WATAALAMU WA AFYA NA MAZINGIRA WATAKIWA KUJISAJILI NA KUHUISHA LESENI ZAO

Na WAJMW-Dodoma

Wataalamu wa Afya na mazingira nchini wametakiwa kujitokeza kujisajili na kuhuisha leseni zao ili waweze kutambulika na kupata nafasi ya kufanya kazi kwa weledi na bila usumbufu.

Hayo yamesemwa na kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliud Eliakim wakati alipomuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Mazingira la awamu ya nne kilichofanyika leo katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma. 

Dkt. Eliud amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanikiwa kuhuisha mwongozo wa maadili na nidhamu kwa watumishi wa umma ambapo kila Baraza limetakiwa kufuata mwongozo huo ili lisimamie maadili na nidhamu ya taaluma husika.

Baraza la Afya ya Mazingira limetakiwa kuhakikisha wataalam wote wa Afya ya Mazingira wakiwemo maafisa afya nchini wanajitokeza kujisajili na kuhuisha leseni zao ili waweze kusimamia vyema mazingira kwa kutoa miongozo na kufanya usafi ili kuweza kuepuka magonjwa ya milipuko yanayoweza kujitokeza.

Aidha, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali amelitaka Baraza kupitia upya Sheria kwa kuangalia maeneo muhimu kwa ajili ya kufanya maboresho na pia kumshauri Mhe. Waziri ili kutengeneza kanuni chini ya Sheria ya usajili sura 428.

Kwa upande wake Msajili wa Baraza hilo Iddi Hoyange amesema kikao hicho kilichohusisha wadau mbalimbali wa mazingira kilikua na malengo mahsusi ikiwa ni Pamoja na kufahamiana, kupokea majukumu kutoka kwa wajumbe na kupata kamati za baraza zinazoundwa kwa misingia ya kisheria.

Bwana Hoyange amesema Baraza limetoa muda wa kujisajili na kuhuisha leseni kwa Wataalamu wa Afya ambapo mwezi Februari mwaka 2021 utakua mwisho wa kujisajili na ametoa wito kwa wataalamu hao kufanya hivyo kwani baada ya muda huo Baraza litaanza kufanya ukaguzi na kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote hawatatii wito huo.

Nae Mwenyekiti wa Baraza hilo Dkt. Hussein Mohamed amesema kikao hicho kimekua na mafanikio baada ya kupitia mambo mbalimbali yanayohusu taaluma ya Afisa afya Mazingira ambapo moja ya vitu vilivyozungumziwa ni Pamoja na kuweka mkakati wa muundo wa taaluma ya Afisa Afya na kuweka mipango ya kukusanya maduhuli ili Baraza hilo liweze kujiendesha.







 

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"