Thursday, December 31, 2020

WANAVYUO JIAMININI ELEZENI VITENDO VYA UKATILI NA UNYANYASAJI WA KIJINSIA UNAOTOKEA MAENEO YENU.


Mkuu wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Arusha mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Happiness Temu akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha ufundi Arusha kuhusiana na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu unaohusisha makosa ya mitandao katika kikao kilichofanyika katika bwalo la chuo hicho Jijini la Arusha.
Mlezi wa wanafunzi Bi. Stella Ngowa (aliyekaa katikati), Rais wa serikali ya wanafunzi katika chuo cha ufundi Arusha (aliyevaa koti jeusi) Bwana Issa Mohamed wakifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa katika kikao kilichojadili masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu unaohusisha makosa ya mitandao kilichofanyika katika bwalo la chuo hicho mapema leo Jijini Arusha.
Mmoja wa mshiriki akichangia mada katika kikao kilichojadili masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu unaohusisha makosa ya mitandao kilichofanyika katika bwalo la chuo cha ufundi Arusha  Jijini Arusha.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinatolewa katika kikao kilichojadili masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu unaohusisha makosa ya mitandao kilichofanyika katika bwalo la chuo hicho  Jijini Arusha.

Na Vero Ignatus Arusha

Wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati wametakiwa kuwa na uwezo wa kujileza na kujiamini kueleza na kubainisha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia vinavyotokea katika maeneo yao .

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa dawati la Jinsia na watoto mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Happiness Temu wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa chuo cha ufundi Arusha kuhusiana na masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu unaohusisha makosa ya mitandao katika kikao kilichofanyika katika bwalo la chuo hicho.

Alisema kuwa ngazi ya chuo ni sehemu muhimu yenye jamii kubwa ya wanafunzi ambao wametoka maeneo mbalimbali na kukutana ndani ya chuo wakiwa na tabia tofauti, hivyo kutokana na tabia hizo vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa  wanafunzi wamekuwa na aibu kuvieleza.

‘‘Wapo baadhi ya wanafunzi wanawafanyia wenzao vitendo vya kikatili na wanaona ni mambo ya kawaida na wale wanaofanyiwa ukatili wanaumia lakini kwa hofu wanaogopa kusema au  hawaelewi ni wapi wanaweza kupeleka malalamiko yao, tunawaasa wawe na uwezo wa kujieleza kwa sababu kuwa na jamii ya wasomi ambao ni waoga wa kujieleza kuhusiana na vitendo vya ukatili ama kuona aibu ni vibaya, hivyo tumefika hapa ili kuwajengea uelewa na uwezo ili waweze kutoka na kukemea vitendo hivyo kwenye jamii’’.  Alisema Mkuu huyo wa dawati la jinsia.

Aidha alisema ili kuweza kuisaidia jamii, ni wakati sasa wa kutengeneza watu ambao watatoka vyuoni wakiwa bora na wasiopenda masuala ya ukatili na wenye uwezo wa kukemea, hivyo waliona ni vyema elimu hiyo waitoe katika maeneo ya vyuo.

Naye rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho Bwana Issa Suleiman Mohamed kwa niaba ya wanafunzi  wa chuo hicho alitoa shukrani kwa jeshi la polisi mkoa wa Arusha kupitia kitengo cha dawati la jinsia na watoto kwa elimu  waliyoitoa kuhusiana na masuala ya ukatili na uhalifu unaotokana na matumizi mabaya ya mitandao.

Alisema elimu hiyo imekuja katika muda muafaka kwakuwa asilimia kubwa ya wanafunzi wanatumia mitandao na hawana uwelewa kuhusu uhalifu wa kimtandao pamoja na masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambapo watahakikisha elimu hiyo inawafikia wanafunzi wote chuoni hapo.

‘‘Kama wanafunzi tutaangalia ni namna gani tunahamasishana ili kujiepusha na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na matumizi mabaya ya mitandao ambayo inaweza kutupelekea katika makosa ya uhalifu wa mitandao’’. Alisema  Issa

Aliendelea kusisitiza kwa kuwa wanafunzi wanatoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, anaimani elimu waliyoipata itasambaa maeneo yote kwani watakuwa mabalozi wazuri wa kuieleza jamii kuepukana na makosa hayo.

Huo ni mwendelezo wa elimu ambazo dawati hilo la jinsia na watoto mkoa wa Arusha linatoa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni, vyuoni na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata uelewa kuhusiana vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

0 comments:

Post a Comment