KAMBI YA MATIBABU YA MOYO YAOKOA MIL. 493
Na Salome Majaliwa.
Taasisiya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha shilingi milioni 493 ambazo Serikali ingetumia kama wagonjwa 15 wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
Dkt. Peter Kisenge alisema katika kambi hiyo maalum ya siku tano ya matibabu ya
moyo iliyofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa
Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani wameweza kuwafanyia upasuaji
wagonjwa ambao walihitaji kurekebishiwa mfumo wa umeme wa moyo kwa ufasaha wa
hali ya juu.
Dkt. Kisenge alisema pamoja na
wataalam hao kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa pia wametoa mafunzo kwa wataalam
wa afya wa JKCI hivyo kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya mfumo wa umeme
wa moyo katika Taasisi hiyo.
“Gharama za matibabu za wagonjwa hawa
15 ni shilingi milioni 253 lakini kama wagonjwa hawa wangeenga kutibiwa nje ya
nchi wangetumia shilingi milioni 746. Serikali imeweza kuokoa kiasi cha
shilingi milioni 493 kwa wagonjwa hawa kutibiwa ndani ya nchi”, alisema Dkt.
Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge amewaomba wananchi
kukata bima za afya ili kupata huduma za matibabu kwa urahisi pale wanapohitaji
huduma hizo kwani matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo ni ya gharama.
“Bima ya afya kwa wote
itakapoanzishwa nawaomba wananchi mjitokeze ili mpate fursa ya kupata matibabu kwa
urahisi kwani ugonjwa utokea wakati wowote na unaweza kukukuta hauna fedha
lakini unapokuwa na bima ya afya itakupa urahisi wa kupata matibabu”, alisema
Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa JKCI Yona Gandye alisema katika
kambi hiyo wamewatibia wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yalikuwa chini na
wengine mapigo yao ya moyo yalikuwa juu
sana .
“Tumewatibia wagonjwa ambao mapigo
yao ya moyo yanazalishwa kwa kiwango cha chini sana kwa kuwawekea kifaa kisaidizi cha moyo ambacho
kinausaidia moyo kufanya kazi vizuri (pace maker) na wale ambao mapigo yao ya
moyo yako juu sana tumeyapunguza kwa
kutumia mtambo wa Carto 3”, alisema Dkt. Gandye.
“Katika kambi hii wagonjwa sita walikuwa na
matatizo katika mfumo wa uzalishaji wa mapigo ya moyo hivyo mioyo yao kwenda
haraka sana na kusababisha moyo kutanuka, wagonjwa wawili walibadilishiwa vifaa
visaidizi vya moyo vilivuokuwa vimeisha
muda wake”,
“Wagonjwa watano ambao mapigo yao ya
moyo yalikuwa chini waliwekewa vifaa visaidizi vya moyo (pace maker) hawa
mapigo yao ya moyo yalikuwa yapo chini sana, na wagonjwa wengine wawili mapigo
yao ya moyo upande wa kushoto yalikuwa hayazalishi umeme wa moyo vizuri”, alisema
Dkt. Gandye.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo
nchini Marekani Prof. Matthew Sackett alisema wamekuja katika Taasisi hiyo kuboresha
huduma za matibabu kwa wataalam wa afya wa JKCI kuifanya Taasisi hiyo kuwa
kituo cha kibingwa cha matibabu ya moyo kusini mwa jangwa la Sahara.
“Nchi nyingi za ulaya hutoa matibabu haya, tukaona ni vyema tusogeze huduma hizi na nchi za Afrika ili nao waweze kupata huduma kwa urahisi na kwa karibu ndio maana tumeendelea kushirikiana na Taasisi hii kuboresha huduma za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo”, alisema Prof. Sackett
Comments
Post a Comment