HALMASHAURI ZIAJIRI WATUMISHI WA MIKATABA KWA MAPATO YA NDANI
Na. WAF - Lindi
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Halmashauri ikiwemo ya Wilaya ya
Kilwa kuajiri watumishi wa mikataba kwa kutumia mapato ya ndani ili kupunguza
changamoto za uhaba wa wataalamu wa Afya katika Wilaya hizo.
Waziri Ummy amesema hayo Februari 28, 2024 baada ya
kupokea taarifa ya hali ya Afya katika Halmashauri ya Wilaya hiyo iliyotolewa
na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Lusajo Mwakajoka ambayo inaonyesha hali ya
upatikanaji wa huduma za Afya katika Mkoa wa Lindi, upatikanaji wa Vifaa na Vifaa
Tiba pamoja na changamoto.
“Tutatumia njia kuu Tatu ili kupunguza changamoto za
watumishi ikiwa ni pamoja na njia ya vibali vya ajira kutoka Ofisi ya Rais
Utumishi, kuajiri watumishi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja
na wadau wetu wa maendeleo katika Sekta
ya Afya nao wanaajiri ajira za mikataba pamoja.” Amesema Waziri Ummy
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab
Telack amemshukuru Waziri wa Afya Mhe. Ummy kwa kufanya ziara katika Mkoa huo na kumuomba aupe kipaumbele kwa kuwa una
wananchi wengi wa kipato cha chini ambao hushidwa kufata huduma mbali na makazi
yao.
“Vifaa tiba ikiwemo Dawa zinaposambazwa na Bohari
Kuu ya Dawa (MSD) tunaomba wawe wanawahi kwa wakati kwa kuwa wananchi wengi wa
Mkoa wa Lindi wanakipato cha chini, dawa zinapochelewa tunamkwamisha Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwakuwa ameshatoa fedha za dawa, kikubwa ni sisi
watendaji.” Amesema Mhe. Telack
Waziri Ummy anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa
Lindi na anatarajia kutembelea na kukagua hali ya utoaji wa huduma katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi (Sokoine), Hospitali za Wilaya, Vituo vya
Afya pamoja na Zahanati.
Katika ziara hiyo Waziri Ummy ameambatana na timu kutoka Wizara ya Afya akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa Dkt. Caroline Damian anae muwakikisha Mkurugenzi wa huduma za Tiba, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali watu upande wa Hospitali za Rufaa za Mikoa Bw. Danny Temba.
Comments
Post a Comment