MIAKA MITATU YA UONGOZI WA RAIS SAMIA NA KUIMARIKA KWA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
MAKALA
Rushwa
ni tatizo la kidunia lenye madhara makubwa kwa mtu,
jamii, nchi na mataifa kwa ujumla. Rushwa imetumika kupoka haki za watu kwa
kumnyang’anya haki yeye aliyeistahili na kumpa yule asiyeistahili kwa sababu
mwenye jukumu la kutoa haki amepokea hongo au kaahidiwa kupewa hongo ili apindishe
sheria. Ni kwa sababu ya rushwa wapo vijana wanaokosa fursa za masomo au za kupata
mikopo ya kibiashara na wengine kupendelewa na kupewa fursa hizo japo hawana
sifa kwa kuwa wametoa rushwa.
Rushwa imewanyima wananchi wengi hasa maskini fursa ya kupata
huduma bora za kijamii kama vile majisafi na salama, elimu bora, afya, makazi
au miundombinu bora ya barabara kwa fedha inayotengwa kuboresha huduma hizi
kuhujumiwa na watendaji au watu wachache na kuitumia kwa maslahi binafsi.
Tumeshuhudia pia matukio ambayo vitendo vya rushwa vimetumika kuchepusha au
kuvujisha mapato ya Serikali hivyo kuikosesha Serikali fedha ya kutoa au
kuboresha huduma kwa umma.
Mapambano dhidi ya rushwa yametamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 9(h) ambapo Serikali na
taasisi zake zimetakiwa kuhakikisha aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa,
uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini. Ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Machi 19, 2021 siku
ambayo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliapa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na kuahidi kuilinda, kuhifadhi na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, yapo mengi ya kujivunia yaliyofanyika katika mapambano
dhidi ya rushwa nchini katika kipindi hicho.
Alipohutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mnamo Aprili 22, 2021 jijini Dodoma, Rais Samia alieleza dhamira
ya dhati ya Serikali ya kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kutowaonea
aibu viongozi na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma. “Tutaendeleza
pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma,” alisisitiza Rais
Dkt Samia. Dhamira hii inadhihirika kwa matokeo yanayotokana na hatua
zilizochukuliwa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Mathalani, taarifa ya utafiti uliofanywa na Transparency International ya mwaka 2023 kuhusu Corruption Perception Index (CPI) inaonesha kuwa Tanzania imefanya
vizuri na kupata alama 40 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180
zilizofanyiwa utafiti, ikilinganishwa na alama 38 ilizopata mwaka 2022
ambapo ilishika nafasi ya 94. Tanzania, kwa mujibu wa taarifa hiyo, imeshika
nafasi ya pili katika mapambano dhidi ya rushwa katika ukanda wa Afrika
Mashariki ikitanguliwa na nchi ya Rwanda.
Aidha, ili kuimarisha mapambano dhidi ya
rushwa hivyo kuhakikisha ustawi wa umma, Serikali imefanya maboresho ya Sheria ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 ili iendane na mazingira ya sasa ya
kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Muswada wa maboresho hayo ya Sheria upo
katika hatua ya kuwasilishwa Bungeni. Hii ni hatua muhimu katika mapambano
haya.
Pia, Serikali imeimarisha uwezo wa kiutendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuiwezesha kwa rasilimali watu, rasilimali fedha, vitendea kazi pamoja na mafunzo ya weledi kwa watumishi. Mapema mwaka huu 2024, Serikali imetoa kibali cha ajira za watumishi 350 hivyo kufanya idadi ya watumishi wapya wa TAKUKURU katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia kufikia 880. Uimarishaji huu wa TAKUKURU umeifanya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Kutokana na uwezeshaji wa TAKUKURU uliofanywa
na Serikali, kiasi cha Shilingi bilioni
201.72 imedhibitiwa na kurejeshwa Serikalini kupitia operesheni
mbalimbali za uchunguzi wa tuhuma za rushwa pamoja na ufuatiliaji
wa miradi ya maendeleo. Sehemu ya fedha hii imetumika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo kama vile
ujenzi wa vituo vya afya, manunuzi ya dawa na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa shule na barabara
ili kuleta ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa.
Serikali pia imetaifisha mali zenye thamani
ya Shilingi bilioni 2.14 zikijumuisha
nyumba, viwanja na magari. Aidha, miradi ya maendeleo 3,576 yenye thamani
ya Shilingi trilioni 16.76 ilifuatiliwa kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa fedha hiyo inatumika kadiri ilivyokusudiwa ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Vilevile, katika kipindi hiki cha miaka mitatu, uchunguzi wa tuhuma za vitendo
vya rushwa uliendelea na pale penye ushahidi na kwa kibali cha Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP), kesi zilifunguliwa na kuendeshwa mahakamani. Jumla ya kesi
1,922 za rushwa ziliendeshwa
mahakamani zikiwamo kesi 19 zilizofunguliwa
katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama Kuu ya
Tanzania. Mahakama ilitoa maamuzi katika kesi 1,303 za rushwa ambapo katika kesi 801 sawa na asilimia 61 Jamhuri ilishinda baada ya washtakiwa
kupatikana na hatia ya kutenda makosa ya rushwa na kuhukumiwa kifungo jela au
kulipa faini.
Serikali inayoongozwa
na Rais Samia pia imeimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuipatia TAKUKURU
fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi. Fedha hiyo imewezesha kuanzisha na kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za TAKUKURU
za mikoa ya Kilimanjaro na Simiyu na kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za
wilaya saba za Kilolo mkoani Iringa, Kongwa (Dodoma), Kiteto (Manyara), Mvomero
(Mvomero), Liwale (Lindi), Nyasa (Ruvuma) na Momba (Songwe). Vilevile, ujenzi
wa jengo la Makao Makuu jijini Dodoma, majengo mawili ya mikoa ya Iringa na Shinyanga pamoja na
majengo matano ya ofisi za wilaya za Nkasi (Rukwa), Nzega (Tabora), Kishapu
(Shinyanga), Monduli (Arusha) na Rombo mkoani Klimanjaro unaendelea.
