SEKTA BINAFSI KUNUFAIKA NA MIKOPO BENKI YA DUNIA
Na
Benny Mwaipaja, Washington DC
TANZANIA
inatarajia kupata dola za Marekani milioni 200 sawa na shilingi za Tanzania,
bilioni 460 kutoka Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake inayoshughulika na
utoaji wa mikopo na misaada kwenye Sekta Binafsi – International Finance
Corporation (IFC), kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo
kupitia sekta binafsi.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba baada
ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia wa
Taasisi inayoshughulika na utoaji mikopo na misaada kwenye Sekta Binafsi
(International Finance Corporation-IFC), Kanda ya Afrika, Bw. Sergio Pimenta, Jijini
Washington DC, Marekani.
Bw.
Tutuba alisema kuwa fedha hizo zittumika kuendeleza shughuli za uzalishaji
kwenye viwanda, maendeleo ya tehama na kusaidia miradi ya wanawake, wenye
ulemavu na vijana kupitia taasisi mbalimbali za fedha.
Alisema
kuwa uwekezaji wa Benki ya Dunia kwenye Sekta binafsi kupitia IFC umefikia dola
milioni 282 kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji na kwamba
kiasi hicho cha nuongeza kitasaidia kuimarisha sekta binafsi na kuimarisha
shughuli za uzalishaji na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini Tanzania.
“Serikali
imewasilisha miradi mbalimbali kwenye Taasisi hii ya Benki ya Dunia inayosaidia
Sekta Binafsi ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia nne ya kuanzia Dar Es
Salaam-Chalinze hadi Dodoma, ujenzi wa hoteli na maduka ya kisasa kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere-Dar es Salaam, pamoja na miundombinu ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo tunataka itekelezwe kwa
njia ya ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma” alisema Bw. Tutuba.
Aidha,
Bw. Tutuba alisema kuwa Taasisi hiyo ya Benki ya Dunia imesema iko tayari
kuhamasisha wawekezaji kutoka kila pembe ya dunia kwenda kuwekeza nchini
Tanzania kupitia sekta za nishati ya umeme jua, upepo na joto ardhi Pamoja na
mradi wa kuzalisha umeme wa Somanga Fungu unaotarajiwa kuzalisha megawati 320
za nishati ya umeme kupitia ubia katia ya Sekta binafsi na Umma.
“Mafanikio
haya ni matokeo ya mkutano kati ya Me. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa IFC, Bw. Makhtar Diop, wakati wa
ziara yake aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Februari 2022, ambapo alimwomba
Kiongozi huyo kuisadia sekta binafsi ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa
Taifa: alisema Bw. Tutuba.
Alibainisha
kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utasaidia kutekeleza Mpango wa Tatu wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wenye thamani za shilingi trilion 114.8
ambao umeainisha kuwa asilimia 40 ya utekelezaji wa mpango huo sawa na shilingi
trilioni 40.6 zinatakiwa kutoka katika sekta binafsi huku asilimia 60 ya
gharama za mpango huo sawa na shilingi trilioni 74.2 zinatakiwa kutoka
Serikalini
Katika
hatua nyingine, kwa mara ya kwanza, Tanzania inatarajia kuwa nchi ya kwanza
kunufaika na hati fungani mpya ya usawa wa kijinsia (Gender Bond)
itakayozinduliwa na Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake inayoshughulika na
utoaji wa mikopo na misaada kwenye sekta binafsi, ambapo kiasi cha dola za
Marekani milioni 10 sawa na shilingi bilioni 24 kinatarajiwa kukusanywa na
zitakazotumika kuwakopesha wajasiliamali kupitia Benki ya NMB.
Makamu
wa Rais wa Benki ya Dunia wa Taasisi inayoshughulika na utoaji mikopo na
misaada kwenye Sekta Binafsi (International Finance Corporation-IFC), Bw.
Sergio Pimenta, alisema kuwa Hati Fungani hizo zinatolewa kwa mara ya kwanza na
Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kunufaika nazo katika Bara la Afrika.
Aidha, Bw. Pimenta aliipongeza Tanzania kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha sekta binafsi na kuahidi kuwa Taasisi yake imekusudia kuongeza fedha zaidi ili kusaidia mipango ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya wananchi wake kupitia uwekezaji kwenye sekta za kilimo biashara, nishati, ujenzi wa miundombinu na kuwasaidia wajasiriamali kufanya biashara.
Mkutano
huo uliohudhuriwa pia na Mkurugenzi anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki wa
Taasisi hiyo ya IFC, Bi. Jumoke Jagun-Dokunmu.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akisalimiana na Makamu wa
Rais wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji Mikopo kwenye Sekta
Binafsi, Kanda ya Afrika (International Finance Corporation-IFC), Bw. Sergio
Pimenta, baada ya mazungumzo yaliyolenga kuisaidia sekta binafsi nchini
Tanzania, mazungumzo hayo yalifanyika Washington DC, Marekani, wakati wa
Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la
Kimataifa-IMF.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fefdha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akiwa katika mkutano na
uongozi wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji mikopo kwenye
Sekta Binafsi (IFC), Jijini Washington DC, Marekani. Kushoto ni Kamishna wa
Idara ya Fedha na Mipango, Bi Sauda Msemo. (Picha
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Washington DC)
Comments
Post a Comment