Monday, October 26, 2020

RC KUNENGE AWATAKA BODABODA KUWAFICHUA WAHALIFU, ASEMA SERIKALI ITAENDELEA KUWAWEKEA MAZINGIRA BORA YA KAZI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge amewataka waendesha Bodaboda na Bajaji kuwa  mabalozi wazuri wa kulinda amani na utulivu wa Mkoa huo na kuwaomba kutoa taarifa pindi wanapobaini watu au kundi la watu wahalifu.

RC Kunenge ametoa kauli hiyo leo wakati wa mkutano na waendesha bodaboda na Bajaji uliofanyika viwanja vya Mnazi mmoja jijini humo ambapo amesema kazi yao imewafanya wakutane na watu wa aina mbalimbali ikiwemo wahalifu hivyo ni vizuri wakashirikiana na jeshi la polisi pindi wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani.

Aidha RC Kunenge amewahakikishia ushirikiano na Serikali kwenye masuala mbalimbali huku akiwahimiza kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri.

Pamoja na hayo RC Kunenge amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli imefanya kazi kubwa Katika kuwatatulia changamoto na kero zilizokuwa zikiwakabili na itaendelea kuwawekea mazingira Bora na salama ya kufanya kazi ili kuhakikisha ajira yao inaheshimika na kuwanufaisha kiuchumi.

Hata hivyo amewahimiza kujitokeza kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika October 28 kwa kuwachagua Viongozi wanaofaa.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es salaam, RPC Ilala, makamanda wa Polisi, na Bajaji pamoja na waendesha Bodaboda na Bajaji
 

0 comments:

Post a Comment