyao vya Afya vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto
tumboni (CEmONC) vilivyobakia pamoja na Zahanati.
Pia,
Waziri Ummy amezitaka kila Hospitali pamoja na Vituo vya Afya vinavyotoa huduma
ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) zianzishe wodi maalumu
ya watoto wachanga inayofanya kazi kwa kuwa na vifaa tiba pamoja na watoa
huduma waliojengewa uwezo.
“Jambo
jingine nataka nisisitize, tutoe taarifa sahihi za vifo vya wajawazito, vifo
vya watoto wenye umri chini ya miaka Mitano, vifo vya watoto wenye umri chini
ya Mwaka Mmoja pamoja na takwimu sahihi za vifo vya watoto wachanga wenye siku
0-28.” Amesema Waziri Ummy
Mwisho,
Waziri Ummy amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka hadi kufika Mwaka
2027 tuwe tumepunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 24 katika kila vizazi hai
1,000 hadi kufikia 12 katika kila vizazi hai 1,000 “hii inawezekana kupitia
mafunzo haya, hatutamuangusha Rais Dkt. Samia.”
Comments
Post a Comment