Tuesday, January 26, 2021

WAZIRI BASHUNGWA KUTOA KADI ZA MATIBABU KWA WANAMUZIKI

 

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Stella Joel.
 


Na Dotto Mwaibale


WAZIRIa wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) litakalofanyika Februari 13, 2021 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel alisema pamoja na mambo mengine Bashungwa atatoa  kadi za Bima ya Afya ya NHIF kwa Wanamuziki pamoja na kusikiliza changamoto zao mbalimbali ili kuzipatia ufumbuzi.

"Serikali imetukumbuka wanamuziki kwa kutupatia kadi za bima ya afya ya Taifa kwa gharama nafuu kupitia Tanzania Music Foundation (TAMUFO) jambo litakalo tusaidia wanamuziki kupata matibabu." alisema Joel. 

Joel aliwataja baadhi ya wanamuziki watakao kabidhiwa kadi hizo kuwa ni wa muziki wa Injili, bongo fleva, dansi, taarabu na ngoma za asili. 

Aidha Joel alisema kitendo cha Serikali kutoa kadi hizo za bima ya afya kwa wanamuziki ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuwasaidia wasanii hapa nchini.

Katibu mkuu huyo wa TAMUFO alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kuelezea kuwa wamepata ari na nguvu mpya  ya kutekeleza shughuli zao kwa vitendo kwa ajili ya maendeleo ya sanaa hapa nchini.

Alisema maandalizi yote ya kongamano hilo yamekwisha kamilika ikiwa na taratibu  za kuwapata wanamuziki. 

Joel aliongeza kuwa katika kongamano hilo maafisa kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na maafisa utamaduni na wadau wengine watakuwepo.

0 comments:

Post a Comment