TSB KUANZISHA KLABU SHULENI ZA KUTANGAZA ZAO LA MKONGE
Katika
kampeni yake ya kuhamasisha kilimo cha Mkonge nchini, Bodi ya Mkonge Tanzania
(TSB), iko kwenye mchakato wa kuanzisha klabu za wanafunzi katika shule za
sekondari kwa lengo kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia kilimo hicho.
Mkurugenzi
Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema hayo jana katika mahafali ya Kidato cha Sita
ya Shule ya Sekondari Coastal jijini Tanga ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Pamoja
na mambo mengine amesema kwa kuanza na klabu hizo wataanza na shule hiyo kwa
majaribio kabla ya kuhusisha shule nyingine huku akiahidi kulifanyia kazi ombi
la uongozi wa shule hiyo kuwapatia ardhi kwa ajili ya kulima Mkonge.
“Kama
mnavyofahamu Bodi ya Mkonge ni taasisi ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ni kama
imekufa sasa tumekuja kama kuifungua rasmi ofisi kama jengo na sekta ya Mkonge
kwa ujumla wake.
“Lakini
tunategemea tunapokwenda mbele vijana wengi sana kutoka kwenye shule za Tanga
ndiyo wahusike kwenye mpango mzima wa kuleta mapinduzi kwenye zao la Mkonge
kwani sasa hivi tunapozungumzia mkonge tunazungumzia bidhaa moja tu ya nyuzi za
mkonge zitengeneze vikapu, makapeti, magunia, kamba na bidhaa nyingine
zitokanazo na Mkonge,” alisema.
Mkurugenzi
Kambona alisema Mkonge ni zao ambalo mnyororo wake wa thamani una shughuli
nyingi sana ambazo zinaweza zikafanywa kwa vijana ambapo kama tafiti
zitafanyika vizuri zitazalisha ajira nyingi.
“Tunapokwenda
mbele tunataka ikiwezekana tufungue klabu kwenye shule ya zao la Mkonge, ile
mipango ya kuhusisha wanafunzi kwenye vile vitalu vya kuwajenga vijana kwa
ajili ya kuendeleza zao la Mkonge itaanza kwa kuihusisha Shule ya Coastal.
“Bodi
ya Mkonge pia tunafikiria tuwe na miradi ya wanafunzi ambayo tutaifadhili,
watafanya tafiti mbalimbali kwenye zao la Mkonge kuangalia mabaki ya Mkonge
kama sasa hivi tunaambiwa kwamba kwenye Mkonge unaweza ukapata ethanol, unaweza
ukatengeneza pombe ya tequila, sukari ya mkonge, kuzalisha uyoga na mengine,”
alisema.
Alisema
Serikali ya Tanzania imepitia katika hatua mbalimbali za kielimu tangu tupate
uhuru na kila hatua imelenga katika lengo la kumfanya mhitimu wa masomo fulani
kuwa na ujuzi utakaomwezesha kuyatawala mazingira yake.
“Sasa
hivi kuna tatizo kubwa la ajira kuna vijana wengi wamesoma ngazi za chuo kikuu
lakini hawana kazi mtaani ambao wamesoma lakini hawana ajira mbaya zaidi ni
kuwaona vijana hao wakiwa wamekaa tu bila kujishughulisha na hapo ndiyo
utajiuliza je elimu yao imewasaidia nini kama vijana hawa hawawezi kujiajiri
hata kidogo.
“Hivyo
nawaasa wahitimu mnapoingia mtaani msibweteke, jitahidini kujishughulisha na
mambo mbalimbali yatakayowaingizia kipato ikiwezekana mje Bodi ya Mkonge
tuwapatie mashamba,” alisema.
Kuhusu
ombi uongozi kwamba Bodi inaweza kuangalia namna gani itaisaidia shule hiyo
kuipatia ardhi kama shule ikiwa sehemu ya kuiongezea mapato alisema Bodi
itajitahidi kuhakikisha inawapatia ardhi isiyopungua ekari 100.
“Bodi
itajitahidi kutekeleza hilo pamoja na kuwapatia masuala ya ushauri wa kiufundi
wa namna gani mnaweza mkaanza kilimo cha Mkonge na wataalamu wangu wa TSB
watajihusisha moja kwa moja na uongozi wa shule kuhakikisha tunaanza jambo
hili.
“Tuna
maombi mengi yanayosubiri bado ya taasisi mbalimbali hatujayasahau hayo maombi
tunatumaini yatakwenda sambamba na maombi haya ya shule,” alisema.
Awali,
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joseph Gasper alisema kutokana na changamoto ya
kusuasua kwa malipo ya ada kutokana na changamoto za kiuchumi na kijamii lakini
kubwa zaidi ni shule kutegemea chanzo kimoja cha fedha ambacho ni ada ambapo
alimuomba Mkurugenzi Kambona kuwapatia ardhi kwa ajili ya kulima Mkonge kama
chanzo mbadala cha fedha.
“Lakini pia tungependa kuanzisha uhusiano na taasisi mbalimbali ikiwamo Bodi ya Mkonge ikiwezekana kufungua klabu zinazoendana na malengo yao lakini pia kutumia shule na wanafunzi kama mabalozi wa bidhaa mfano kutangaza zao la Mkonge.“Tukiwa wadau wa Mkonge, mwaka huu shule iliandaa Makala maalumu ya utunzaji wa mazingira na kuhamasisha utalii inayoitwa ‘Urithi wa Pwani’ ambapo vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani Tanga ikiwamo zao la Mkonge vimetangazwa na washiriki wakuu walikuwa wanafunzi wetu wa Klabu ya Mazingira na Utalii ambao wengi ni kidato cha sita,” alisema.
Comments
Post a Comment