Wednesday, August 4, 2021

WAZIRI JENISTA MHAGAMA AWAONYA WANAOTAPELI WASTAAFU WATARAJIWA WA PSSSF, AAGIZA VYOMBO VYA DOLA VIWASHUGHULIKIE

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, amewaonya wale wote waliojiandaa kuwatapeli Watumishi wa Umma wanaotarajiwa kustaafu utumishi wa Umma kuacha mipango hiyo kwani vyombo vya dola vitawashughulikia kwa mujibu wa sharia za nchi.

Waziri Mhagama aliyasema hayo leo Agosti 4, 2021, wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wastaafu watarajiwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022, iliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la Golden Jubilee Towers jijini Dar es Salaam.

“ Baada ya kuanza utaratibu huu wa mafunzo, Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia ya kulinda wastaafu, jambo hili la kuwatapeli wastaafu tunataka kulikomesha mara moja na tunaomba vyombo vinavyohusika na vile ambavyo vipo hapa leo ninapofunga mafunzo haya na wao waanze mkakati wa kubaini matapeli wote ndani ya serikali na nje ya serikali wanaojihusisha kuangamiza maisha ya wastaafu wetu.” Alisisitiza.

Aliwaasa wastaafu hao watarajiwa kuwa makini kwa kufuata vyanzo sahihi vya utoaji taarifa za Mfuko ili kujiepusha na taarifa za watu wenye nia mbaya.

“Ilikuwa ni kiu yangu mstaafu ajue taarifa zake zote kama ziko sahihi, Mfumo tunaokwenda kuuzindua leo unakuwezesha mwanachama na msfaatu mtarajiwa kufungua simu yako na kuangalia michango yako yote iko sahihi? Kuna michango haijapelekwa? Kuna michango imepelekwa pungufu?...”Alisema

Alisema Mfumo huo utawawezesha wastaafu watarajiwa kuweka mambo sawa kabla haijafikia siku ya mwisho ya utumishi wa Umma.

“Ninawaomba sana mtumie Mfumo huu walau kila baada ya miezi mitatu angalia taarifa zako ili kuhakikisha ni sahihi.” Alibainisha.

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo, Mhe. Mhagama alisema mafunzo hayo yanalenga kuwaelimisha namna bora na sahihi ya kutumia fedha wanazolipwa baada ya kustaafu.

“PSSSF ilipokea maagizo kutoka serikalini na hasa ile dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuona ni namna gani wastaafu wanashirikishwa kupata uelewa wa maisha baada ya kustaafu nawapongeza Mfuko kwa kutimiza agizo hilo.” Alisema.

…..Ndio maana mafunzo haya tumeona yaendeshwe nchi nzima ili wastaafu wetu watarajiwa waliobakiza miaka mitano, mitatu, miwili, mmoja na hata kama wamebakiza miezi mitatu, wajue ni namna gani wanaweza kufanya matumizi sahihi ya fedha watakazozipata kama malipo yao ya pensheni baada ya kustaafu.” Alibainisha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba alisema jumla ya wastaafu watarajiwa wanaofikia 600 wameshiriki katika mafunzo hayo na kwamba wanahitimisha awamu ya kwanza ya mafunzo hayo mahsusi kwa wanachama wanaokaribia kustaafu.

Alisema semina hizo zimeshafanyika kwenye mikoa mbalimbali zikianza Julai 14, 2021 jijini Dodoma, na kuendelea kwenye mikoa ya Mwanza, Mbeya, Tanga, Arusha, Ruvuma, Mtwara, Morogoro na Zanzibar ambapo hadi sasa washiriki 3,000 wamehudhuria mafunzo hayo.

Alisema Mfuko umetimiza miaka mitatu tangu uanzishwe baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya PSPF, PPF, LAPF NA GEPF na kuzaliwa , Mfuko mpya ulirithi madai mengi ya mafao kutoka katika mifuko iliyounganishwa, madai yote yalilipwa na Mfuko unaendelea kulipa mafao mbalimbali ya wanachama yale ya kawaida.

