MAASKOFU NA WACHUNGAJI WAZINDUA KITABU CHA UONGOZI ULIOTUKUKA WA RAIS JOHN MAGUFULI.

 

Askofu Mkuu wa Makanisa ya Naioth Gospel Assemblies of God ambaye pia ni Katibu Mkuu mstaafu wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania, Dkt. David Mwasota., akizungumza na Maaskofu  na Wachungaji kwenye  maombi ya kukiombea Kitabu cha Uongozi Uliotukuka wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki.

Askofu Mkuu wa Makanisa ya Naioth Gospel Assemblies of God ambaye pia ni Katibu Mkuu mstaafu wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania, Dkt. David Mwasota.(kushot) akiwaongoza Maaskofu na Wachungaji kwenye  maombi ya kukiombea Kitabu cha Uongozi Uliotukuka wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki..





Maombi ya kukiombea kitabu hicho yakiendelea kufanyika.

Muonekano wa kitabu hicho.

Bishop Sedrick Ndonde wa Kanisa la Restroration Bible ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kanisa hilo walioandika kitabu hicho,



Uzinduzi wa kitabu hicho ukifanyika.




Na Dotto Mwaibale

MUUNGANO wa Maaskofu zaidi ya 15 na Wachungaji 100 mwanzoni mwa juma walizindua kitabu kinachoelezea uongozi uliotukuka wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Kitabu hicho kimeandikwa na Mtendakazi katika shamba la Bwana, Restoration Bible Church Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi wa kitabu hicho kiitwacho Uongozi Uliotukuka, JPM ni Kiongozi wa Kisiasa na Kiroho, uliofanyika jijini Dar es Salaam uliongozwa na Askofu Mkuu wa Makanisa ya Naioth Gospel Assemblies of God ambaye pia ni katibu Mkuu mstaafu wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania, Dkt. David Mwasota.

Mwasota alisema lengo la kuandikwa kitabu hicho ni kutazama uongozi wa Rais Magufuli kwa pande za kisiasa na kiroho.

Askofu huyo alisema katika utendaji kazi wake, Magufuli anamtegemea Mungu hivyo kumfanya aonekane anaiongoza nchi kwa upande wa kiroho.

“Imani ya Mheshimiwa Magufuli katika kushughulikia janga la Corona kiroho limefanya kuinua imani ya watu wengi kwa kulisaidia kanisa ambalo ndiyo kazi yake kubwa kuwajenga watu kiimani,” alisema askofu huyo.
 
Mwasota aliwaomba maaskofu, wachungaji na waumini wote kuendelea kumuombea Rais Magufuli kwani ndiyo yalikuwa maombi yao kwa miaka mingi kwa Mungu atuletee kiongozi kama yeye.

“Tunamshukuru Mungu aliyejibu maombi yetu kwa kutuletea kiongozi tuliyemuomba miaka mingi ambaye ni Magufuli anayeliongoza taifa letu kisiasa na kiroho,” alisema Mwasota.

Askofu huyo aliongeza kuwa katika nchi yetu hatukuwahi kumpata kiongozi wa juu anayemtaja Mungu wakati wote na kuwaagiza watendaji wake kila anapowaapisha wamtangulize na kumtegemea Mungu.

Naye Bishop Sedrick Ndonde wa Kanisa la Restroration Bible ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kanisa hilo walioandika kitabu hicho, alisema lengo la kitabu hicho ni kuelezea ukweli kuhusu Rais Dkt. John Magufuli ili kufahamu zaidi nini alichobeba mbali ya wadhifa wa urais alionao na kulikumbusha kanisa na watumishi wa Mungu kuutafakari uongozi wake.

“Umuhimu wa kitabu hiki ni kuwakumbusha watumishi wa Mungu kuwa na muda wa kutafakari uongozi wa JPM kwa yote aliyoyafanya kwa upande wa kiroho,” alisema Askofu Ndonde.

Aliongeza kwa kumtegemea Mungu amefanya mambo makubwa kama kujenga miundombinu ya barabara, umeme, maji, shule, hospitali na kuwawezesha watanzania kunufaika na madini, mbuga za wanyama ambapo awali waliokuwa wakinufaika walikuwa watu kutoka nje.

 “Magufuli ni mfalme anayekiri ufalme wa Mungu kutawala taifa letu,” alisema Ndonde.

Ndonde aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kukisambaza kitabu hicho kwa waumini wao na wananchi wengine kwa ujumla  bila kujali dini wala madhehebu wanayotoka ili waweze kuwa na mtazamo chanya. 

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"