DKT.KIJAZI AWATAKA WATUMISHI KUFANYA MAZOEZI

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akimvisha medali Afisa Rasilimaliwatu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Stella Msuya ikiwa ni moja ya pongezi ya kushiriki bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo.

Washiriki wa mchezo wa mbio za magunia wakichuana wakati wa bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo.
Na Happiness Shayo –Dodoma
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi amewataka watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujenga mshikamano na upendo katika maeneo yao ya kazi.
Dkt. Kijazi ametoa wito huo wakati wa bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika leo katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mazoezi iwe ni sehemu ya maisha yetu na pia iwe ni sehemu ya kazi zetu amesisitiza Dkt. Kijazi.
Ameongeza kuwa, Wizara yake itajipanga kuhakikisha kila mtumishi anashiriki katika kufanya mazoezi na pia kila mtumishi anashiriki kwenye mabonanza na amewataka watumishi kuendelea kuhamasishana ili ushiriki uzidi kuongezeka katika matamasha yanayokuja.
Dkt. Kijazi amefafanua kuwa Wizara itaweka utaratibu wa kuwatambua washiriki bora wa kila mwaka wanaofanya mazoezi na wanaoshiriki kikamilifu katika matamasha kama hayo na kuwapa zawadi maalumu. 
Pia, amesema kuwa, Wizara itahakikisha ushiriki wa watumishi katika matamasha hayo hauishii Dodoma bali utaendelea kwenye matamasha mengine yanayofanyika nchini, kama Kilimanjaro Marathon, Ngorongoro Marathon na Serengeti Marathon.
 Watumishi watakaofanya vizuri tutawadhamini ili waiwakilishe Wizara kwenye Marathon hizo.
Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Kijazi amewapongeza washiriki wote walioweza kukimbia mbio za kilomita tano kwa kupata medali na kuwataka ambao wameshindwa wajitahidi kipindi kijacho wamalize mbio hizo.
Ni imani yangu kuwa bonanza linalokuja wote tutamaliza mbio za kilomita tano, cha msingi tuendelee kufanya mazoezi ,tusisubiri hadi matamasha haya yafike ndo tufanye mazoezi Dkt. Kijazi amesema.
Dkt. Kijazi amewashukuru Dodoma Fitness Club na Muungano Fitness Club kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kufanikisha bonanza hilo  na kusema kuwa uwepo wao ni chachu kwa Wizara katika  kuimarisha mabonanza.
Naye, Mwenyekiti wa Jogging Clubs Dodoma, Bw.Mugisha Mujungu ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara kila itakapohitaji ushirikiano katika kufanya mazoezi na kuwataka watumishi wa serikali kujiunga na Jogging Clubs ili kuimarisha afya zao.
Bonanza hilo limehudhuriwa na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na washiriki kutoka Dodoma Fitness Club na Muungano Fitness Club za Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi  akiteta jambo na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bw. Lucius Mwenda (kulia) wakati wa bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika leo katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza na washiriki wa bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika leo katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bw. Lucius Mwenda na Mwenyekiti wa Jogging Clubs Dodoma Bw.Mugisha Mujungu.
Washiriki wa mchezo wa kuvuta kamba kutoka Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, wakishindana na Idara ya Utawala Wizara ya Maliasili na Utalii (hawapo pichani) katika bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lililofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo.
Washiriki wa bonanza la watumishi lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii wakifanya mazoezi ya viungo katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo.


 

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"