BENKI YA AfDB YAMTAKA MKANDARASI WA MRADI WA UMEME TANZANIA – KENYA KUONGEZA KASI


Na. Peter Haule, WFM, Arusha

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imemtaka Mkandarasi wa Ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Singida - Arusha hadi Isinya nchini Kenya unaogharimu dola za Marekani milioni 258 zilizotolewa kwa mkopo na Benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) na Serikali ya Tanzania, kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ili ifikapo mwezi Desemba mwaka huu uweze kukamilika.

Rai hiyo imetolewa jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anaesimamia nchi tisa za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Eritrea Uganda na Somalia katika Benki hiyo, Bw. Amos Cheptoo, wakati alipotembelea na kukagua Mradi wa Kituo cha Umeme cha Lemugur, mkoani Arusha, ambacho ni sehemu ya mradi mkubwa wa umeme wa Singida- Arusha hadi Isanya Kenya.

Bw. Cheptoo ambaye yuko nchini kwa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi iliyopata fedha za mkopo nafuu kutoka Benki hiyo upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, alisema ni vema mradi huo ukakamilika kwa wakati ili uweze kutoa huduma zitakazochochea maendeleo kwa nchi za Afrika hususani Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Sekta ya umeme ni muhimu katika kuchochea kwa haraka maendeleo ya biashara katika nchi za Afrika, miundombinu ya umeme nchini Tanzania ikiunganishwa na ile ya Kenya ambayo tayari imeunganika na Ethiopia na upande mwingine wa Tanzania imeunganishwa na Zambia, itasaidia biashara ya nishati hiyo kufanyika kwa haraka katika upande wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika”, alisema Bw. Cheptoo.

Alisema Nishati ya umeme imepewa kipaumbele kikubwa na  Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kutokana na umuhimu wake, hivyo asilimia 16 ya uwekezaji unaofanywa na Benki hiyo nchini Tanzania ni ya Nishati hiyo.

Bw. Cheptoo alisema zipo sekta nyingine ambazo zinamanufaa makubwa kwa ukuaji wa uchumi katika Bara la Afrika kama sekta ya ujenzi hususani katika uwekezaji wa miundombinu ya Reli, lakini uwekezaji wake una gharama kubwa ikilinganishwa na miundombinu ya nishati ya umeme.

Kwa upande wake mratibu wa Mradi wa Umeme kati ya Tanzania na Kenya (KTPIP), Bw. Peter Kigadye, alisema kuwa   mradi huo wa umeme unaounganisha Tanzania na Kenya, ni sehemu ya mradi mkubwa wa kuunganisha umeme katika  nchi za Afrika Mashariki kutokea Ethiopia na Kenya ambao unaunganishwa na Kituo cha Lemugur-Arusha na  Isinya  upande wa Kenya.

Alisema mradi huo ni sehemu ya mradi wa pili mkubwa wa Msongo wa Umeme wa Kilovoti 400 wenye kilomita 670 kutoka Iringa hadi Shinyanga ambao unaunganishwa na  Singida -Arusha kuelekea Isanya nchini Kenya.

Alisema mradi wa Umeme wa Kenya na Tanzania ni wa  msongo wa Kilovoti 400 kwa kilomita 510 ambapo kilometa 414 ni upande wa Tanzania na  kilometa 96 kutoka  mpaka wa Tanzania na Kenya (Namanga) hadi Kituo cha Isinya nchini Kenya.

Amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kuunganika kikamilifu kwa njia ya nishati ya umeme na nchi za kaskazini kupitia mpaka wa Namanga kwenda Kenya na upande wa kusini kupitia mpaka wa Tunduma mkoani Songwe kwenda nchini Zambia.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Consortium Energoinvest unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu na kuinufaisha Tanzania, kwa kuwa miundombinu yake itatumiwa na miradi mingine mikubwa ukiwemo mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere ambapo msongo wa kilovoti 400 unawezesha kusafirisha umeme wa Megawati 2,000.

Katika ziara yake, Bw. Amosi Cheptoo, aliambatana na Mshauri Mwandamizi wa masuala ya kiuchumi wa AfDB, Bw. Jonathan Nzayikorera, Kaimu Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dkt. Jacob Oduorn na Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Dawati la Benki hiyo, Bw. Said Nyenge

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Amos Kipronoh Cheptoo (kushoto) anayesimamia nchi tisa za Afrika katika Benki hiyo, akipewa maelezo ya mradi wa umeme kati ya Tanzania na Kenya (KTPIP) na Mratibu wa mradi huo, Bw. Peter Kigadye, alipotembelea mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 528, jijini Arusha. Wa pili kushoto ni Kaimu Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dkt. Jacob Oduorn.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Amos Kipronoh Cheptoo (kushoto) anayesimamia nchi tisa za Afrika katika Benki hiyo, akitoa maelekezo kwa Meneja Mradi wa Umeme wa Tanzania na Kenya (KTPIP), Bw. Clive Sihwa, alipotembelea Kituo cha Umeme cha Lemugur ambacho ni sehemu ya mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 528.
Meneja Mradi wa Umeme wa Tanzania na Kenya (KTPIP), Bw. Clive Sihwa, akionesha eneo la Kituo cha Umeme cha Lemugur ambacho ni sehemu ya mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 528. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Amos Kipronoh Cheptoo (kushoto) anayesimamia nchi tisa za Afrika, Wa tatu kushoto ni Mratibu wa mradi huo, Bw. Peter Kigadye na wa tatu kulia ni Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Dawati la Benki hiyo, Bw. Said Nyenge.
Mratibu wa mradi wa Mradi wa Umeme wa Tanzania na Kenya (KTPIP), Bw. Peter Kigadye, akifafanua kuhusu michoro ya mradi huo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo, anayesimamia nchi tisa za Afrika katika Benki hiyo (hayupo pichani), alipotembelea Kituo cha Umeme cha Lemugur, jijini Arusha.

Muonekano wa miundombinu ya umeme katika Kituo cha Umeme cha Lemugur, kilichopo jijini Arusha, ambacho ni sehemu ya Mradi wa Umeme wa Tanzania na Kenya (KTPIP) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 528.

Muonekano wa Jengo litakalofungwa mitambo ya kuzalisha Umeme katika Kituo cha Umeme cha Lemugur kilichopo jijini Arusha, ambacho ni sehemu ya mradi wa Umeme wa Tanzania na Kenya (KTPIP) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 528.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Arusha)

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"