TANZANIA YAPOKEA SH. BILIONI 34 KUTOKA KUWAIT KUTEKELEZA MRADI WA UMWAGILIAJI LUICHE KIGOMA
NA PETER HAULE NA
JOSEPHINE MAJURA, WFM, DODOMA
SERIKALI ya Tanzania imepokea mkopo wa
masharti nafuu wa Dinar milioni 4.5 sawa na Shilingi bilioni 33.9 kutoka Mfuko
wa Maendeleo wa Kuwait (KFED), kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Umwagiliaji
katika Bonde la Mto Luiche mkoani Kigoma.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya fedha na Mipango, Bw. Benny
Mwaipaja.
Bw. Mwaipaja alisema kuwa Mkataba huo
umesainiwa nchini Kuwait kati ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Bi. Aisha
Amour, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi Mkuu wa KFED, Abdulwahad
Ahmed Al- Bader, kwa niaba ya Serikali ya Kuwait.
“Fedha hizo za mkopo zitatumika katika
uhakiki wa usanifu wa kina wa mradi na usimamizi wa ujenzi wa bwawa la maji la
mita 375 lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 70 za maji”, alisema
Bw. Mwaipaja.
Alisema kuwa fedha hizo pia zitatumika
katika ujenzi wa miundombinu kama mifereji ya maji, kinga za mafuriko, daraja
na barabara zitakazotumika kutoa huduma zenye urefu wa kilometa 21.
Bw. Mwaipaja alisema kuwa mradi huo
unategemewa katika kuongeza wigo wa kilimo cha umwagiliaji kwa takribani eneo
la hekta 3,000 na kutoa fursa za ajira mbalimbali kabla na baada ya kuanza
kutekelezwa kwa mradi.
Zao ambalo linatarajiwa kuzalishwa
katika eneo la mradi ni Mpunga, zao hilo linatarajiwa kuongeza kipato cha
wakulima lakini pia kutekelezwa kwa dhana ya Serikali ya kuwa na kilimo cha
kisasa kitakachoongeza usalama wa chakula nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara
ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, akitoa taarifa ya mkopo wa
masharti nafuu wa Dinar milioni 4.5 sawa na Shilingi bilioni 33.9 kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait
(KFED), kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Umwagiliaji katika Bonde la Mto
Luiche mkoani Kigoma, mkoani Dodoma
Comments
Post a Comment