MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ZA ARDHI NZEGA MJINI KUKAMILIKA JUNI 30, 2024
Na Eleuteri Mangi
Utekelezaji
wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP)katika Halmashauri ya
Mji Nzega katika mkoa wa Tabora umetekelezwa kwa asilimia 55 na kutarajiwa kukamilika Juni 30, 2024.
Akimkaribisha
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe.
Japhet Hasunga na ujumbe wake wakati wa
ziara ya Kamati hiyo wilayani Nzega
tarehe 27 Machi 2024, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesema utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama
wa Milki za Ardhi katika mji wa Nzega unatekelezwa katika mitaa 14 iliyopo Kata
za Nzega Mashariki, Nzega Magharibi, Nzega ndogo, Kitangiri na Uchama.
Amebainisha
kuwa, katika kata ya Nzega Mjini Mashariki mradi unatekelezwa Mitaa ya
Maporomoko, Uwanja wa Ndege, Msoma, Mwaisela, Nyasa pamoja na Kitongo. Aidha,
Kata ya Nzega Mjini Magharibi mradi unatekelezwa katika mitaa ya Ipilili,
Mbugani, Ushirika na Utemini.
Aidha,
kwa upande wa Kata ya Nzega ndogo mradi unatekelezwa kwenye mtaa wa
Zogolo. Kata ya uchama mradi
unatekelezwa katika Mtaa wa Uchama na kwa kata ya Kitangiri Mradi unatekelezwa
Mitaa ya Kitangiri na Budushi.
Awali
akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu
utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema katika halmashauri ya Mji wa Nzega mradi
ulianza kutekelezwa Novemba, 2023 kwa lengo la kurasimisha vipande vya ardhi
20,000 na kuongeza Alama za Msingi za Upimaji 14.
“Hadi
sasa vipande vya ardhi 18,655 vimetambuliwa, vipande 8,814 vimepangwa na
viwanja 3,960 vimepimwa na Alama za Msingi za Upimaji 14 zimesimikwa ardhini,
kazi hii imetekelezwa kwa asilimia 55 na bado inaendelea na itakamilika kwa
wakati kama ilivyopangwa kwa kuwa sehemu kubwa kazi ambazo zinahitaji utaalam
na muda mwingi zimeshakamilishwa” amesema Mhandisi Sanga.
Kwa
mujibu wa Mhandisi Sanga bajeti
iliyotengwa kutekeleza Mradi huo katika Halmashauri ya Mji Nzega ni Shilingi
bilioni 1.42 ambapo kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 1.396 zilitengwa kwa
ajili ya urasimishaji wa makazi na Shilingi milioni 24.926 kwa ajili ya
kusimika alama za msingi za upimaji.
Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi ameongeza kuwa, hadi kufikia Machi 25, 2024, jumla
ya Shilingi milioni 557.779 zimetumika kutekeleza mradi huo katika Halmashauri
ya Mji Nzega ambazo ni sawa na asilimia 39 ya fedha zilizotengwa.
Aidha,
katika zoezi la upimaji linaloendelea, migogoro 36 imewasilishwa na migogoro 24
imetatuliwa katika kata za Nzega Mashariki, Nzega Magharibi na Kitangiri
na migogoro 12 inaendelea na hatua za
utatuzi ili wananchi wapate haki ya kumiliki ardhi wanayoitumia kwa shughuli za
maendeleo.
Akihitimisha ziara ya Kamati hiyo katika Halmashauri ya mji wa Nzega, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Japhet Hasunga amesema, kazi ya Kamati hiyo ni kuangalia maendeleo ya mradi thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali ambayo imetitishwa na Bunge kwa lengo la kutekeleza mradi huo.
Comments
Post a Comment