3/02/2021

WAZIRI LUKUVI AAGIZA MAENEO YA MRADI WA KIMKAKATI KUPANGWA

Na Munir Shemweta, MISUNGWI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameitaka halmashauri ya wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza kuhakikisha inapanga na kupima maeneo yanayopitiwa na miradi ya kimkakati ya treni ya Mwendokasi (SGR) na Kivuko cha Kigongo katika halmashauri hiyo mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo ya miradi ya upimaji katika maeneo ya miradi hiyo leo tarehe 1 Februari 2021 Lukuvi alisema, hakuna kuendeleza maeneo yanayopitiwa na miradi ya SGR na Kivuko cha Kigongo mpaka maeneo hayo yatakapopangwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

" Maisha lazima yabadilike na msinyang'anye wananchi maeneo yao bali maeneo hayo yapangwe na kupangiwa matumizi yatakayoendana na hadhi ya miradi" alisema Lukuvi.

 Alisema, halmashauri ni mamlaka ya upangaji hivyo Misungwi inapaswa kuzuia kuendelea kwa ujenzi katika maeneo hayo mpaka yapangwe kwa lengo la kupandisha hadhi na kuwa mji wa kisasa (modern city) ambapo alisisitiza kuwa haiwezekani kuacha eneo linaloweza kuhudumia takriban nchi tano likaachwa kiholela.

" Zuieni maendezo yote kandokando ya daraja ili muyapange vizuri na wanaotaka kuendeleza mhakikishe wanaendeleza yale yanayoshabihina na mradi" aliongeza Waziri wa Ardhi.

Aliongeza kwa kusema kuwa kiasi cha shilingi milioni 300 ilizokopeshwa  halmashauri ya wilaya ya Misungwi na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ziendelee kubaki kwa ajili ya kupanga maeneo ya mradi na kubainisha kuwa, hata halmashauri hiyo ikihitaji wataalamu kutoka wizarani kusaidia mradi wa upimaji katika eneo hilo  basi inaweza itapatiwa.

"Lazima misungwi uwe mji maarufu mtu akitaka kuja kulala aje maana hili ni daraja la kimkakati litakalohudumia  takriban nchi tano, tunataka satelite city iliyopangwa na itakayokuwa na huduma zote za msingi zenye hadhi inayofanana na mji huo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alitembelea eneo la mradi wa upimaji katika kitongoji cha Kigongo kilipo kivuko cha Kigongo (Kigongo Ferry) pamoja na eneo la kimkakati la Fella inapopita treni ya Mwendokasi ya SGR.  

Mkuu wa Idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Misungwi Fredrick Nyoka alisema, tayari idara imeanza kazi ya upangaji na kupima maeneo yanayopitiwa na miradi ya SGR na Kivuko cha Kigongo na tayari baadhi ya wananchi wameshalipwa fidia na Mamlaka ya Bandari Tanzania huku Shirika la Reli likitarajiwa kumaliza kuwalipa fidia wananchi mwisho wa wiki hii.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akioneshwa ramani ya eneo la kimkakakti la Fella inapopita reli ya Mwendokasi ya SGR wakati wa ziara yake katika wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza tarehe 1 Februari 2021
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza wakati akikagua mradi wa upimaji katika kitongoji cha Kigongo unapopita mradi wa kimkakati wa kivuko cha Kigongo wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza tarehe 1 Februari 2021 wakati wa ziara ya kikazi katika mkoa huo.

    

0 comments:

Post a Comment