10/21/2020

KAMATI YA AMANI MKOA WA SHINYANGA AONYA UVUNJIFU WA AMANI KWENYE UCHAGUZU MKUU

 


Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoa wa Shinyanga Sheikh Khalfani Ally, akizungumza na vyombo vya habari wakati akitoa tamko la kamati ya amani mkoa wa Shinyanga kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu. Picha na Marco Maduhu- Shinyanga.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoa wa Shinyanga Sheikh Khalfani Ally, akizungumza na vyombo vya habari wakati akitoa tamko la kamati ya amani mkoa wa Shinyanga kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoa wa Shinyanga Sheikh Khalfani Ally, akizungumza na vyombo vya habari wakati akitoa tamko la kamati ya amani mkoa wa Shinyanga kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
Wajumbe wa Kamati ya Amani mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga Sheikh Soud Kategile akizungumza kwenye mkutano huo.
Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga,Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Shinyanga mjini John Kilinda, akizungumza kwenye mkutano huo.
Picha na Marco Maduhu- Shinyanga.

***
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kamati ya Amani mkoa wa Shinyanga imewataka Watanzania kutokubali kutumiwa na wanasiasa wakati huu wa kipindi cha uchaguzi hasa siku ya kupiga kura Oktoba 28,2020 huku ikiwaonya baadhi ya viongozi wa dini wanaojitokeza kuungana na watu wanaohamasisha vijana kujitokeza barabarani ,kukaa kwenye vituo vya kupigia kura na kuhamasisha uvunjivu wa amani  kuacha tabia hiyo mara moja.

Rai hiyo imetolewa leo Jumanne Oktoba 20,2020 na Kaimu Mwenyekiti wa kamati  ya Amani Mkoa wa Shinyanga Shekh Khalfan Ally wakati akisoma Tamko la Kamati ya Amani mkoa wa Shinyanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2020.

Alisema kumekuwepo na viashiria kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuanza kuhamasisha wananchi kufanya fujo siku ya uchaguzi hivyo wamewataka kuacha tabia hiyo ili kuepuka uvunjifu wa amani unaoweza kujitokeza katika jamii.

“Kamati ya Amani mkoa waShinyanga inawataka Watanzania kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuvuruga amani ya nchi kwenye uchaguzi mkuu.Tunatoa wito kwa wananchi waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na kisha warudi majumbani mwao wakaendelee na majukumu mengine huku wakisubiri matokeo,” alisema Ally. 

Alisema watanzania wanapaswa kuilinda amani ya nchi ambayo inatamaniwa na baadhi ya mataifa kuvurugika, bali wakatae kushawishiwa na baadhi ya wanasiasa kufanya fujo kwenye uchaguzi mkuu, ili kupeuka uvunjifu huo wa amani. 

"Tunawaasa wazazi na walezi wa familia kujiepusha na kushawishiwa kushiriki maandamano,fujo na vurugu zozote wakati wa uchaguzi kwa matokeo yake watakabiliana na mkono wa sheria wakati wahamasishaji wa vurugu wakikimbia nchi na kuwaacha wachache wakihangaika",alisema Ally.

“Uvunjifu wa amani ukitokea waathirika wakubwa ni watoto, akina mama, wazee na watu wenye mahitaji maalum. Lakini pia uchumi wa nchi utayumba kwa sababu hapatakuwa na shughuli zozote zile za maendeleo,” aliongeza. 

Aidha alisema kamati ya Amani mkoa wa Shinyanga  inatoa rai kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaojitokeza kuungana na watu wanaohamasisha vijana kujitokeza barabarani ,kukaa kwenye vituo vya kupigia kura na kuhamasisha uvunjivu wa amani, kuacha tabia hiyo mara moja kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na misingi ya dini.

"Ikumbukwe kuwa upigaji kura haufanywi kwa misingi ya kidini hivyo Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga inawataka viongozi hao wa dini badala ya kuunga mkono, wakemee suala la udini katika siasa",alisisitiza Ally.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga John Kilinda ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Shinyanga Mjini, alisema mfumo wa vyama vingi uliwekwa kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya nchi, lakini baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kuutumia vibaya. 

Aidha aliwataka viongozi wa vyama vya siasa, wazitumie siku hizi zilizosalia kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, kunadi sera zao kwa wananchi ili wapate kukubalika na kuchaguliwa, na siyo kutaka kutumia nguvu kupata madaraka, na kuhamasisha wananchi kuingia barabarani kufanya maandamano ambayo yatagharimu maisha yao. 
    

0 comments:

Post a Comment