WANACHUO WA CHUO CHA UHASIBU, IAA JIJINI ARUSHA WACHANGAMKIA "BOOM VIBES NA NSSF" KWA KUJIUNGA NA MFUKO
NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, ARUSHA
KAMPENI ya “BOOM VIBES NA NSSF” yenye lengo la
kuhamasisha Wanachuo kuhusu Hifadhi ya Jamii na Uwekaji Akiba imefanyika kwenye
Chuo cha Uhasibu jijini Arusha (IAA) leo Mei 31, 2022.
Kampeni hiyo ni mkakati wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) chini ya Mpango wa Taifa wa Hifadhi
ya Jamii kwa sekta isiyo rasmi kutembelea taasisi mbalimbali za elimu ya juu na
kati nchini ili kuhamasisha wanachuo kujenga tabia ya kujiwekea akiba kwa
kujiunga na Mfuko na kuchangia kila mwezi ili hatimaye wanufaike na mpango
wenyewe, Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi, NSSF Bi. Rehema Chuma amewaambia wanachuo
hao wakati akitoa Elimu ya Hifadhi ya
Jamii.
Alisema wanachuo ni
wanufaika wakubwa wa mpango huo kutokana na kipato wanachokipata wanaweza
kutenga ziada na kujiwekea akiba NSSF kwa manufaa ya sasa na baadaye.
“Ni
muhimu wewe kama mwanachuo kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba kupitia NSSF,
ukianza kuweka akiba mapema itakuwezesha kuwa na akiba ya kutosha kwa faida ya sasa
na baadaye.” Alisisitiza.
Kuhusu namna ya
kuchangia, Meneja huyo alifafanua kuwa mwanachama wa NSSF anatakiwa kuhakikisha
anachangia kiasi kisichopungua shilingi elfu ishirini (20,000/=) kila mwezi au
zaidi.
“Uwasilishaji
wa michango ya kila mwezi ni rahisi sana unaweza kufanya hivyo kupitia simu
yako ya mkononi ukiwa popote pale, lakini pia unaweza kuwasilisha kupitia benki
au mawakala wa benki.” Alifafanua.
Katika kuunga mkono mkakati
huo wa NSSF, baadhi ya Wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na
Katiba, Mhe.Suma Fyandomo,Mhe.Joseph Tadayo na Mhe. Agnes
Hokororo wameshiriki katika kampeni hiyo ambapo wamesisitiza umuhimu wa
wanachuo kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga na Mfuko na kujiwekea akiba.
Mhe. Joseph Tadayo; “Nilijiunga na NSSF na kuanza kuchangia kabla sijawa mbunge, miaka hiyo ya nyuma ya umri wangu huduma nyingi zilikuwa bure na hata ajira pia zilikuwa tele, kwa sasa hali haiku hivyo mtu anakuwa nacho sio kwa kile anachoingiza bali kile anachoweka, tunahitaji kuwa na utamaduni wa kuweka akiba tena kutokana na kile ulichovuna kutokana na jasho lako.” Mhe. Tadayo.
"Niliwahi kuuza mayai ya kuchemsha, nimeuza mifuko ya kubebea bidhaa, lakini pia nimefanya kazi ya uhudumu kwenye mgahawa na hata nilipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilikuwa nafundisha masomo ya ziada “tuition” na ninyi mnaweza kujiwekea akiba kupitia pato unalopata hapa chuoni la mkopo na wengine fedha za kujikimu kutoka kwa wazazi, lazima tuweke akiba ili kukabiliana na maisha yetu hapo baadaye.” Mhe. Tadayo.
Comments
Post a Comment