SERIKALI YAGAWA INJINI ZA BOTI KWA VYAMA VYA WAVUVI KANDA YA ZIWA VICTORIA
Na
Mbaraka Kambona, Kagera
Katika
kuhakikisha shughuli za Wavuvi zinaboreshwa ili kukuza kipato chao, Serikali
imegawa Injini za Boti nne (4) aina ya Yamaha zenye thamani ya shilingi milioni
35 kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi vinne vinavyofanya shughuli zao katika Ukanda
wa Ziwa Victoria.
Wakati
akikabidhi Injini hizo kwa Wavuvi Wilayani Muleba Mkoani Kagera jana, Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa ugawaji wa Injini hizo
ni katika kutekeleza moja ya majukumu ya
Wizara ya kuhakikisha wanawezesha upatikanaji wa utaalamu, rasilimali fedha na
vitendea kazi ili kuwasaidia Wavuvi kuboresha kazi zao na kuendeleza sekta ya
uvuvi kwa ujumla.
Dkt.
Tamatamah alisema kuwa katika kuhakikisha Vyama vya Wavuvi vinawezeshwa, mwaka wa fedha 2020/ 2021 Wizara ya Mifugo na
Uvuvi imetenga shilingi milioni mia mbili (200,000,000) kwa ajili ya
kuviwezesha vyama vya Ushirika vya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji.
“Rai
yangu kwa Vyama hivi vya Ushirika wazitumie injini hizi kwa kufanya uvuvi
endelevu na kuachana na uvuvi haramu”, alisema Dkt. Tamatamah
“Nawahamasisha
pia wavuvi wajiunge katika vikundi vya ushirika ili iwe rahisi kuwezeshwa kwa
mikopo na vitendea kazi ili waweze kujikwamua kiuchumi”,aliongeza Dkt.
Tamatamah
Kuhusu
muitikio wa Wavuvi kujiunga na Vyama vya ushirika, Dkt. Tamatamah alisema kuwa
muitikio ni mzuri na Wilaya ya Muleba imekuwa kinara wa kuanzisha vyama hivyo.
Akiongea
baada ya kupokea Injini ya Boti, Mwakilishi wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi,
Izigo, Wilayani Muleba, Naziru Kassanga alisema kuwa Injini hiyo ya Boti waliyopatiwa itawasaidia
sana wao kama wavuvi wadogo wadogo kufanya uvuvi wa kisasa utakaowasaidia
kuboresha maisha yao.
“Injini
hii itatusaidia sisi wavuvi wadogo kwenda kuvua katika kina kirefu kwa urahisi
na kuondokana na uvuvi wa kienyeji ambao tija yake ni ndogo”, alisema Kassanga
Naye,
kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi cha Zilagula,Wilayani
Buchosa, Agnes Mbasha aliishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwakabidhi boti ambayo anasema itawasaidia
kufanya doria ya kulinda nyavu zao dhidi ya wezi.
“Nitumie
nafasi hii pia kuwahamasisha wanawake wenzangu kujiunga na Vyama hivi vya
Ushirika kwani vinasaidia sana kujikwamua kimaisha”,alisema Mbasha
Kuhusu Vyama vya Ushirika kuunganishwa na taasisi za
fedha, Dkt. Tamatamah alisema mikopo iliyoombwa na kupitishwa kwa ajili ya
vyama vya ushirika ni shilingi bilioni 2.6 na ambayo tayari imeshatolewa ni
shilingi milioni 873.8 na vyama 14 viko katika hatua za mwisho kupatiwa mikopo.
“Wizara
imeihamasisha Benki ya Posta Tanzania (TPB) kuzindua akaunti ya Wavuvi (Wavuvi
account) kwa ajili ya mikopo na bima mahususi kwa Wavuvi hususani wavuvi
wadogo”,alifafanua Dkt. Tamatamah
Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia)
akikabidhi Injini ya Boti kwa Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi,
Zilagula, Agness Mbasha katika hafla fupi ya kugawa Injini za Boti kwa Vyama
vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria iliyofanyika katika Wilaya
ya Muleba, Mkoani Kagera Oktoba 23,
2020.
Injini
za Boti (4) aina ya Yamaha ambazo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezikabidhi kwa
Vyama vinne vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria katika hafla fupi
iliyofanyika Wilayani Muleba, Mkoani Kagera Oktoba 23, 2020.
Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati
waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wawakilishi wa Vyama vya
Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria muda mfupi baada ya kukabidhi Injini
za Boti kwa Vyama (4) vya Ushirika wa Wavuvi Oktoba 23, 2020. Kutoka kulia
waliokaa ni Mkurugenzi Msaidizi, Kitengo cha Huduma za Ugani za Uvuvi, Anthony
Dadu na wapili kutoka kulia ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utafiti na Mafunzo
ya Uvuvi, Dkt. Erastus Mosha. Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi
Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Omary Mchengule na wapili kutoka kushoto
ni Kaimu Mwenyekiti, Chama cha Ushirika cha Wavuvi, Zilagula, Agness Mbasha.
Comments
Post a Comment