Wednesday, March 31, 2021

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AMTEUA BALOZI HUSSEIN A. KATTANGA KUWA KATIBU MKUU KIONGOZI


NA K-VIS BLOG

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Hussein A. Kattanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuchukua nafasi ya aliyekuwa akishika wadhifa huo Balozi Dkt. Bashiru Ali Kakurwa ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge.

Rais amefanya mabadiliko hayo wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma Machi 31, 2021.

Rais pia amefanya mabadiliko kwenye baraza la Mawaziri ambapo Mhe. Mwigulu Nchemba ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango akitokea wizara ya Sheria na Katiba.

Rais amemuhamisha Mhe. Ummy Mwalimu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na kumpeleka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, huku aliyekuwa Waziri kwenye ofisi hiyo Mhe., Selemani Jafo amehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais.

Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi amehamishiwa Wizara ya Sheria na Katiba ambapo Waziri wa Mambo ya Nje sasa atakuwa Balozi Liberata Mulamula ambaye awali aliteuliwa na Rais kuwa Mbunge.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge Job Ndugai, mara baada ya hafla ya Uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kushuhudia Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akitia saini Hati ya Kiapo mara baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

0 comments:

Post a Comment