JKCI YAFANYA UPASUAJI WA AXILLOBIFEMORAL BYPASS GRAFT SURGERY KWA MARA YA KWANZA
NA MWANDISHI MAALUM – DAR ES SALAAM
MADAKTARI bingwa wa upasuaji wa
moyo, mishipa ya damu na kifua wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kutoka kwenye
mshipa wa damu wa kifuani na kupeleka kwenye mishipa ya damu ya miguuni
(Axillobifemoral Bypass Graft Surgery).
Upasuaji huo ni wa kwanza
kufanyika hapa nchini ambapo mgonjwa alikuwa na tatizo la kupata maumivu makali
maeneo ya miguuni, mapaja na sehemu ya kukalia kwa muda wa miezi nane baada ya
uchunguzi ikagundulika mshipa wake mkubwa wa damu (Abdominal Aorta) umeziba
kabisa na hivyo kushindwa kupeleka damu kwenye miguu (Aortoilliac
Occlusion Disease) damu ilikuwa inapelekwa kupitia mishipa midogo
(Collaterals).
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi jana jijini Dar es Salaam daktari bingwa wa upasuaji wa moyo,
mishipa ya damu na kifua wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph
alisema walimpokea mgonjwa huyo wiki iliyopita kutoka Hospitali ya Mnazi mmoja
iliyopo Visiwani Zanzibar.
Dr. Alex alisema upasuaji
wa aina hiyo haujawahi kuufanya hivyo basi baada ya majadiliano ya jopo la
madaktari bingwa na kushauriana na mgonjwa waliona waufanye kwani kulikuwa na
uwezekano mkubwa kwa mgonjwa kupona na kutoka katika maumivu makali aliyokuwa
nayo.
“Upasuaji tulioufanya ni wa
kupandikiza mrija bandia wa damu na kuukwepesha eneo
ambalo limeziba. Tuliweka mrija kama mshipa bandia wa
damu kutoka kwenye mshipa wa damu wa kifua upande wa kushoto na kuupitisha
pembeni ya kifua na tumbo mpaka kwenye mguu wa kushoto na kisha kuelekea
mguu wa kulia”,.
“Baada ya kufanya upasuaji
huo hivi sasa miguu yote miwili inapata damu ambayo inatoka moja kwa
moja kwenye mshipa wa damu wa kifuani kwani tuliikwepesha eneo
la tumboni ambalo mshipa umeziba”, alisema Dkt. Alex.
Dkt. Alex alisema hii ni faraja
kwao kwani hivi sasa huduma za matibabu ya magonjwa kama hayo pamoja na mengine
ya matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu zinapatikana hapa nchini na hakuna
haja ya kusafiri kwenda kutibiwa nje ya nchi ambako gharama ni kubwa kati
ya milioni 15 hadi 20 wakati hapa nchini huduma inapatikana kwa
gharama naafuu.
Kwa upande wake Mama Fatma
Khamis ambaye alifanyiwa upasuaji huo alisema kwa muda wa miezi nane iliyopita
miguu ilikuwa inamuuma baadaye akapata kidonda ambacho hakikupona hata baada ya
kwenda Hospitali. Baadaye akaenda kwa daktari wa mifupa katika
Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar ambapo baada ya kufanyiwa vipimo akaambiwa
anatatizo la damu kuganda na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) iliyopo Dar es Salaam kwani hospitali hiyo
haikuwa na uwezo wa kumtibu.
“Baada ya kufika JKCI
nilifanyiwa vipimo na kuambiwa mshipa mkubwa wa damu
haupitishi damu katika miguu na hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji wa
kupandikiza mishipa ya damu niliambiwa katika upasuaji huo naweza kupona au la
na hivyo kupewa fomu za kusaini nikasaini.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji
niko vizuri kama unavyoniona naweza kusimama na kutembea vizuri
maumivu ya miguu yamepungua tofauti na nilivyokuwa mwanzo”, alisema
Mama Fatma.
Aliwashauri watanzania wenye
matatizo kama hayo wasipate tabu na wasihangaike kwenda kutibiwa nje ya nchi
kwani hapa nyumbani ambapo ni karibu huduma hiyo inapatikana.
“Ninaishukuru sana Serikali
yangu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kunilipia gharama za matibabu
haya na sasa hivi nimefanikiwa niko vizuri”, alishukuru Mama Fatma.
Wataalamu
wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika
picha ya pamoja na Mama Fatma Khamis mkazi wa Zanzibar ambaye alifanyiwa
upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kutoka kwenye mshipa wa damu wa kifuani
na kupeleka kwenye mishipa ya damu ya miguuni (Axillobifemoral Bypass
Graft Surgery). Upasuaji huo ni wa
kwanza kufanyika hapa nchini. (Picha na JKCI)
Comments
Post a Comment