Thursday, October 1, 2020

WAFUGAJI NCHINI WATAKIWA KUACHA UFUGAJI WA MAZOEA

 

Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tz Bwana Imani Sichalwe (aliyevaa koti jeupe) akiwa na wawikilishi wa wafugaji kutoka mikoa mbalimbali waliopatiwa Mafunzo ya ufugaji wa kisasa yaliyofanyika Kwenye ofisi za Uwakala wa Vyuo vya mafunzo ya Mifugo kampasi ya Tengeru Jijini Arusha.
Na.Vero Ignatus,Arusha

Wafugaji Nchini wametakiwa kuacha Ufugaji wa mazoea na kugeukia Ufugaji wa Kisasa Katika Kipindi hiki cha  ongezeko la Uanzishwaji wa Viwanda vingi vya Nyama Nchini.

Akizungumzia wakati wa kufunga mafunzo ya ufugaji wa Kisasa yaliyotolewa kwa Wafugaji wa Mikoa ya Arusha,Dar es salaam,na Manyara yaliyofanyika Kwenye ofisi za Wakala wa vyuo vya mafunzo ya mifugo kampasi ya Tengeru Mkoani Arusha, Kaimu Msajili bodi ya Nyama Tanzania  Imani Sichalwe  amesema mafunzo hayo ni ngao Muhimu sana kwa wafugaji kwakuwa yanamsaidia Kuongeza fursa za biashara ya mifugo jambo litakalosaidia kuongeza thamani ya nyama ndani na nje ya nchi.

Kwa Upande wake James Taki akiwa ni Mfugaji kutoka wilaya ya ngorongoro amesema amefurahishwa na mafunzo ya ufugaji wa kisasa yaliyotolewa na wizara ya mifugo na kuomba yawe endelevu ili  kuwasaidia wafugaji nchini kufuga kisasa ikiwemo kupewa elimu juu ya umuhimu wa kutenga nyanda za malisho na elimu ya Unenepeshaji mifugo jambo litakalo wasaidia kuuza mifugo yao kwenye masoko ya Mifugo yaliyopo.

Aidha akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake kutoka wilaya ya Meru Bi Mary Tairi amesema Mafunzo hayo yamemuwezesha kufahamu namna bora ya kuboresha uzalishaji wa mifugo kutoka Kwenye kufuga kimazoea na kugeukia ufugaji wa kisasa na kuahidi elimu aliyoipata kwenda kuwasaidia wafugaji wenzake.

Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bwana Imani Sichalwe ,amehitimisha  kwa kusema kuwa Mafunzo haya  ya ufugaji wa Mifugo kisasa yanamsaidia moja kwa moja Mfugaji ,kutambua fursa zilizopo jambo litakalosaidia Mfugaji kunufaika na Mifugo yake hasa kipindi hiki cha mageuzi makubwa ya Viwanda na Tanzania tukiwa Kwenye Uchumi wa Kati wa Viwanda Pamoja na uwepo wa ongezeko kubwa la uanzishwaji wa Viwanda vya Nyama nchini.

0 comments:

Post a Comment