WACHIMBAJI WADOGO KUPOKEA KIFUTA JASHO CHA MILIONI 90 -SINGIDA
Na Steven Nyamiti – Mkalama Singida
Jumla ya
Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu 90 katika eneo la kijiji cha Tumuli wataanza
kupokea kifuta jasho kuanzia tarehe 2
Agosti, 2021 baada ya utaratibu wa kupewa kifuta jasho kukamilika.
Hayo yameelezwa
na Waziri wa Madini Doto Biteko tarehe 31 Julai, 2021 katika kijiji cha Tumuli
wilaya ya Mkalama Mkoani Singida wakati wa ziara ya kukagua na kutembelea
shughuli za wachimbaji wadogo.
Ameeleza kuwa,
wachimbaji watakaopokea kifuta jasho hicho ni wale walioandikishwa na ambao
taarifa zao zipo kwenye Kanzidata kufuatia kuondolewa kuchimba kwenye eneo
lenye leseni.
“Mgogoro huu una
historia ndefu sana zaidi ya miaka 9, mwanzo walikua wachimbaji 26 wanaopaswa
kupewa lakini sasa wameongezeka zaidi ya
100, lazima tutende haki kwa watu wote kuanzia mchimbaji hadi mwekezaji ili pande zote ziridhike,”
amesema Biteko.
Aidha, Waziri
Biteko ameagiza mgodi wa Chama cha Ushirika cha Uchimbaji Madini (Sekenke One
Mining Cooperative Society) uliosimamishwa mwezi Disemba 2019, kutokana na zuio
la kiusalama katika mgodi huo ufunguliwe mara moja ili shughuli za uchimbaji ziendelee.
Biteko
amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Singida, Chone Lugangizya kuzungumza na
kampuni ya Sekenke One ili wakubaliane
waendelee kuchimba dhahabu kwa kuzingatia Sheria na Taratibu.
“Mimi
ninachotaka kuona shughuli zinaendelea, utaratibu wa kufunga funga migodi huu
huwa hautusaidii sana, tunaopoteza ni sisi, tunachotaka kuona wachimbaji
wanarudi kwenye uchimbaji ili masoko haya yaweze kupanuka Zaidi,” amesisitiza
Biteko.
Kuhusu utatuzi
wa mgogoro baina ya Nabii Elia Makuli na kikundi cha Bathlomew Waziri Biteko
amerejesha suala hilo kwenye ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa ajili ya kulitatua ambapo
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda amehaidi kufanyia kazi mgogoro huo
kuanzia siku ya Jumatatu tarehe 2 Agosti.
Naye, Mkuu wa
wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amethibitisha kuwa wilaya yake imepokea fedha
hizo kutoka kampuni ya uchimbaji madini ya PuBo (PuBo Mining Limited) kiasi cha
Shilingi Milioni 90 ambazo zimekabidhiwa kwenye ofisi ya TAKUKURU ili kifuta
jambo hicho wapatiwe wananchi 90 waliopo kwenye kanzidata ambao watapokea kiasi
cha Shilingi Milioni moja kila mmoja.
Kizigo ametoa
onyo kwa wachimbaji wanaotaka kufanya udanganyifu ili kuongezea majina zaidi ya
yale yanayotambulika.
"Wapo
wananchi wananipigia simu wakitaja kuwa wao ni sehemu ya kupata kifuta jasho
hicho, majina yao hayapo kati ya majina 90 ambayo tumeyapokea kutoka ofisi ya
madini, nasisitiza tutafuata kanzidata ya Wizara ya Madini kama Waziri alivyoelekeza,"
amesema Kizigo.
Waziri Biteko amehitimisha ziara ya siku mbili Mkoani ambapo ametembelea wachimbaji wadogo na kukagua Mgodi wa Kati wa Shanta, kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo pamoja na kutoa elimu ya Sheria ya madini kwa wadau waliojitokeza. Katika ziara hiyo pia aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahembe na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Vijiji na Halmashauri
Comments
Post a Comment