WAZIRI UMMY MWALIMU ATOA WITO KWA WAZAZI NA WALEZI KUSIMAMIA KIKAMILIFU CHANJO KWA WATOTO

 Na Englibert Kayombo, WAF - Dar Es Salaam.

Wito umetolewa kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano (5)wanapata chanjo zote muhimu zinazotolewa ili kuwajengea kinga imara ya kukabiliana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Jijini Dar Es Salaam ambapo hivi sasa kuna ongezeko la watoto wanaougua ugonjwa wa Surua.

“Nilitoa taarifa kwamba tunaona ongezeko la watoto wenye ugonjwa wa Surua nchini Tanzania na ongezeko hilo tunaliona katika WIlaya ya Temeke, Daktari ametuambia kuwa hapa wanapata watoto wanaougua ugonjwa wa Surua takribani watano kila siku katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke” amesema Waziri Ummy.

“Nitoe wito kwa Wazazi na Walezi wenzangu kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata chanjo zote muhimu ikiwemo chanjo ya Kifua Kikuu, Polio, na Surua” amesisitiza Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amesema kuwa Wizara ya Afya itaweka mpango jumuishi wa kuhakikisha kwamba wataalam wanapokwenda kutoa huduma za mkoba wajumuishe kutoa chanjo nyinginezo ikiwemo chanjo ya Surua.

“Tutahakikisha tunapokwenda nyumba kwa nyumba, Kijiji kwa Kijiji, Kata kwa Kata kutoa chanjo ya Polio tutoe pia chanjo ya Surua kwa sababu tumeona ongezeko ni kubwa sana la ugonjwa huu ambao unaweza kuleta madhara makubwa sana na hata kupelekea kifo” amefafanua Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema baadhi ya Wazazi na Walezi wamekuwa hawasimamiii vyema zoezi la chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano na kusababisha watoto kukosa dozi kamili za chanjo hivyo kuwaweka watoto katika hatari ya kuugua magonjwa yanazuilika kwa chanjo.

“Watu wanachelewa, wanaona mtoto ameshafikisha miezi tisa anamuona haumwi ameshakuwa mkubwa hivyo wanapuuzia kusimamia ukamilishaji wa chanjo zote za mtoto” amesema Waziri Ummy Mwalimu huku akikemea hali hiyo na kuwataka Wazazi na Walezi kuwajibika kusimamia chanjo za watoto.

Aidha, Amesema kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Vyombo vya habari na Wadau wa Sekta wataendelea kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo hizo kwa watoto ili Jamii iweze kufahamu na kuwa na uelewa mzuri zaidi juu ya manufaa ya chanjo. 




Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"