WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, Taasisi, Mashirika yote ya Serikali na Sekta Binafsi pamoja na vikundi vya uzalishaji zinazotumia nishati ya kuni na mkaa zianze kutumia nishati mbadala kwa kupikia na shughuli nyingine za uzalishaji. Ametoa wito huo leo (Jumanne Juni Mosi, 2021) wakati akitoa tamko kuhusu Wiki ya Mazingira Duniani, katika ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma. Amesema kuwa taasisi kama shule, vyuo, hospitali na majengo makubwa zinapaswa kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia. “Kila Wizara ifanye ufuatiliaji kwenye taasisi zake na nipatiwe taarifa ya hali ya utekelezaji kila baada ya miezi sita inayoonesha ni taasisi ngapi zimefikiwa, zimebadili mifumo au zimejenga majengo kwa kuzingatia hitaji la nishati mbadala” “Suala la uhifadhi, utunzaji, usimamizi na usafi wa mazingira lisiwe jambo linalofanyika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani pekee, bali tujenge tabia ya kuliona kwamba ni suala la kila siku” amesisitiza