9/18/2020

KILIMO CHA UMWAGILIAJI NDIO UKOMBOZI WA MKULIMA -KUSAYA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa na viongozi wa skimu ya umwagiliaji mpunga ya Dakawa wakitazama mtambo wa kusukuma maji kwenda mashambani leo alipotembelea mkoani Morogoro. 
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa tshirt ) akiongea na wakulima wa mpunga katika skimu ya umwagiliaji Dakawa mkoani Morogoro.Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akitazama kifaa kinachotumika kuhamia/kufukuzia ndege shambani kinachotumiwa na kijana Sunday Lukobya ( kulia) leo alipokagua skimu ya umwagiliaji mpunga Dakawa mkoani Morogoro. 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua mashamba ya mpunga ya wakulima katika skimu ya umwagiliaji Dakawa mkoani Morogoro leo.Nyuma yake ni mratibu wa mradi huo Mhandisi Senzia Maeda. 

( Habari na picha na Wizara ya Kilimo) 

********************************** 



Wakulima wameshauriwa kujikita katika kuanzisha mashamba ya mazao ya kilimo kwa kutumia umwagiliaji kama njia ya uhakika wa kupata mavuno mengi na uhakika wa kipato. 

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipotembelea skimu ya umwagiliaji ya wakulima wadogo wa mpunga (Uwawakuda) iliyopo Dakawa mkoani Morogoro leo (17.09.2020) ambapo serikali imetumia shilingi bilioni 24 kujenga miundombinu ya umwagiliaji. 

Akiwa kwenye skimu hiyo yenye ukubwa wa hekta 2000 alijionea miundombinu ya kisasa ikiwemo mfereji mkuu wenye urefu wa kilometa saba na mashamba ya wakulima yaliyovunwa mpunga. 

Katibu Mkuu huyo aliwapongeza wakulima hao kwa kuwa na kilimo bora cha umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa mpunga kufikia tani 7.2 kwa hekta mwaka 2019 toka tani 4.0 mwaka 2014. 

“ Nimefarijika kusikia wakulima sasa wanavuna magunia 35 hadi 40 kwa ekari mwaka 2019 tofauti na magunia 8 waliyokuwa wanavuna kabla miundombinu hii ya umwagiliaji haijajengwa na serikali kupitia Tume ya Umwagiliaji mwaka 2012 “ alisema Kusaya. 

Aliongeza kusema nia ya wizara ya kilimo ni kumkomboa mkulima ili siku moja tuwe na mabilionea wengi na uhakika huo utatokana na kulima kisasa kwa njia ya umwagiliaji na matumizi ya mbegu na pembejeo bora zenye gharama nafuu. 

Akiwa shambani hapo Kusaya alijionea uharibifu wa tuta la kuzuia maji nje ya shamba kuingia shambani ambapo eneo la ekari 384 ziliharibiwa na maji ya mafuriko mwezi Machi na Aprili mwaka huu na kusababisha baadhi ya wakulima kushindwa kulima mashamba yao. 

Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu huyo aliagiza Tume ya Umwagiliaji kupeleka mitambo na wataalam katika kipindi cha wiki mbili zijazo ili kufanya ukarabati wa tuta hilo ili maji ya mto Wami yaendelee kupita kwa utaratibu kwenye mashamba ya wakulima. 

Pia amewaahidi wakulima hao kuwa wizara yake inatafuta fedha shilingi bilioni mbili ili zitumike kuanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji awamu ya pili kwenye skimu hiyo ya Dakawa ambapo hekta 1000 ( sawa ekari 2500) zitafikiwa ili wakulima wengi zaidi wapate mashamba ya kuzalisha mazao. 

“ Tunalenga kama wizara kumkomboa mkulima toka kuwa na kilimo cha mazoea kinachotegema mvua hadi kuwa na kilimo cha kibiashara kwa kutumia umwagiliaji kote nchini hivyo tutaleta bilioni mbili ili zianze awamu ya pili ya mradi huu ” alisisitiza Kusaya 

Kusaya alisema uwepo wa miundombinu bora ya umwagiliaji ni mapinduzi makubwa katika kilimo kumwezesha mkulima kupata manufaa kwani lengo la wizara ni kufanya kilimo biashara ili kukuza uchumi wa taifa. 

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa wakulima wadogo wa mpunga Dakawa ( Uwawakuda ) Bertha Chilosa alisema wamenufaika na skimu hiyo ambapo sasa mahitaji ya eneo la mashamba yameongezeka sana. 

Alisema wanamshukuru Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa kusisitiza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa manufaa yake ni ya uhakika na wanyonge wananufaika na skimu hiyo ya Dakawa . 

“Kilimo kilikuwa kitu cha aibu lakini baada ya kuingia Rais Magufuli tumepata heshima kwa kuwa mazao yetu yanapata soko na pia skimu nyingi za wakulima zinakarabatiwa hali inayotuongezea uhakika wa kipato” alisema Bibi Chilosa ambaye pia ni mkulima kijiji cha Wami Dakawa 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji Mhandisi David Kaali alisema katika kutekeleza agizo la serikali kufikia hekta milioni moja mwaka 2025 za umwagiliaji wamejipanga kuendeleza mabonde ya kimkakati ya umwagiliaji yenye jumla ya hekta 110,000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. 

Tume pia imepanga kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Ziwa Victoria hekta 22,000 na kujenga na kukarabati skimu ndogo ndogo,za kati na kubwa zipatazo 384 mwaka huu. 

Akizungumzia mafanikio ya skimu ya umwagiliaji Dakawa Meneja wa ushirika wa Uwawakuda Abel Francis alisema uzalishaji mpunga umefikia takribani tani 14,400 kwa mwaka na zaidi ya ajira za muda mfupi kwa vibarua 5,000 toka Dakawa na maeneo ya jirani kipindi cha msimu. 

Alitaja changamoto iliyopo sasa ni ukosefu wa ghala la uhakika la kuhifadhia mazao ya wakulima na kutoa ombi kwa serikali kuwapatia mtambo wa kukoboa mpunga na ghala la (TANRICE Mills Ltd) ambalo lilibinafsishwa kwa mfanyabiashara lakini sasa halitumiki kijijini hapo.
    

0 comments:

Post a Comment