ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI KURAHISISHA BIASHARA MTANDAO

Na Faraja Mpina WUUM, Dodoma

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) na taasisi zilizo chini ya sekta hiyo zipo katika utekelezaji wa mpango mkakati shirikishi wa kukamilisha mpango wa  anwani za makazi na postikodi unaotarajiwa kufikia halmashauri zote nchini ifikapo mwaka 2022 ili kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika ziara ya kukagua uwekeaji wa namba za nyumba katika kata 
Tatu za Chamwino Ikulu, Ipagala na Hazina, jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa ukamilishaji wa mpango huo utarahisisha shughuli za biashara mtandao na huduma za posta mlangoni.

“Wizara ipo kwenye utekelezaji wa mkakati wa kuhakikisha kila nyumba inakuwa na anwani ya makazi inayojumuisha jina la barabara, mtaa na namba ya nyumba, ili wananchi waweze kufikiwa katika maeneo wanayoishi kwa urahisi na  kukuza biashara mtandao na posta mlangoni kuelekea uchumi wa kidijitali”,  alizungumza Dkt. Chaula.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema kuwa, mpango wa anwani za makazi na postikodi unatambulika kimataifa, ukamilishwaji wake utasaidia kuongeza fursa za kibiashara na kujiajiri hasa kwa upande wa biashara mtandao ambapo wananchi wataweza kuagiza bidhaa na kuletewa mpaka mlangoni.

Aliongeza kuwa, utekelezaji wa zoezi hilo unahusisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,TAMISEMI, Halmashauri na wadau mbalimbali ambapo kazi inayoendelea kwa sasa ni uwekaji wa namba za nyumba  katika halmashauri za jiji la Dodoma chini ya mkandarasi SUMA JKT, Jumla ya nyumba 21,947 zitawekewa namba kati ya nyumba 30,152.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema kuwa ushirikishaji wa serikali na wananchi katika zoezi la uwekaji vibao vya namba za nyumba ndio unaorahisisha kufanyika kwa zoezi hilo huku UCSAF ikiwa imechangia shilingi milioni 60 kwa ajili ya kata tatu za Chamwino Ikulu, Bahi na Hazina zilizopo jijini Dodoma.

Mpango wa uwekaji wa anwani za makazi na postikodi umetekelezwa katika kata 116 nchini kati ya kata 3956, kwenye Halmashauri 18 kati ya 185 nchini. Mwitikio wa zoezi hili kwa wananchi ni mzuri kwa sababu wenye manufaa kwa wananchi na Serikali katika ufikishaji wa huduma za dharura, biashara na huduma za posta.

Faida nyingine za mpango huu kwa Serikali ni kurahisisha ukusanyaji wa kodi, kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi na kuhudumia wananchi wakati wa dharura za majanga ya moto na dharura ya wagonjwa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano)




 

Comments

Popular posts from this blog

CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA PABLO FRANCO MARTIN "USIPIME"