WCF YATOA MAFUNZO KWA MADAKTARI 1,178 NCHI NZIMA YA KUFANYA TATHMINI ZA ULEMAVU ULIOTOKANA NA AJALI NA MAGONJWA YATOKANAYO NA KAZI

 NA KHALFAN SAID, MOROGORO

KATIKA kuhakikisha huduma za tathmini ya ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi zinawafikia walengwa huko waliko kwa haraka na kwa wakati, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umezidi kuongeza mtandao wa madaktari na watoa huduma za afya kwa  kuwapatia mafunzo ya kufanya kazi hiyo.

Akizungumza mjini Morogoro wiki hii wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya tahmini ya ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi madaktari na watoa huduma za afya 93 kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema baada ya mafunzo hayo idadi ya madaktari na watoa huduma za afya wenye ujuzi wa kufanya tathmini itaongezeka kutoka 1,085 iliyokuwepo na kufikia 1, 178 nchi nzima.

“Lengo ni kuongeza mtandao wa wataalamu wenye ujuzi kwenye hospitali za umma na binafsi nchini kote ili kuondoa changamoto ya kuwafikia walengwa kwa muda na kwa haraka na hivyo kutoa tathmini stahiki na kwa wakati.” Alisema Dkt. Mduma

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar akizunguzma wakati wa kufunga mafunzo hayo Ijumaa Juni 18, 2021 alisema mafunzo hayo yaliendeshwa na wataalamu kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa kushirikiana na wataalamu wabobezi wa masuala ya tathmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

“Tuna hakika watakuwa wamefaidika sana na utaalamu huu ambao ni mpya kwao na kwetu sisi kama Mfuko tumedhamiria kwa dhati kuhakikisha huduma zetu zinafika kila pembe ya nchi yetu na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi watakaopata matatizo hayo kazini.” Alisema Dkt. Omar.

Baadhi ya madaktari walioshiriki mafunzo hayo walieleza jinsi yalivyowawezesha kuwapa utaalamu na uwelewa kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi na jinsi wanavyotakiwa kufanya tathmini kwa mtu aliyepata ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi kwa weledi.

“Nitakuwa balozi mzuri kwa wataalamu wenzangu kwenye kituo changu cha kazi kwani nimeelewa kuwa tathmini za ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi, itafanyika tu pale mgonjwa atakapokuwa amepona na kwamba hakuna tena tatizo litakaloendelea baada ya matibabu  (Maximum Medical Improvement-MMI) na sio kabla.”Alisema Dkt. Mohammed Khalifa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara.

Naye Dkt. Noel Saitoti kutoka Hospitali ya Ekenywa jijini Dar es Salaam alisema kabla ya kufika kwenye mafunzo hayo licha ya kuifahamu WCF kama ni Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi mafunzo yamesaidia kujenga uelewa zaidi wa majukumu ya Mfuko kuwa ni zaidi ya kulipa fidia.

“Baada ya mafunzo haya nimejifunza kuwa Mfuko pia unatoa mafao mbalimbali kama vile Fao la matibabu, na ikitokea mfanyakazi amefariki kutokana na kazi basi wale wategemezi wanapata fidia.” Alisema Dkt. Saitoti.

Akieleza zaidi kuhusu manufaa aliyoyapata baada ya mafunzo, Dkt. Saitoti alisema mafunzo aliyoyapata hakuwahi kujifunza hapo kabla, kwa hiyo ameongeza utaalamu kwenye eneo maalum na kuupongeza Mfuko kwa kuandaa mafunzo hayo na kuomba mafunzo yaendelee ili kuweza kuwapata wataalamu wengi zaidi wenye uwezo wa kufanya tathmini.

“Nawaasa watoa huduma wenzangu (madaktari) tunatakiwa kuwa katikati yaani tutende haki, kama mtu anastahili kupata mafao tufanye tathmini kama tulivyojifunza ili kuusaidia Mfuko kutenda haki, kwa sababu mtu anayeonana na yule mgonjwa ni sisi madaktari kwa hiyo maelezo ya kina kuhusu tatizo lililompata muathirika ni sisi madaktari ndio tunaolibeba kwa hiyo tunaowajibu mkubwa wa kimaadili kuona tatizo lilipo na kuwasilisha kwa Mfuko ili aweze kupata haki inayostahili.” Alisema Dkt. Noel Saitoti kutoka Hospitali ya Ekenywa ya jijini Dar es Salaam.

