Naibu Waziri Gekul amuibua Mbaraka Mwinshekhe mahafali ya Malya

 Adeladius Makwega -Kwimba Mwanza (WHUSM)

Serikali imesema kuwa Watanzania wanahitaji burudani ya muziki  kwani  mara baada ya kujishughulisha  na  shughuli  za maendeleo mchana kutwa  basi jioni ni muda wa kupumzisha miili na akili zao.

Hayo yamesemwa Julai 17, 2021 katika mahafali ya 10 ya  Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ambapo Mheshimiwa Pauline Gekul Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amekuwa mgeni rasmi.

“Watanzania tunapenda muziki iwe dansi, Bongo fleva, rege  au  muziki wa kiutamadauni, si mmeona wanachuo cha Malya  walivyokuwa wakicheza muziki  vizuri, huku wakinengua?  huo ndiyo muziki” alisema  Mheshimiwa Gekul.

Yawe mashairi au ala za muziki zinaweza kumtoa nyoka pangoni alisema kwa  bashasha huku akiiweka vizuri mikrofoni wakati wa mahafali hayo.

Tanzania yetu ina utajiri mkubwa wa muziki mathalani   nyimbo za  zamani zimekuwa  zikipigwa katika  baadhi ya redio na kumbi za starehe. Serikali chini ya Jemedari, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inatoa ushirikiano wa kutosha kwa wanamuziki wa Tanzania.

Pia aliikumbusha hadhira wakati wa mahafali hiyo kuwa muziki wa Kitanzania unamchango katika kukikuza Kiswahili, tunawapenda wanamuziki wetu na ndiyo maana  Serikali katika Bajeti ya sasa 2021/2022 imeweka bilioni 1.5 katika kukuza Sanaa nchini.

Akiunga mkono kauli hiyo ya Serikali Samsoni Mhando ambaye ni mdau wa  muziki hasa wa zamani nchini amesema kuwa  ni kweli  muziki wa Tanzania unapendwa sana na umekikuza mno kiswahili  lakini zipo changamoto  za hapa na pale.

Mdau huyu ambaye alikuja kwenye mahafali ya  mtoto wake aliyehitimu mafunzo hayo Stashahada ya Michezo

anaamini kuwa Serikali imeshaanza kuzitatua changamoto zote za muziki ikiwamo suala la mirabaha ambalo ni mwazo mwema.

“Mimi nampenda sana Mbaraka Mwinshekhe na nazipenda mno nyimbo zake, hakuna siku inayonipita bila ya kusikiliza wimbo wa Mbaraka kwani ndani yake nimekuwa nikipata elimu na burudani” anasema ndugu Mhando.

Mdau huyo wa muziki anakubaliana na kauli ya Serikaili juu ya upenzi wa  Watanzania katika  muziki  na ndiyo maana baadhi ya wanamuziki wa zamani wamefariki lakini nyimbo zao  bado zinaishi na zinapendwa.

Akitaja baadhi ya wanamuziki waliofariki; Mbaraka Mwinshekhe (Mtaa wa Saba), Marijani Rajabu (Mayasa), Salim Abdalla (Mkono wa idd), Moshi William (Ndoa ndoano), Muhidini Ngurumo (ikiwa kam haunitaki), Shabani Dede (Fatuma), Shem Kalenga (dada Asha) na wengine wengi wanaendelea kukonga nyoyo za Watanzania.

“Kilichokuzuzua ni nini, 

mwenyewe ukanirudia tena,

Je umepambana na nini dada huko ulipokwenda, Maisha uliyopata kwangu dada oh oh , Hautapata kwa mwingine dada oh oh, Kaa sasa utilie ewe dada oh oh.”

Mdau huyu alidokeza kwa kuimba sehemu ya wimbo huo alinainisha kuwa unafahamika kama "Kilichokuzuzua ni nini?" kutoka kwa bendi ya Morogoro Jazz iliyoongozwa  na Mbaraka Mwinshehe .








Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"