SERIKALI KUENDELEA KULINDA THAMANI YA SHILINGI
NA FARIDA RAMADHANI, WF, DODOMA
Serikali
imesema kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kulinda thamani ya shilingi
ya Tanzania ikiwemo kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia
uwekezaji kutoka nje.
Hayo
yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck
Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemas
Maganga, aliyetaka kujua mikakati ya Serikali kuongeza thamani ya shilingi ya
Tanzania ikilinganishwa na nchi jirani za Afrika Mashariki.
Mhe.
Nchemba alisema Serikali inaendelea kulinda thamani ya shilingi nchini ikiwa ni
pamoja na shughulikia tatizo la upungufu wa dola ili kuweza kukabiliana na
changamoto inayoendelea kutokea duniani.
Alisema
miongoni mwa hatua zinachukuliwa na Serikali ni pamoja na kushirikisha Sekta
Binafsi katika kuimarisha mikakati ya kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya
nchi pamoja na kuhimiza wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma
zinazozalishwa hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni.
“Kuendelea
kusimamia utekelezaji wa kifungu 7(3) na 13(1) cha Kanuni za Fedha za Kigeni za
mwaka 2022, zinazoelekeza wafanyabiashara kuweka katika benki zilizopo nchini
fedha za mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ndani ya siku 90 tangu siku ya
kusafirisha bidhaa au kutoa huduma na wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka
nje kufanya malipo kwa kutumia benki na taasisi nyingine za fedha zilizopo
nchini”, alibainisha Mhe. Nchemba kuwa ni miongoni mwa hatua za kunusuru thamani
ya shilingi nchini.
Alisema
Serikali pia itaendelea kusimamia kwa karibu wazalishaji wa ndani ili kuongeza
ubora katika uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa lengo la kupunguza uagizaji wa
bidhaa kutoka nje ya nchi.
Waziri
huyo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa
fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu na kusimamia utekelezaji wa sera ya
fedha ili kuhakikisha utulivu wa mfumuko wa bei nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Nchemba amelieleza Bunge kuwa hesabu zinazowasilishwa na maafisa masuuli kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka ni za uhakika kwa kuwa zinaandaliwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 30 (2) cha Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348, viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (IPSAS), miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na mifumo madhubuti ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha ikijumuisha Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE).
Dkt.
Nchemba alieleza hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde Mhe. Mohammed
Said Issa, aliyetaka kujua uhakika wa hesabu zinazowasilishwa na CAG kila
mwaka.
Aidha
alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2019/20 – 2021/22),
taarifa ya CAG imeonesha ongezeko la hati zinazoridhisha kutoka asilimia 92
mpaka 96 kwa Serikali Kuu, asilimia 70 mpaka 94 kwa Serikali za Mitaa, na
kupungua kutoka asilimia 97 mpaka 98 kwa mashirika na taasisi nyingine za umma.
Comments
Post a Comment