WAZIRI TABIA MAULID MWITA AWATAKA MAAFISA HABARI SERIKALINI KUHUWISHA TAARIFA KWENYE TOVUTI NA MITANDAO YA KIJAMII YA SERIKALI
NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
WAZIRI
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe.
Tabia Maulid Mwita amefunga Kikao Kazi cha 18 cha Maafisa Habari, Mawasiliano
na Uhusiano kutoka Serikalini (TAGCO) na kuwataka kuhuwisha taarifa zilizomo
kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya Serikali.
Ameyasema
hayo Machi 30, 2023 mbele ya washiriki kutoka Tanzania Bara na Tanzania
Zanzibar kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)
jijini Darves Salaam .
“Niwangapi
kati yenu ambao mmetekeleza agizo la Waziri wa Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye aliyewataka kuhakikisha taarifa za
serikali zinawekwa mara kwa mara kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ili kuwa
na ufanisi katika kutumia njia za kisasa za mawasilino katika utoaji taarifa
kwa umma?.” Aliuliza.
Alisema
anaungana na Mhe. Nape ambaye alisema baadhi ya tovuti na mitandao hiyo ya
serikali ina taarifa za muda mrefu zilizopitwa na wakati.
“Tuna
kazi kubwa mbele yetu ya kufanya nawasihi mnapotoka hapa muende kutumia elimu
mliyopata ili kupeleka mabadiliko kwa kuondoa taarifa hizo za muda mrefu na
kuweka taarifa mpya ambazo ziko nyingi na zina tija.”Alisisitiza Mhe. Mwita.
Alisema
ulimwengu wa sasa unakwenda na mitandao ya kijamii inayofatiliwa na wananchi
wengi.
Alisema
Maafisa hao wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha Serikali inatoa taarifa kwa umma
kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Toeni
taarifa hususan takwimu za miradi, fedha zilizotumika, manufaa ya miradi husika
kwa maendeleo ya wananchi na wajibu wa wananchi katika miradi husika.”
Alibainisha.
Akimkaribisha
Waziri Mwita, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.
Mhandisi Kundo Mathew alisema madhumuni ya kikao yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kupitia ushirikiano wa Wizara, Idara ya Habari Maelezo na TAGCO.
Alisema
Kikao Kazi cha 18 kilishirikisha Maafisa Habari kutoka Wizara zote, Idara na
Taasisi za Umma na Serikali Kuu, TAMISEMI na Sekretarieti za Mikoa.
Alisema
Wizara inaelewa umuhimu wa Maafisa Habari, Mawasiliano serikalini ambao ni
daraja la mawasiliano ya Serikali na wananchi wake.
Jukumu
la msingi la Maafisa hao ni kuisemea serikali kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu
utekelezaji wa miradi ya maendeleo, miradi ya kimkakati na kujenga mawasiliano
chanya na vyombo vya habari, wananchi na taasisi binafsi, alisema Mhandisi
Kundo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa TAGCO, Bi. Sarah Kibonde kwa niaba ya wanachama wa
Chama hicho amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya Sita kwa kutatua changamoto ya muda
mrefu ya muundo wa vitengo vya Habari, Mawasiliano na Uhusiano vya Serikali.
Amesema jambo hilo limeinua morali na nguvu ya kufanya kazi kwa bidii katika kuisemea na kuiunganisha Serikali na wananchi. "Jambo lingine la kumshukuru Mhe. Rais na Serikali yake kwa ujumla ni nia yake thabiti ya kutaka na kuelekeza maafisa wake wa habari tutumike ipasavyo katika kutekeleza majukumu yetu katika Wizara na Taasisi za Umma, jambo hili linatupa nguvu ya kusimamia na kutekeleza majukumu yetu ya kihabari.” Alisisitia Bi. Sarah Kibonde.
Washiriki wa Kikao hicho watakamilisha siku ya tano ya mafunzo kwa kufanya ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na Mradi wa Kimkakati wa ujenzi wa reli ya Kisasa SGR Ijumaa Machi 31, 2023.
Katibu Mkuu wa TAGCO, Bw. Abdul Njaidi
Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maafisa Habari Zanzibar (ZICOO), Bi. Raya Hamad Suleiman, akitoa neno la shukrani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Selestine Kakele (katikati) akikabidhiwa shati la TAGCO na Mwenyekiti Bi. Sara Kibonde na Katibu Mkuu Bw. Abdul Njaidi. Kwa takriban siku nne za Kikao hicho Bw. Kakele amekuwa akisimamia kikao hicho kama Mwenyekiti.
Wajumbe wa Kamati Tendaji ya TAGCO wakungana na washiriki kupongeza hotuba ya mgeni rasmi.
Comments
Post a Comment