TAARIFA YA BENKI KUU YA TANZANIA

Taarifa ya Kamati ya Sera ya FedhaKamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Benki Kuu ya Tanzania katika kikao chake cha 212 kilichofanyika tarehe 22 Januari 2021, imeamua kwamba Benki Kuu iendelee na utekelezaji wa sera ya fedha ya kuongeza ukwasi ili kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia mikopo ya mabenki kwa sekta binafsi.

 Aidha, Kamati imeidhinisha kufanyika minada ya dhamana za Serikali za muda mfupi na muda mrefu kwa ajili ya uendeshaji wa bajeti ya Serikali kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Serikali wa kuuza dhamana hizo katika mwaka wa fedha 2020/21.Kamati imeridhika kwamba, tangu kikao chake kilichopita, mwenendo wa uchumi wa Tanzania umekuwa wa kuridhisha, licha ya changamoto za athari za COVID-19 kwenye uchumi wa dunia. 

Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020, uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 4.9. Sekta zilizoongoza katika kuchangia ukuaji huo ni ujenzi, kilimo, usafirishaji na madini. Mfumuko wa bei uliendelea kuwa mdogo na tulivu katika nusu ya pili ya mwaka 2020, ukiwa kati ya asilimia 3.0 na 3.3, kutokana na kuwapokwa chakula cha kutosha, pamoja na utulivu katika thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni na bei za mafuta ya petrol na dizeli nchini. 

Sekta ya nje imeendelea kuimarika kutokana na mauzo nje ya nchi, hususan dhahabu, mazao ya kilimo na bidhaa za viwandani. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kutosheleza uwezo wa kugharamia bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 5.6. 

Mwenendo wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali unaendelea vizuri kutokana na kuimarika kwa mapato yatokanayo na kodi.Kamati ya Sera ya Fedha imeridhika kwamba utekelezaji wa sera ya fedha ya kuongeza ukwasi katika uchumi umewezesha kupungua kwa riba za muda mfupi, na hivyo kuweka mazingira mazuri kwa mabenki kuongeza mikopo kwa shughuli za biashara na uwekezaji nchini. 

Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa wastani wa asilimia 5.1 katika kipindi cha miezi sita ya mwisho ya mwaka 2020, inatarajiwa kuendelea kuongezeka katika nusu ya pili ya mwaka wa fedha wa 2020/21 kutokana na uchumi wa dunia kurejea katika hali ya kawaida. Sekta ya benki iliendelea kutoa faida na kuwa na mtaji wa kutosha unaoweza kuhimili mitikisiko ikitokea.

Kutokana na mwenendo wa kuridhisha hivi karibuni katika sekta muhimu za uchumi, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhika kwamba matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia 5.5 kwa mwaka 2020 yatafikiwa, na kwamba kuna matarajio ya ongezeko kubwa la ukuaji wa uchumi wa takribani asilimia 6 au zaidi, katika mwaka 2021. 

Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa mdogo na tulivu, ukiwa ndani ya makadirio ya wigo wa asilimia 3 na asilimia 5, kwa kuwa hakuna viashiria vya kusababisha mfumuko wa bei kupanda. Kutokana na matarajio hayo mazuri ya viashiria vya uchumi, thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kuwa tulivu. 

Aidha, Kamati ya Sera ya Fedha, iliridhika na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha mabenki yanaongeza mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza riba za mikopo, Kamati imeitaka Benki Kuu kuendelea kushirikisha mabenki na wadau wengine ili kufanikisha jitihada za mabenki kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kwa riba nafuu.

Gavana 

Benki Kuu ya Tanzania

 

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"