TANZANIA, USWISI NA IRELAND ZASAINI MKATABA WA KUNUSURU KAYA MASIKINI.
Na Scola Malinga na Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam.
Serikali
ya Tanzania imesaini mikataba miwili ya msaada yenye thamani ya dola za
Marekani milioni 20.3 sawa na shilingi bilioni 50.13 kwa ajili ya kunusuru kaya
masikini awamu ya pili (PSSN II).
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba alisema msaada huo umetolewa
na Serikali ya Uswisi dola za Marekani milioni 18 na Euro milioni 2.2 sawa na
dola za Marekani milioni 2.3 zimetolewa na Serikali ya Ireland.
"Kiasi
cha misaada kilichosainiwa leo ni mwendelezo wa misaada mingine iliyopokelewa
kutoka kwa serikali hizi mbili ambapo misaada ya kipindi cha nyuma kwa mpango
huu wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili ilikuwa faranga za Uswisi milioni
15.72 sawa na dola za Marekani milioni 17.1 kutoka serikali ya Uswiss na Euro
milioni 2 sawa na dola za Marekani milioni 2.1 kutoka serikali ya Ireland.
," alisema Dkt. Mwamba.
Alisema
misaada hiyo imewezesha serikali kufanya kazi yao kuwa rahisi katika kuleta
maendeleo kwa watanzania wote.
Aidha,
PSSN II inaendana na Dira ya Tanzania ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo inatoa
mwelekeo wa juhudi za kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii hadi kufikia
mwaka 2025.
"Dira
hii kwa sasa inatekelezwa kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa kipindi
cha mwaka 2021/22 hadi 2025/26 ," alisema Dkt. Mwamba.
Alisema
kwamba pia misaada hii pia inaendana na lengo la kwanza la Malengo ya Maendeleo
Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambalo linalenga kuondoa umaskini wa aina zote
ifikapo mwaka 2030, na ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 ambayo inalenga kuwezesha
mpango wa Afrika kufikia ukuaji jumuishi na endelevu wa uchumi na maendeleo
ifikapo mwaka 2063.
Alisema
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umewezesha wanafunzi kutoka Kaya maskini kupata
elimu ya sekondari na elimu ya Juu. Mwaka 2022 wanafunzi 2,950 kutoka kaya
maskini walipata mkopo wa asilimia 100 kutoka bodi ya mikopo ya Elimu ya juu
chini ya msaada wa PSSN II.
Aidha
alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeanza kuimarika ambapo katika robo ya
kwanza ya mwaka 2023 ukuaji ulikuwa ni asilimia 5.6.
Alisema
kwa mwaka 2019 kabla ya UVIKO – 19, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakuwa kwa
asilimia 7 lakini ukuaji huo ulishuka na kuwa asilimia 4.8 mwaka 2020 kutokana
na madhara ya UVIKO – 19 na mwaka 2021 ukuaji ulipanda hadi asilimia 4.9 kabla
ya kushuka kuwa asilimia 4.7 mwaka 2022 kutokana na madhara ya vita vya Ukraine
na Urusi.
"Natumaini
misaada yenu kupitia PSSN II itawezesha kaya nyingi maskini kuondokana na
umaskini na kuchangia ukuaji wa pato la taifa," alisema Dkt. Mwamba.
Dkt.
Mwamba alisema bajeti yote ya PSSN II ni dola za Marekani milioni 883.32 ambapo
watafikia malengo yaliyokusudiwa ifikapo mwishoni mwa PSSN II mwwezi Septemba
2025 kwa kuwezesha kaya maskini kupata huduma za kijamii na kiuchumi.
Dkt.
Mwamba alisema Serikali za Uswisi na Ireland siyo tu wanachangia kwa mpango wa
kunusuru kaya maskini lakini pia wanachangia sekta nyingine zikihusisha Afya,
Elimu, Haki za Binadamu, Utawala bora na Demokrasia.
Dkt.
Mwamba aliwahakikishia utayari wa Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia
Suluhu Hassan kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi hizo kwa maendeleo ya
watu wetu na kuahidi kuwa msaada uliotolewa utatumika kwa malengo
yaliyokusudiwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray, alisema PSSN II itaboresha upatikanaji wa fursa za mapato na huduma za kijamii na kiuchumi kwa kaya zenye uhitaji sambamba na kuimarisha na kulinda rasilimali watu ya watoto wao.
Alisema
TASAF hadi sasa imefikia walengwa milioni Moja na laki tatu huku wakiwa wametoa
ruzuku ya shilingi bilioni 7.78, pia wametoa ajira 760,000 na vikundi 50,000
vimewezeshwa kiuchumi.
"PSSN
II itafikia malengo yake kupitia utekelezaji wa hatua zilizojumuishwa, kuongeza
mapato ya kaya kupitia kujenga na kufanya kaya kujiamini, kuimarisha udhibiti
na kuwezesha kuwepo kwa ajira zenye tija zaidi," alisema Mziray .
Naye
Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot, alisema msaada walioutoa
ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Uswisi, tangu mwaka 2020
serikali ya Uswisi imekuwa itoa misaada kwenye PSSN .
Balozi
wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Mary O'neil, alisema ushirikiano wa Tanzania
na Ireland ni wa zaidi ya miaka 40, kwa kipindi hicho chote wamekuwa wakisaidia
katika kuwawezesha wanawake, sera, amani na kaya masikini.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia) na Balozi wa Uswisi
nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot (kushoto), wakionesha hati ya makubaliano
ya msaada wa Dola za Marekani milioni 18 (sawa na shilingi bilioni 44.4 za
Tanzania), kwa ajili ya kufadhili mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili
(PSSN II) unaosimamiwa na TASAF, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini
Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kushoto) na Balozi wa
Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania, Mhe.
Mary O’neil (kulia), wakibadilishana hati ya makubaliano ya msaada wa Dola za
Marekani milioni 2.3 (sawa na shilingi bilioni 5.6 za Tanzania), kwa ajili ya
kufadhili mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili (PSSN II) unaosimamiwa
na TASAF, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kushoto) na Balozi wa
Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania, Mhe.
Mary O’neil (kulia), wakisaini hati ya makubaliano ya msaada wa Dola za
Marekani milioni 2.3 (sawa na shilingi bilioni 5.6 za Tanzania), kwa ajili ya
kufadhili mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili (PSSN II) unaosimamiwa
na TASAF. katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia) na Balozi wa Uswisi
nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot
(kushoto), wakisaini hati ya makubaliano ya msaada wa Dola za Marekani milioni
18 (sawa na shilingi bilioni 44.4 za Tanzania), kwa ajili ya kufadhili mpango
wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili (PSSN II) unaosimamiwa na TASAF. katika
ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu Ikulu, Bw. Mululi Majula Mahendeka (Katikati), Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa pili kushoto), Balozi wa Jamhuri ya Ireland
nchini Tanzania, Mhe. Mary O’neil (wa kwanza kushoto), Balozi wa Uswisi nchini
Tanzania, Mhe. Didier Chassot na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw.
Shedrack Mziray, wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa ubalozi wa
Ireland na Uswizi, watumishi wa Wizara ya Fedha na TASAF, baada ya kusaini
mikataba miwili ya msaada; Dola za Marekani milioni 18 (sawa na shilingi
bilioni 44.4 za Tanzania), kutoka Serikali ya Uswisi na Dola za Marekani
milioni 2.3 (sawa na shilingi bilioni 5.6 za Tanzania) kutoka Serikali ya
Ireland kwa ajili ya kufadhili mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili
(PSSN II) unaosimamiwa na TASAF. Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Benki
Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment