ZIMAMOTO YATOA TAMKO UUNGUAJI WA SHULE NCHINI
NA MWANDISHI WETU,
KAGERA
Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji nchini limewataka wamiliki wa shule nchini kuhakikisha wanafunga vifaa
maalumu vya awali vya kuzimia moto ili kuweza kudhibiti majanga pindi
yanapotokea na kupunguza athari za majanga hayo
Hayo yalisemwa na
Kaimu Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, DCF Charo Mangare
baada ya kutembelea Shule ya Msingi ya Byamungu Islamic iliyopo Kata ya Itera,
wilayani Kyerwa mkoa wa Kagera ambapo kulitokea ajali ya moto na kusababisha
vifo vya wanafunzi 10 na majeruhi sita.
“Pamoja na kuwaagiza
wamiliki wa shule kufunga vifaa maalumu vya kudhibiti moto pia nawaagiza
makamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini kukagua shule zote na zoezi
hilo liwe endelevu ili kuweza kudhibiti madhara ya ajali hizo pindi
zinapotokea” alisema DCF Mangare
Akizungumzia chanzo
cha ajali hiyo DCF Mangare alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama inaendelea na
uchunguzi na pindi utakapokamilika taarifa itatolewa kwa wananchi ili kuwepo
sasa mbinu za kudhibiti ajali kama hizo.
Akizungumza wakati wa
ziara hiyo Muuguzi Mkuu Msaidizi, Justine Katalaiya alisema majeruhi wanne kati
ya sita waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Karagwe wamehamishiwa
Hospitali ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Kaimu Kamishna wa
Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, DCF Charo Mangare akifanya ukaguzi
baada ya kuwasili eneo la tukio la ajali ya moto iliyosababisha vifo vya
wanafunzi 10 katika Shule ya Msingi ya Byamungu iliyoko Kata ya Itera,Wilayani
Karagwe mkoa wa Kagera. (Picha na Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji)
Comments
Post a Comment