RAIS WA IPU AWAOMBA WATANZANIA USHRIKIANO ILI KUONESHA UTOFAUTI

 

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ameomba ushirikiano kutoka kwa Watanzania wote ili kuionyesha Dunia utofauti wa Tanzania kuishika nafasi hiyo. 

Dkt. Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania ametoa kauli hiyo leo Bungeni Dodoma katika halfa ya kumpokea akitokea Nchini Angola ambako alishinda nafasi ya Rais wa IPU katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023. 

Amesema Tanzania inayo nafasi ya kufanya vizuri katika nafasi hiyo iwapo kutakuwepo ushirikiano kutoka kwa watu wote.

“Nafasi hii ni yetu wote, ukiwa na ushauri wa namna ya kuupeleka umoja huu mbele tuletee ili tufanye vizuri, usisuburi tushindwe.

“Ifike mahali tukitaka nafasi nyingine kimataifa tupate kwa kuwa tulifanya vizuri kwenye hii, tutasikiliza ushauri wenu, ninaamini tutafanya vizuri na Dunia itajua kwamba tulishawahi kushika hii nafasi, viongozi wa dini muendelee kutuombea,” alisema.

Alitoa wito kwa Watanzania kuondoa tofauti zao kwenye masuala ya uwakilishi wa Tanzania Kimataifa kwa kuacha kuidharau nchi mbele ya nchi nyingine.

“Nafasi kama hizi siyo za kuzipiga teke, tujitahidi kujizuia hasa katika mambo ya kimataifa, tusifike mahali ya kuiuza au kuidharau nchi yetu kwa wengine, usiungane na adui kwa ajili ya kulipiga Taifa lako,” alisema.

Mheshimiwa Dkt. Tulia alitoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuwesha kupita katika mchakato wa uchaguzi uliodumu kwa miezi mingi na kwamba isingiwezekana bila yeye kutoa kibali.

“Vilevile namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Hasan Suluhu kwa kuridhia nigombee nafasi hii, nafasi kama hii huwezi kugombea bila nchi yako kuruhusu na anayeruhusu ni Mheshimiwa Rais.

“Nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia Bunge la Tanzania kuchukua nafasi hii, pia niwashukuru wote walioshiriki kwa nafasi yao, kwa maombi, maoni, kututia moyo na michango ya kifedha pamoja na waliotukatisha tamaa kwa kuwa ilitufanya tupige hatua kwa haraka zaidi” alisema.

Alisema Mheshimiwa Rais pamoja na kutoa usafiri wa ndege kumrudisha Tanzania, lakini pia ametoa ushirikiano mkubwa ambao ndiyo umemfikisha hapo toka mchakato wa uchaguzi  ulipoanza.

“Hatukuwa peke yetu, wapo marafiki wengine walikuja kutusaidia ili tushinde nafasi hii, tumeungwa mkono na mataifa mengi kwa kuwa wanaamini sera za nchi yetu ambazo zinaendana na misingi ambayo IPU inaisimamia,” alisema

Aidha, Mheshimiwa Dkt. Tulia alieleza historia yake kwa ufupi akitambua mchango wa Mheshimiwa Balozi Dkt. Asha Rose Migiro katika mafanikio yake huku akiahidi kuandika kitabu. 

Waziri Mkuu 

Awali Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa  akitoa salamu za Serikali alisema

Mheshimiwa Rais Samia Hasan Suluhu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wanampongeza kwa ushindi mnono wa nafasi hiyo nyeti.

“Sisi tumefarijika kama Serikali kwa sababu moja kati ya majukumu yako utakuwa unashiriki vikao vyote vya Umoja wa Mataifa, tunayo mikataba mingi katika nyanja za kimataifa, tutakutumia wewe kuingiza ajenda za nchi.

“Tuna uhakika utatupigania, tulikuwa tunakufuatilia katika mchakato wa kuomba kura, kazi kubwa mmeifanya leo tunifurahia kazi hii.

“Mheshimiwa Rais amefurahishwa na akaamua kukuletea ndege kubwa kwa ajili yako na kwa ajili ya ya heshima uliyoileta nchini. Naahidi Serikali itashirikiana na wewe kila hatua, na maeneo ambayo utahitaji Serikali ikupe taarifa kwa ajili ya kwenda kufanyia kazi huko katika majukumu yako tutakupatia,” alisema.

