MAONESHO YA 45 YA BIASHARA YA KIMATAIFA YA DAR ES SALAAM YAANZA, MAKAMPUNI 3,200 KUSHIRIKI

NA K-VIS BLOG

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo amesema jumla ya makampuni 3,200 kutoka ndani na nje ya nchi yamethibitisha kushiriki maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyoanza leo Juni 28, 2021 kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa TanTrade ulioko ndani ya viwanja hivyo Mhe. Waziri alisema,maonesho hayo yatadumu kwa muda wa siku 16 na yamebeba  kauli mbiu isemayo “ Uchumi wa Viwanda Kwa Ajira na Biashara Endelevu”.

“Kuna makampuni 76 kutoka nchi 7 za kigeni na kuna taasisi binafsi na za umma yakiwemo makampuni ya watu binafsi kutoka hapa nchini yatashiriki.” Alisema Profesa Mkumbo na kuongeza……. “Maonesho yameanza leo Juni 28, 2021 kama mnavyoona na ufunguzi rasmi utafanyika Julai 5, 2021 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.” Alisema

Alisema kuhusu masuala ya udhibiti wa maradhi ya Covid19 katika kipindi cha maonesho hayo  Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Kushirikiana na Wizara ya Afya zimechukua hatua mbalimbali za tahadhari dhidi ya ugonjwa huo .

“Kama mnavyofahamu Dunia na Tnazania tunapambana na Covid kwa hiyo tunataka tuzingatie miongozo ya Shirika la Afya Duniani ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afya ambayo imetoa muongozo wa kudhibiti maradhi hayo.” Alisema na kuongeza.

Katika sehemu za kuingilia yametengwa maeneo yatakayokuwa na maji tiririka ya kunawa mikono na milango ya kutosha ya kuingilia na kutoka, kuweka utaratibu wa kuweka matangazo ya mara kwa mara kuwakumbusha watu watakaokuwa kwenye eneo la maonesho. 


“Tumezungumza na MSD wataweka barakoa za kutosha nje ya viwanja ili wananchi watakaokuja bila barakoa basi waweze kununua kwa bei rahisi nje ya uwanja ili mtu akiingia basi awe amevaa barakoa.” Alibainisha Profesa Mkumbo.

--

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"