NCHI WANACHAMA EAPP ZAKUBALIANA KUIPA MSUKUMO MIRADI YA UMEME
Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa
umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika
(EAPP Council of Ministers-COM)
limekubaliana kwa pamoja kuwa na
usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya umeme katika nchi wanachama, ili
iweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia wananchi nishati ya kutosha.
Kukamilika
kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha nchi hizo
kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme huku msisitizo
ukiwekwa kwenye miradi ya usafirishaji umeme.(Transmission lines).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko tarehe 27 Februari 2024 katika Mkutano wa 18 wa
Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika
(EAPP Council of
Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Nairobi, Kenya.
“ Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za
Afrika zinaungana kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja
na kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na
katika Mkutano huu kila nchi imeonesha utayari kufanya biashara ya umeme pale
kunapokuwa na umeme wa ziada.” Amesema Dkt. Biteko
Ameeleza kuwa
kuna idadi kubwa ya watu katika nchi wanachama wa EAPP, hivyo
inahitajika nishati zaidi kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na ndio
maana kila nchi imejikita katika kuendeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ajili ya
kujipatia nishati ya uhakika.
Amesema kuwa, Tanzania itakuwa sehemu ya soko la
umeme pale nchi jirani zitakapohitaji nishati hiyo, na hii ni baada ya kuwashwa
kwa mashine zote Tisa katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo
litazalisha megawati 2,115 ambazo zinatoa uhakika wa kutosheleza mahitaji ya
ndani.
“Tanzania kuna njia mbalimbali za usafirishaji umeme
(interconnectors) mfano Tanzania na Uganda, Tanzania na Burundi pamoja na
Tanzania na Rwanda na sasa kuna laini ya umeme kutoka Tanzania hadi Kenya
ambayo imekamilika na ipo kwenye majaribio itakayotuwezesha kufanya biashara
kati ya nchi hizi mbili pale kila nchi ikiwa na umeme wa kutosha.”Amesema Dkt.
Biteko
Ameongeza kuwa, kuna upembuzi yakinifu unafanyika
chini ya Benki ya Dunia (WB) kwa ajili
ya kujenga mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa msongo wa Kilovoti 400 kutoka
Tanzania hadi Uganda kutokea Shinyanga, ambao
utasafirisha umeme mwingi zaidi kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera na
pia kuwezesha nchi hizo kufanya biashara ya umeme.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa,
Sekta ya Nishati ni injini katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii,
hivyo suala la kupeleka nishati ya kutosha, salama na ya gharama nafuu kwa
wananchi si suala la hiari bali ni wajibu kwa ajili ya shughuli za uzalishaji
na kijamii.
Ameeleza kuwa, ukuaji wa Sekta ya Nishati kwa nchi
za Mashariki mwa Afrika ni asilimia 6 kwa mwaka, hivyo bado kuna kazi kubwa ili
kuhakikisha wananchi katika nchi hizo
wanapata nishati ya uhakika na kwa gharama nafuu.
Amesema chini ya mfumo wa pamoja wa umeme EAPP kuna
miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kuimarisha
upatikanaji wa nishati katika nchi wanachama akitolea mfano mradi wa ujenzi wa
miundombinu ya umeme wa Kenya-Uganda, Kenya-Ethiopia, Kenya-Tanzania,
Tanzania-Rwanda, Tanzania-Uganda, Tanzania-Burundi na DRC-Burundi.
Amesisitiza kuwa, nchi Wanachama zinapaswa
kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kupunguza changamoto za
umeme kwani umeme huo utaweza kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine na
kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika .
Awali, Mwenyekiti wa kikao hicho cha Baraza la
Mawaziri wa Nishati ambaye ni Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Mhe. Davis
Chirchir amesema lengo la nchi kuwa na mfumo huo ni nchi wanachama 13 kufanya biashara ya
mauziano ya umeme pale kunapokuwa na ziada ya umeme, na kwamba ili suala hilo
liwezekane lazima kuwepo na miumbombinu ya umeme inayounganisha nchi hizo.
Amesema kuwa, majadiliano ya viongozi hao yamelenga
katika kuimarisha muundo wa umoja huo pamoja na ushirikiano na hii ikijumuisha
namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za umeme pale zinapojitokeza.
Amesema Kenya tayari inafaidika na mfumo huo wa
umeme baada ya kupokea magawati 200 za
umeme kutoka nchini Ethiopia, hivyo kuongeza kiasi cha umeme katika nchi hiyo.
Ameongeza kuwa, takriban watu milioni 600 bado
hawajapata nishati ya umeme barani Afrika kati ya watu takriban Bilioni 1.5 na
hii ikionesha jinsi nguvu zaidi inavyohitajika ili kuwa na nishati ya kutosha
kuweza kukidhi mahitaji.
Nchi Wanachama wa Umoja wa EAPP ni pamoja na Kenya,
Tanzania, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Somalia, Libya, Ethiopia, Misri,
Djibouti, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wadau wa Maendeleo
ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).
Viongozi wengine wanaoshiriki Mkutano huo kutoka
Tanzania ni Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima-Nyamohanga.
Comments
Post a Comment