Naibu Spika

Mheshimiwa Naibu Spika, Mussa Azan Zungu alisema mambo matatu ndiyo yalimfanya Mheshimiwa Dkt. Tulia kushinda nafasi hiyo ambayo ni kujiamini, heshima na ukweli huku akisema jambo kubwa zaidi ni kumuamini Mwenyezi Mungu na msaada kutoka kwa Mheshimiwa Rais.

“Sisi tuliogopa uchaguzi lakini Mungu alishasema tunashinda, you deserved it (ulistahili) na umefanya kazi kubwa sana,” alisema. 

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar. 

Naibu Katibu Mkuu CCM, Zanzibar, Dkt. Mohammed Said Mohammed aliungana na wengine wote kumpongeza Dkt. Tulia kwa kuwa Rais IPU wa kwanza mwanamke kutoka Afrika. 

CCM imefarijika sana kupata kiongozi katika nafasi hiyo, nifahari kubwa kwa wanawake wote Barani Afrika hususan wanawake wa Chama Cha Mapinduzi, kuchaguliwa kwa Dkt. Tulia kunaiweka Tanzania kileleni katika ramani ya Dunia kwenye masuala ya demokrasia na usawa wa binadamu kwa kuwa mwanamke kashika nafasi hiyo,” alisema, Katibu wa Bunge.

Mheshimiwa Joseph Mhagama

Mheshimiwa Joseph Mhagama ambaye alikuwa mwenyekiti wa Timu ya Kampeni aliwashukuru watu wote walioshiriki kampeni za kumnadi Mheshimwa Dkt. Tulia wakiwemo wabunge sita wawakilishi wa IPU, wawakilishi wa vyama mbalimbali vya kikanda na kimataifa, mabalozi watatu na sekrearieti ya Bunge. 

“Tunakuopongeza kwa kuleta heshima kwa Taifa, ushindi huu umechangiwa na neema na baraka za mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais kwa kutoa baraka na kuwezesha kwa hali na mali na ushirikiano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

“Ubora wa mgombea wetu, sifa zake lukuki, weledi, maarifa na utaalamu wa hali ya juu, haya yote yamewashinda wapinzani wake wote, sera ya mambo ya nje na mahusiano ya diplomasia ambayo ni bora sana chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Rais imefanya kazi hii iwe nyepesi na umahili wa timu yetu ya kampeni.

Mheshimiwa Shally Raymond

Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Mheshimiwa Shally Raymond alimpongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia kwa niaba ya wabunge wote wanawake . 

“Shukrani kwa wazazi wako, Mungu alisema ukijitahidi utakuwa kichwa huwezi kuwa mkia, nawasihi wazazi wengine wawalee Watoto wao vizuri ili tupate kina Tulia wengi. Asante Mheshimiwa Rais kwa kukubariki hili, nakupongeza kwa niaba ya wanawake wote, umeliheshimisha Bunge la Tanzania, Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla,” alisema.

Mheshimiwa Oran Njeza 

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wate alisema wabunge wote walipokea taarifa za ushindi wa Dkt. Tulia kwa furaja na vifijo.

“Shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kuitangaza Tanzania kidiplomasia, nina imani hata IPU utaipaisha na utaonyesha utofauti.Umetupa matumaini makubwa na sisi wana Mbeya tunajivunia,” alisema.

Katibu wa Bunge

Katibu wa Bunge Nenelwa Mwihambi akizungumza katika hafla hiyo alisema kwa ushindi alioupata Dkt. Tuliaunamuwezesha kuwa mkuu wa kisiasa wa chombo hicho ambacho atakuwa akiongoza vikao vya maamuzi.

“Kwa nafasi hii aliyoipata Mheshimiwa Dkt. Tulia atakuwa akiiwakilisha IPU katika mikutano na makongamano mbalimbali ya kimataifa. IPU inafanya kazi kwa ukaribu na Umoja wa Mataifa (UN) hivyo Mheshimiwa Rais wa IPU atakuwa anashiriki vikao vya UN.

“Tunaimani kwa uwezo na uzoefu wako utayatekeza majukumu yote uliyoanayo kwa ufanisi na viwango, mimi na watumishi wenzangu tutafanya kila liwezekalao kukuwezesha kutekekeza majukumu yako,” alisema.







Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"