WAKILI MKUU WA SERIKALI AWAPONGEZA WAFANYAKAZI KWA MAFANIKIO MAKUBWA YALIYOPATIKANA NDANI YA MUDA MFUPI
NA DENNIS BUYEKWA – MOROGORO
SERIKALI
ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inatambua na kuthamini
mchango mkubwa unaotolewa na watumishi wa Umma wakiwemo watumishi wa Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali katika kuiletea maendeleo nchi yetu.
Hayo
yamezungumzwa mapema leo na Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel Pascal Malata
wakati akifungua kikao cha tatu cha Baraza la wafanyakazi wa ofisi hiyo
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA)
uliopo mkoani Morogoro.
Bw.
Malata amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo mwaka 2018, ofisi yake
imeendelea kutekeleza vyema majukumu yake ya Uratibu, Usimamizi, Ushauri, na
Uendeshaji wa Mashauri yote ya Madai na Usuluhishi yanayofunguliwa dhidi ya
Serikali pamoja na Taasisi zake ndani na nje ya nchi.
Ameongeza
kuwa ili tuweze kufikia malengo ya vipaumbele vikubwa katika nchi yetu ambavyo
vimewezesha kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa kati, kuvutia wawekezaji
na ujenzi wa viwanda, ni muhimu kuwa na uwazi na ushirikishwaji baina ya
viongozi katika taasisi mbalimbali za umma pamoja na watendaji ambao ni
watumishi wa ngazi zote wanaozingatia sheria, taratibu, na miongozo mbalimbali
ya nchi.
“naomba nitoe wito kwa wajumbe na
washiriki wote wa Baraza hili kutumia fursa hii mliyoipata kuhoji na kutoa
mapendekezo chanya yatakayokuwa na msaada kwa taasisi yenu ili hatimaye mchango
wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali uonekane katika jitihada za pamoja za
kuiletea maendeleo nchi yetu”, alisema Bw.Malata
Akizungumza kuhusu mafanikio
yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo, Bw. Malata amesema kuwa ofisi yake
imefanikiwa kuokoa shilingi za kitanzania Trioni 11.4 baada ya kushinda mashuri
mbalimbali yaliyofunguliwa dhidi ya serikali kiasi ambacho kingelipwa kama
Serikali ingeshindwa katika mashauri hayo.
Ameongeza kuwa taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali CAG) kwa mwaka wa fedha
2018/2019 inaonyesha kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imepata hati safi
katika taarifa ya hesabu zake za fedha katika kipindi hicho ikiwa ni mwaka
mmoja tu tangu kuanzishwa kwake.
“Hati safi ya ukaguzi wa
taarifa ya fedha ni uthibitisho kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ina
udhibiti bora katika kusimamia rasilimali za serikali”, alisema Bw. Malata.
Aidha
kutokana na mafanikio ambayo nchi yetu imekuwa ikiyapata katika nyanja
mbalimbali ikiwemo nyanja ya kiuchumi, baadhi ya watu wasiotutakia mema
wamekuwa wakijaribu kufanya hujuma ili kuharibu na kuturudisha nyuma katika
jitihada zetu za kujiletea maendeleo aidha kwa maslahi yao binafsi au kwa
maslahi ya watu wanaowatuma.
Akielezea
kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya watu hao wenye nia mbaya, kwa mamlaka na
wajibu ilionao, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali daima imeiwakilisha Serikali
vyema katika Mahakama mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kudai na kutetea
haki hatua iliyopelekea kuokoa mali za serikali ambazo zingepotelea mikoni mwa
watu hao wenye nia ovu.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pia imefanikiwa kuboresha maktaba yake kwa
kununua vitabu vya sheria, nakala za
sheria na machapisho mbalimbali hatua ambayo imesaidia kuwaongezea ujuzi
watumishi wake hasa wanasheria hatua ambayo imeisaidia serikali kushinda
mashauri mengi yanayofunguliwa dhidi yake.
Kuhusu uboreshwaji wa miundombinu ya ofisi wakili Mkuu wa Serikali amesema kuwa ofisi yake imefanikiwa kuweka mifumo ya kielektroniki ya kusajili, kuendesha, kusambaza na kusimamia mashauri kwa mawakili na watumishi mbalimbali, ikiwemo mfumo wa uendeshaji wa mashauri ndani na nje kwa njia ya kielekroniki (Video Conference) hatua iliyosaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri kwani mawakili hawalazimiki kusafiri kwenda katika mikoa mbalimbali kuendesha mashauri badala yake wamekuwa wakisimamia mashauri hayo wakiwa ofisini hapo.
Bw.
Malata amewapongeza wajumbe wa Sekretariat kwa
maandalizi mazuri waliyofanya
katika kuhakikisha kikao hicho
kinafanyika huku akiwakumbusha wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali, kujadili masuala yote yatakayoletwa mbele yenu kwa
weledi, hekima na busara ili Baraza hili liwe na tija ofisi na taifa kwa
ujumla. Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
kimefanyika baada ya mafunzo ya siku moja kuhusu umuhimu wa vyama vya
wafanyakazi na wajibu wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi.
Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel
Malata akisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na
Wajumbe waliohudhuria kikao hicho mapema leo mkoani Morogoro.
Baadhi ya Wajumbe waliohudhuria kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao hicho.
Comments
Post a Comment