Sunday, November 29, 2020

TANESCO MSHINDI WA JUMLA MASHINDANO YA SHIMMUTA

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya SHIMMUTA baada ya kunyakua vikombe tisa na kuibuka kidedea katika mashindano hayo ya michezo ya mwaka 2020, yanayofanyika Mkoani Tanga.

Matokeo hayo yanaifanya TANESCO kuwa mshindi wa jumla katika mashindano ya SHIMMUTA mwaka huu yaliyomalizika Mkoani Tanga.

Michezo ambayo TANESCO imeibuka na ubingwa ni wavu wanaume na wanawake, kikapu wanaume na wanawake. Aidha, TANESCO imekuwa mshindi wa pili mchezo wa pete.

Hii ni mara ya nne mfululizo timu ya kikapu wanaume wanakuwa washindi, na mara ya pili mfululizo kwa timu ya wavu wanaume inaibuka na ushindi. 

Kwa upande wa michezo ya jadi TANESCO imeshinda mchezo wa bao wanawake, karata wanaume na mshindi wa pili bao kwa wanaume. 

Mbali ya vikombe hivyo, TANESCO pia imepata medali saba ambapo Polycaps Ernest amekuwa mahindi wa tatu mbio za mita 100 na mita 200, Kulwa Mangala mshindi wa pili mita 1500, Grace Moshi mshindi wa pili mita 400 na 800, mshindi wa tatu mita 100, Imelda Hango 3000 wa tatu.

Akimwakilisha Meneja Mwandamizi Rasilimali Watu, Festo Mkolla ambaye ni, Meneja Usimamizi Utekelezaji Kazi TANESCO, ameishukuru Menejimenti kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Tito Mwinuka kwa kuona thamani ya michezo na kuipa kipaumbele.

Aidha, amewapongeza wanamichezo wa TANESCO kwa nidhamu, juhudi na hali ya kutetea Shirika kwenye mashindano ambayo wameionesha katika kuhakikisha kila mchezo wanaibuka na ushindi.

"Niwaagize viongozi wa timu ambazo hazikuibuka na ubingwa kuhakikisha mnaweka mikakati ili mwakani tuondoke na vikombe vyote" alisema Mkolla.

 Aliongeza, kwa upande wa uongozi wa TANESCO utahakikisha yanafanyika mashindano ya Kanda za kitanesco ili kupata vipaji vipya vitakavyoongeza nguvu kwa wachezaji waliopo.
 

0 comments:

Post a Comment