MNH TENA, WATOTO 7 WALIOZALIWA NA TATIZO LA KUSIKIA, SASA WASIKIA SAUTI KWA MARA YA KWANZA BAADA YA TIBA

Watoto saba waliozaliwa na tatizo la kusikia, leo wamesikia sauti kwa mara ya kwanza baada ya kupandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear Implant) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufanya idadi ya waliopandikizwa hadi sasa kufikia 49 tangu kuanzishwa huduma hii nchini  mnamo Juni 2017.
Kati ya watoto saba waliopandikizwa, watano wamelipiwa na Msamaria Mwema ambaye hakutaka jina lake litajwe ambapo amechangia TZS. 150 Mil sawa na TZS. 30 Mil kwa kila mtoto ikiwa ni gharama za kununua vifaa. Serikali imechangia karibu TZS. 10 Mil kwa kila mtoto. Gharama halisi ya huduma hii ni TZS. 40 Mil ambapo nje ya nchi inagharimu TZS. 100 Mil kwa mtoto mmoja.   
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Sufiani Baruani amesema kuwa upasuaji ulifanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 25-27 Januari mwaka huu na kwamba kwa asilimia kubwa umefanywa na wataalamu wazalendo.
“Tulipoanza upasuaji huu wa kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia tulikuwa tunashirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi lengo ilikuwa ni kuwajengea uwezo wataalamu wazalendo,  lakini kwa sasa uwezo wa wataalamu wetu umefikia asilimia 95 na tukifanya upasuaji huu kwa awamu nyingine wataalamu watakuwa na uwezo wa kufanya wenyewe kwa asilimia 100”, amesema Dkt. Baruani.
Akizungumzia mchakato wa upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo,  Dkt. Edwin Liyombo amesema watoto wanaonufaika na upasuaji huo ni wale ambao mishipa yao ya fahamu ipo vizuri.
“Siyo kila mtoto mwenye tatizo la kutokusikia anafanyiwa upasuaji huu, tunafanya tathmini kuangalia mishipa ya fahamu kama ipo vizuri, ikiwa vizuri anawekewa ila kwa wale ambao mishipa yao ya  fahamu haifanyi kazi kwa sababu yoyote ili hatawekewa kifaa kwa kuwa hata ukimuwekea hakitamsaidia,” amesema Dkt. Liyombo
Dkt. Liyombo amesema kuwa suala la utayari wa wazazi huzingatiwa sana kwa kuwa baada ya kuwekewa kifaa cha kusaidia kusikia maisha ya mtoto hubadilika hivyo kuhitaji uangalizi mkubwa wa wazazi au walezi.

Tanzania ilipeleka wagonjwa 50 nchini India kupanikizwa vifaa hivi kwa kipindi cha miaka 15 kabla ya kuanza huduma hii nchini Juni 2017. Hospitali ya Taifa Muhimbili imetoa huduma hii kwa wagonjwa 49 kwa kipindi cha miaka minne sawa na 98% ya wagonjwa waliopelekwa na Serikali nje ya nchi kwa miaka 15. Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali ya umma nchini na katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki..
Dkt. Shaban Mawala, Bingwa wa Upasuaji wa Pua, Koo na Maskio (MNH) akipandikiza kifaa cha kusikia kwa mtoto aliyezaliwa na tatizo la kusikia.




 

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"