Aidha Dkt. Husna Lusasi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, yeye alisema wilaya ya Mkuranga ina viwanda vingi sana na kumekuwepo na idadi kubwa ya vijana wanaoumia kutokana na kazi hivyo pamoja na Mfuko kuwahudumia kwa kuwapatia fao la matibabu na wakati mwingine fidia, kuna haja ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha wenye viwanda wanatoa vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi wao na wawe wanavitumia.

“Tuwasaide vijana hawa kwa kufanya ukaguzi wa mazingira ya kazi wa mara kwa mara ili tuwanusuru na ajali, taifa linahitaji nguvu kazi hii kwa ajili ya maendeleo.” Alisema Dkt. Lusasi.

Mafunzo haya yametupa elimu kuu mbili mosi ni kwa waajiri kutambua watumishi wao wanatakiwa kuwa kwenye mazingira sahihi na salama ya kazi mfano kwa kutoa vitendea kazi maalum kwa ajili ya kuwalinda wakiwa kazini na pili ikibidi mfanyakazi kaumia au kuugua kutokana na kazi basi mfuko utatoa matibabu sahihi ili waweze kurudi kazini mapema iwezekanavyo.

Akifunga mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Ukio Kusirye aliwataka madaktari hao kuitumia elimu iliyotolewa katika mafunzo hayo ili kuwawezesha kufanya tathmini ya ulemavu (Impairment Assessment) kwa ufanisi na uweledi wa hali ya juu na hatimaye kuwasaidia wagonjwa na kusaidia Mfuko utimize lengo la kutoa fidia stahiki na kwa wakati.


Baadhi ya madaktari na watoa huduma za afya waliokuwa wakishiriki mafunzo ya siku tano ya tathmini za ulemavu utokanao na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi wakiwa wameshika stika ambazo watazibandika kwenye hospitali zao ili kuonesha wataalamu wa tathmini wanapatikana kwenye hospitali hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Laura Kunenge akimkabidhi stika ya WCF, Dkt. Sechelela Pesse kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya siku tano kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma ya afya ya jinsi ya kufanya tathmini za ulemavu utokanao na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi mjini Morogoro Juni 18, 2021. Stika hiyo itabandikwa hospitalini hapo ili kuonyesha kuwa huduma za tathmini kwa mfanyakazi aliyeumia au kuugua kutokana na kazi zinapatikana.

Dkt. Noel Saitoti na baadhi ya madaktari na watoa huduma za afya waliokuwa wakishiriki mafunzo ya siku tano ya tathmini za ulemavu utokanao na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi wakiwa wameshika stika ambazo watazibandika kwenye hospitali zao ili kuonesha wataalamu wa tathmini wanapatikana kwenye hospitali hiyo.
Dkt. Mohammed Khalifa wa Hospitali ya wilaya ya Newala mkoani Mtwara, akionyesha stika ya WCF.
Madaktari wakipitia stika hizo
Dkt. Husna Lusasi kutoka Hospitali ya wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani  akipoeka cheti cha kuhitimu mafunzo hayo kutoka kwa Katibu wa Afya wa Mkoa wa Morogoro, Verediana Kajala
Katibu wa Afya wa Mkoa wa Morogoro, Verediana Kajala, akitoa hotuba ya kufunga mafunzo kwaniaba ya mganga mkuu wa mkoa.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar akizunguzma wakati wa kufunga mafunzo

Baadhi ya madaktari walioshiriki mafunzo hayo

Baadhi ya madaktari walioshiriki mafunzo hayo
Baadhi ya madaktari walioshiriki mafunzo hayo
Baadhi ya madaktari walioshiriki mafunzo hayo
Dkt. Robert Mhina mtaalamu wa upasuaji wa mifupa akionesha kwa vitendo namna ya kufanya tathmini kwa mtu aliyeumia kutokana na ajali
Meneja wa Tathmini za Madai, Mfuko wa Fidida kwa Wafanyakazi, Dkt. Ally Mtulia, akijibu baadhi ya hoja za washiriki kuhusu utaratibu wa kuwasilisha madai kwa mfanyakazi aliyeumia au kuugua kutokana na kazi.
Afisa Tathmini za madai, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Matilda Rusibamayila, akiwasilisha mada kuhusu Mafao yatolewayo na Mfuko na Huduma inazotoa.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omary akijibu na kufafanua hoja mbalimbali za washiriki kuhusu masuala ya tathmini na utaratibu wakuwasilisha madai

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"