1/18/2021

TARURA SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA BILIONI 1.8 UJENZI WA DARAJA WILAYANI MANYONI

 

Watendaji wa  Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Manyoni wakikagua daraja hilo.

Wananchi na vyombo vyao wakivuka mto Nkonjigwe kwa kutumia daraja hilo.
Wananchi wanaozunguka maeneo ya daraja Nkonjigwe wakifurahia kutokana na kujengewa daraja hilo.


Na Dotto Mwaibale, Singida.


SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kupitia watendaji waaminifu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) imeokoa zaidi ya bilioni 1.8 kwenye ujenzi ambao tayari umekamilika wa daraja la Mto Nkonjigwe Wilayani Manyoni mkoani hapa.

Kabla ya kuanza kwa ujenzi huo kati ya Juni na Septemba upembuzi yakinifu wa mradi huo kupitia wazabuni mbalimbali ulikadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 2, kabla ya Tarura kufanya maamuzi magumu ya kutumia mfumo wa Force Account.

Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kunakwenda kufungua fursa za uhakika wa upatikanaji wa huduma za afya hususani kwa akina mama wajawazito sambamba na kuimarisha wigo wa kibiashara kwa wakazi wa kata takribani tano zinazotumia njia inayounganishwa na daraja hilo yenye urefu wa km 76.2.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wanaozunguka eneo hilo akiwemo Halima Abdallah mkazi wa Kijiji cha Chikuyu alisema wamefurahishwa na ujenzi wa daraja hilo ambalo litawasaidia akina mama wajawazito kuvuka na kwenda kujifungua kwenye Zahanati za Kilimatinde na Chikuyu kwani awali wengi walikatisha maisha yao kwa kushindwa kuvuka mto huo.

Halima alisema walikuwa wanatoa shilingi elfu 2 hadi elfu 3 kuvushwa kwenye Mto huo na watu wenye uzoefu wa kuogelea jambo ambalo halikuwa salama kwao kwani kuna wakati licha ya uzoefu wao hushindwa kuvuka na kupelekwa na maji pamoja na aliyekuwa anavushwa.

"Tulikuwa tukifika hapa tunavua nguo halafu ndio tunavushwa, tunatoa shilingi elfu 2 za mtu kuvushwa na shilingi elfu 3 za nguo.watu wamekufa wengi sana hapa hasa Wanawake wajawazito." alisema  Halima.

Thomas Minaloganawenda mkazi wa Kijiji cha Chinyika kilichopo Kata ya Sasajila alisema moja ya shughuli kubwa ya kiuchumi kwenye maeneo haya ni uchimbaji wa chumvi lakini kuna wakati ilikuwa ikiharibikia kwenye mto kutokana na kukosa daraja.

Alisema amefanya kazi ya kuwavusha watu kwenye mto huo kwa muda mrefu licha ya kujipatia ujira lakini ilikuwa inaumiza anapoona wengi wakipoteza maisha hakuwa anafanya kazi hiyo kwa raha ila ni katika kujaribu kuokoa maisha ya watu waliokuwa wanafika hapo na kuhitaji kuvuka kwenda kupata huduma.

Awali Mratibu wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Boniphace William alisema ujenzi wa daraja hilo umegharimu shilingi milioni 122,415,500 hadi kukamilika kwake ambapo limetumia mfumo wa raslimali za ndani 'Force Account' 

Aidha, William alisema daraja hilo linatoa fursa ya upatikanaji wa huduma mbalimbali kuzunguka Vijiji vya Chikuyu,Chibumagwa, Sasajila, Majiri na Sanza.

"Nawaomba wananchi wanaohudumiwa na daraja hili na miradi mingine sehemu mbalimbali kutambua miradi hiyo ni kwa ajili yao, hivyo ni wajibu wao kuitunza na sio suala la Tarura pekee, wakijenga tabia hiyo miradi mingi itadumu kwa muda mrefu." alisema William.

Kwa upande wake Meneja wa Tarura Wilaya ya Manyoni Mhandisi Yose Mushi alisema daraja hilo ambalo lina urefu wa mita 53 na mita 25 eneo la kupitisha maji, kadhalika lenye tuta mita 28 linatarajia kuchagiza kasi ya ustawi wa uchumi kwa wakazi wanaozunguka maeneo hayo. 

    

0 comments:

Post a Comment