KWA MARA YA KWANZA MATIBABU YA UZIBUAJI WA MISHIPA YA DAMU YA MIGUU YAFANYIKA NCHINI
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) imefanya upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya miguu
iliyoziba kwa wagonjwa 100 wenye matatizo hayo kwa kutumia mtambo wa Cathlab
kuzibua mishipa hiyo.
Matibabu hayo yamefanyika katika kambi
maalumu ya matibabu ya siku tano inafanywa na madaktari bingwa wa moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mwenzao kutoka
Hospitali ya BLK iliyopo nchini India.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema hadi leo tayari wagonjwa 40 wameshapatiwa matibabu na hali zao
kuendelea vizuri ambapo baadhi ya wagonjwa tayari wameruhusiwa.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari
bingwa wa moyo na mishipa ya damu alisema matatizo ya mishipa ya damu ya miguu
kuziba yapo kwa wingi katika jamii na mara nyingi huwapata wagonjwa wa
kisukari, wagonjwa wa shinikizo la juu la damu pamoja na watu wanaovuta sana
sigara na kunywa sana pombe.
“Wagonjwa wengi wenye matatizo ya mishipa
ya damu ya miguu kuziba wamekuwa wakikatwa miguu kwa kuchelewa kupata matibabu
ama wengine kutokujua tatizo linalowasumbua hivyo kufikia hatua ya kukatwa
miguu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI imeona tatizo
la mishipa ya damu ya miguu kuziba linaongezeka kwa kasi hivyo kuamua kuanzisha
huduma ya matibabu hayo na kuifanya endelevu kusaidia wagonjwa wanaosumbuliwa
na matatizo hayo.
“Baada ya kambi hii madaktari wetu
wataendelea kutoa huduma ya matibabu ya mishipa ya miguu baada ya kupata ujuzi
kutoka kwa wenzetu wa hospitali ya BLK iliyopo nchini India”, alisema Dkt.
Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI inaenda
kuanzisha huduma nyingine mpya kwa kushirikiana na mabingwa wa Hospitali ya BLK
iliyopo nchini India ya kuzibua mishipa ya damu iliyoziba na kusababisha
matatizo ya nguvu za kiume kupungua ili kuwasaidia wagonjwa wanaosumbuliwa na
matatizo ya nguvu za kiume.
Kwa upande wake daktari bingwa wa moyo
na mishipa ya damu kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini India Suhail Bukhari
alisema hii ni mara ya kwanza wataalamu kutoka Hospitali ya BLK kutoa huduma
katika Taasisi hiyo lengo likiwa ni kutoa ujuzi kwa wataalam wa JKCI pamoja na
kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya damu ya miguuni kuziba.
Dkt. Suhail alisema upasuaji wa kuzibua
mishipa ya damu ya miguu iliyoziba unafanyika kwa utaalamu wa kisasa hivyo
kuwasaidia wagonjwa kuondokana na maumivu na changamoto walizokuwa wakipita.
“Nimeongea na Mkurugenzi wa JKCI na
kumshauri kuwa na idara tofauti za upasuaji wa mishipa ya damu ili kusaidia
wagonjwa wenye mishipa ya damu ya miguu kuziba kupata huduma kwa haraka na
kufanya matibabu haya kujulikana Afrika yote”, alisema Dkt. Suhail.
Naye Daktari bingwa wa moyo na mishipa
ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. George Longopa alisema
mwamko wa wagonjwa kupata huduma katika kambi hiyo umekuwa mkubwa tofauti na
ilivyotarajiwa hivyo kuonyesha kuwa tatizo la mishipa ya damu ya miguuni kuziba
kuwa kubwa.
“Tulipotoa tangazo kuhusu matibabu haya
wagonjwa zaidi ya 200 walijitokeza hivyo kuwagawanya katika makundi na kuanza
na wagonjwa 100 katika kambi hii, wagonjwa wengine waliobaki tutaendelea
kuwahudumia kwani tayari tumeshapata ujuzi”, alisema Dkt. Longopa.
Dkt. Longopa alisema wagonjwa wenye
matatizo ya mishipa ya damu ya miguuni kuziba sasa watakuwa wanapatiwa matibabu
JKCI na wale ambao watakuwa na matatizo makubwa zaidi wataendelea kushirikiana
na wataalam wa afya kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini India ili ujuzi
uzidi kukuwa na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kwaajili ya
matibabu.
Naye Betha Mkwawa aliyepata matibabu
katika kambi hiyo alisema amesumbuliwa na maumivu ya miguu kwa muda wa miaka
zaidi ya kumi bila kujua kama mishipa yake ya damu kwenye miguu imeziba.
Betha alisema baada ya kupata ajali na
kuvunjika mguu alipatiwa matibabu nchini India miaka 13 iliyopita na baada ya
matibabu hayo alianza kuumwa mguu lakini kila alipoenda hospitali kutibiwa
aliambiwa maumivu anayoyapata yanatokana na ajali aliyoipata.
“Nimehangaika sana na huu mguu hadi mwaka
2017 nilipogundulika kuwa mishipa yangu ya damu ya miguu imeziba haiwezi
kupitisha damu vizuri nikaanzishiwa dawa hadi mwaka huu nilipoona tangazo la
matibabu ya mishipa ya damu ya miguu kuziba nikaona ni wakati sasa wa kufika
hapa JKCI na kutibiwa”,
“Namshukuru Mungu nimepata matibabu na
baada ya matibabu tu nimeona mabadiliko kwani sasa mguu wangu umekuwa mwepesi,
maumivu hakuna, hali ya kuvimba imeondoka sasa mguu umenywea naamini na hii
hali ya mguu kuwa mweusi inaenda kuisha”, alisema Betha.
Comments
Post a Comment