4/16/2021

MAREKANI YAIAHIDI NEEMA TANZANIA

 Na. Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

MAREKANI imeahidi kushirikiana na Tanzania kukuza mitaji na kuvutia uwekezaji kutoka nchini humo ili kuchochea zaidi uchumi na huduma za kijamii hapa nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Don Wright, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ofisini kwake Jijini Dodoma

“Uhusiano wa Tanzania na Marekani ni imara na umedumu kwa zaidi ya miaka 60 sasa, ni wajibu wangu kuendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano huu kwa kuwahamasisha wawekezaji wengi zaidi kutoka Marekani kuja kuwekeza teknolojia na mitaji yao hapa nchini” alifafanua Dkt. Wright.

Mhe. Balozi Don Wright ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu, ameainisha maeneo mengine ya kipaumbele kwamba ni kuwekeza na kuimarisha sekta ya afya pamoja na kuanzisha program ya kusaidia vijana wa Kitanzania kwa kuwajengea uwezo, ujuzi  na maarifa ili kukuza maarifa yao pamoja na ajira.

“Kwa miongo kadhaa sasa Marekani imekuwa ikishirikiana na Tanzania kupambana na maradhi kama vile ukimwi, kifua kikuu, malaria, kutekeleza program za uzazi wa mpango, masuala haya tutayaimarisha zaidi” aliongeza Dkt. Wright

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa  Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amemhakikishia Mheshimiwa Balozi Wright, kwamba Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na kumshukuru Balozi huyo kwa kuahidi kuwahamasisha wawekezaji wengi kutoka Marekani kuja kuwekeza hapa nchini.

Alibainisha kuwa kunapokuwa na uwekezaji mkubwa nchini kutachochea mitaji, ajira, pamoja na kuwa chanzo cha kukuza sekta nyingine zinazozalisha malighafi zinazotumika viwandani na vile vile kitakuwa chanzo cha kodi zitakazosaidia kutekeleza miradi ya maendeleo na kusisimua uchumi wa nchi.

Ameeleza pia kuwa mambo mengine waliyojadili na mgeni wake ni namna ya kuboresha mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani hususan masuala ya misamaha ya kodi kwenye misaada inayoletwa na Marekani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini, baada ya Serikali kubaini kuwepo kwa udanganyifu wa baadhi ya mashirika kutumia vibaya misamaha hiyo, serikali iliweka zuio.

Alimwahidi balozi huyo kwamba Serikali itapitia upya mkataba huo kwa kuwashirikisha wataalam wa pande zote mbili ili walete mapendekezo ya namna ya kufanya kwa lengo la kutokwamisha upatikanaji wa misaada hiyo pamoja na namna ya kuziba mianya ya matumizi mabaya ya misaada hiyo iliyokuwa inafanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

 “Kuna maeneo ambayo sisi kama Serikali tumepanga kuyaangalia ili tusikose misaada kutoka kwa wenzetu kwa sababu ya kuwadai kodi kwenye misaada wanayoyotupa na kwa kufanya hivyo tunakosa kodi pamoja na misaada iliyokuwa ielekezwe kwenye miradi ya maendeleo, tunapoikatalia” alisema Dkt. Nchemba.

Kuhusu suala la kuwasaidia vijana, Dkt. Nchemba aliishukuru Marekani kwa kudhamiria kuleta program ya kusaidia kundi hilo kwa kutengeneza taasisi zinazoweza kuwaandaa vijana kujiajiri, jambo linalowakabili wahitimu wengi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akikabidhiwa kitabu na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Dkt. Don Wright, baada ya Mkutano wao uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.



Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akielezea kuhusu nchi ya Marekani na Tanzania kushughulikia maeneo yaliyokuwa yakitumika vibaya kutokana na msamaha wa kodi katika bidhaa na huduma zinazoingizwa nchini, wakati wa mkutano kati yake na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Don Wright (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Don Wright, akieleza nia ya nchi yake kuwekeza katika Taasisi zinazowaandaa vijana kuwa mahiri katika nyanja mbalimbali za maendeleo, wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, akifafanua jambo wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Don Wright (hawapo pichani), jijini Dodoma.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Don Wright (kushoto) na Afisa Uchumi kutoka Ubalozi huo Bi. Ann Warmenhoven, wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), alipokuwa akielezea hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, katika ukumbi wa Wizara hiyo, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akimuongoza mgeni wake Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt. Don Wright, baada ya mkutano kati yao ulioangazia masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa tano kulia) na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Dkt. Don Wright (wa tano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, baada ya mkutano ulioangazia maendeleo na ushirikiano kati ya nchi hizo, uliofanyika jijini Dodoma.

    

0 comments:

Post a Comment