Serikali pia imeiwezesha TAKUKURU kwa
fedha ya kuendelea kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu madhara ya
rushwa na kuuhamasisha ushiriki katika mapambano dhidi ya adui rushwa. Hii ni sehemu ya jitihada za
kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ambapo baadhi ya wadau wamehamasika na kuchangia kuzuia vitendo vya rushwa kwa kuacha
kushiriki vitendo hivyo au kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa huku wengine
wakipata ujasiri na kujitokeza kutoa ushahidi katika kesi za rushwa mahakamani.
Uelimishaji umma umefanyika kwa
makundi mbalimbali katika jamii kuanzia vijijini hadi mijini kupitia mikutano,
minada, magulio, midahalo, semina, warsha, mbio za Mwenge wa Uhuru, vipindi vya
redio, vipindi vya televisheni, na machapisho mbalimbali. Pia, elimu kwa umma imetolewa
kupitia maonesho ya kitaifa na kimataifa yanayofanyika kila mwaka nchini kama
vile maonesho ya Wakulima (Nanenane) na Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya
Dar es Salaam (Sabasaba).
Ili kuongeza
ushiriki wa wadau katika kuzuia vitendo vya rushwa, Programu ya TAKUKURU - Rafiki
ilizinduliwa 20 Disemba, 2022. Programu hii imelenga kushirikisha wadau kutatua
kero katika utoaji wa huduma kwa umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ambazo zikiachwa bila kutatuliwa zinaweza kusababisha kutokea kwa vitendo
vya rushwa. Utekelezaji wa Programu hii umekuwa wenye
mafanikio ambapo kero nyingi zilizoibuliwa zimetatuliwa hivyo kuzuia vitendo
vya rushwa na kuboresha huduma zinazotolewa kwa umma.
Katika hatua nyingine, mwaka 2023, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya
Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika jijini Arusha
kuanzia Julai 9-11, 2023. Hii ilikuwa heshima kubwa kwa Taifa na inayoashiria
imani ya Mataifa mengine ya Afrika pamoja na Umoja wa
Afrika kwa Tanzania katika suala la mapambano dhidi ya rushwa. Wadau mbalimbali wa mapambano
haya kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwemo kutoka sekta ya umma, sekta
binafsi na asasi za kiraia walishiriki maadhimisho hayo.
Akihutubia wadau hao siku ya
kilele Julai 11, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
pamoja na mambo mengine aliwatahadharisha watu wanaojihusisha na rushwa kuhusu
mienendo yao. “Walarushwa wanapaswa
kufahamu kuwa nchi zetu si vichaka vya kuficha fedha zilizotokana na rushwa au
kufuga walarushwa. Tunataka dunia nzima ifahamu kuwa, Afrika si salama kwa
walarushwa na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua tunazozichukua dhidi ya
walarushwa”, alisisitiza Rais Samia.
Mheshimiwa Rais Samia
hakuishia kutoa onyo hilo bali aliueleza ulimwengu mafanikio ya hatua
zilizochukuliwa na Tanzania kuidhibiti rushwa, yaani kazi zilizofanyika kuzuia
na kupambana na rushwa. Mathalani, alisema kuwa katika kipindi cha miaka
mitatu, kupitia mapambano dhidi ya rushwa Serikali iliokoa zaidi ya Shilingi bilioni 139 ya fedha ya umma. “Fedha hizo ukinipa mimi sasa hivi nikifumba
macho nakwambia nazipeleka kununua vifaa tiba,” alisema Mhe. Dkt. Samia.
Rais Samia aliwaomba
viongozi barani Afrika kushirikiana katika kupambana na vitendo vya rushwa na
kusisitiza kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo barani Afrika ni janga la
rushwa ambalo linadhoofisha mifumo ya kitaasisi na kuathiri mipango na mikakati
ya kujikomboa kiuchumi. Pia, alitumia jukwaa la maadhimisho hayo, pamoja na
mambo mengine, kumtaka kila Mtanzania kujitathmini ni kwa namna gani anadhibiti
rushwa huku akiirejea kaulimbiu ya TAKUKURU. ‘‘Kuzuia
Rushwa ni Jukumu Lako na Langu ; Tutimize Wajibu Wetu. Ni kaulimbiu nzito
na kaulimbiu inayotupa mtihani hasa sisi Watanzania, tujitizame sisi wenyewe
mmojammoja, tunaendana na kaulimbiu hii ?’’ alihoji Rais Samia.
”Nitasimama imara kwenye mapambano dhidi
ya rushwa” hii ni ahadi aliyoitoa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania wakati anapokea taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU
Machi 28, 2021 katika Ikulu ya Chamwino ikiwa ni siku tisa tangu ale kiapo cha
kuwa Rais. Tunawiwa kusema, ahadi hii ameitekeleza kwa vitendo na Watanzania hatuna
budi kusimama imara na kuungana naye kwenye mapambano haya kwa kuizingatia
kaulimbiu ”Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako
na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akipokea Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Kamishna wa Polisi (CP) Salum
Hamduni katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma tarehe 30 Machi,
2022. (PICHA YA MAKTABA)
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2021/2022 kutoka kwa
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo CP. Salum Hamduni Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe
29 Machi, 2023. (PICHA YA MAKTABA)
Comments
Post a Comment