Kuhusu mafunzo hayo CPA Kashimba alisema Mfuko pamoja na majukumu mengine ya msingi una jukumu kubwa la kuhakikisha unawashauri vema wanachama katika matumizi sahihi ya fedha za mafao wanazopata baada ya kustaafu.

“Hatuishii kuwalipa tu mafao na kuwaacha waende tu bila dira ya namna gani wanatumia mafao yao kwa ufanisi,” alisema na kuongeza……. hivyo semina hizi zinajumuisha kutoa elimu kwa wastaafu watarajiwa kwenye maeneo ya msingi kama vile wanachama na michasngo, mafao na mambo mengine ya kuzingatiwa tukiwa katika ajira wakati wa kustaafu na baada ya kustaafu.”Alifafanua.

Alisema katika kufanikisha mafunzo hayo Mfuko umeshirikiana na taasisi mbalimbali za fedha ambazo zinatoa elimu juu ya uwekezaji na matumizi sahihi ya fedha.

Akieleza zaidi kuhusu uhai wa Mfuko tangu uanzishwa miaka mitatu iliyopita, CPA Kashimba alisema hadi kufikia Juni 2021, Mfuko ulikuwa na wanachama 705,484 ambao ni watumishi wa umma na wafanyakazi wa makampuni ambayo serikali inamiliki hisa zaidi ya asilimia 30% na kwa kipindi hicho mfuko ulikuwa unahudumia wastaafu na wategemezi 188,330.

“Katika kipindi cha uhai wa Mfuko miaka mitatu tangu uanzishwe, Mfuko umelipa wanufaika 143,367, jumla ya shilingi Trilioni 5 na kiasi hiki cha fedha kikitumika vizuri na wanufaika  kinaweza kikatoa mchango mkubwa katika kuendeleza miradi mbalimbali, kutengeneza ajira kwa vijana, kuongeza pato la mstaafu na hatimaye pato la taifa.” Alibainisha CPA Kashimba.

Kwa mwezi Julai 2021, umelipa pensheni ya mwezi kw awanufaika 145,417 ya thamani ya shilingi bilioni 56.

“Tumeona haja ya kuandaa mpango wa mafunzo maalum kwa ajili ya wanachama wanaotarajia kustaafu Mafunzo haya yatalenga katika maeneo ya uwekezaji katika viwanda vidogovidogo, uwekezaji katuika masoko ya fedha.” Alisema

Akizungumza kwa niaba ya wastaafu watarajiwa,  Mwalimu Hussein Masoud aliushukuru Mfuko kwa kuandaa mafunzo hayo kwani fedha wanazotarajiwa kupokea zinahitaji maelekezo ya jinsi gani wanaweza kuhifadhi na kutumia fedha hizo vizuri.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akitoa hotuba yake kwenye semina hiyo ya mafunzo Agosti 4, 2021.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Grayson Henry Mwaigombe akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, CPA Hosea Kashimba akitoa hotuba yake ya utangulizi.
Mkurugenzi wa Uendeshaji, PSSSF, Mbaruku Magawa, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba (kushoto), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji benki ya Azania, Bw. Charles Itembe wakiwa kwenye hafla hiyo.




Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Benki ya Mwalimu Bw. Ombeni Kaale akitoa mada kwenye mafunzo hayo kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye benki hiyo.
Sehemu ya washiriki.
Sehemu ya washiriki.
Washiriki wakijisajili
Washiriki wakijisajili
Waziri Mhagama akitoa hotuba yake.
Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA, PSSSF, Bw. Gilbert Chawe (katikati) akiwa na timu yake ya TEHAMA
Mwalimu Hussein Masoud, akizungumza kwa niaba ya wastaafu watarajiwa.
Mkurugenzi wa TEHAMA, PSSSF, Bw. Gilbert Chawe, akitambulisha Mfumo wa "PSSSF KIGANJANI" ambao ulizinduliwa na Waziri Mhe. Jenista Mhagama.
Mhe. Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa PSSSF
Waziri Mhagama akiondoka baada ya kufungua mafunzo hayo.

0 comments:

Post a Comment